Sunday, March 11, 2012

Afande Sele arudi na roho yake

MSANII nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini, Seleman Msindi ‘Afande Sele’, amefyatua wimbo mpya uitwao ‘Nitarudi na Roho Yangu’ wakati akijiandaa kukamilisha albamu yake ya tano. Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, kwa njia ya simu kutoka Morogoro jana, Afande Sele, alisema katika kibao hicho amemshirikisha Abbas Hamis ‘20 Percent’. Afande Sele, ambaye miezi michache iliyopita aliachia kibao kingine kiitwacho ‘Maskini Hafulii’, alisema, amepanga kuongeza nyimbo kutoka kumi hadi 14 katika albamu yake ijayo. “Kaka nimeachia wimbo mpya unaitwa ‘Nitarudi na Roho Yangu’, nikiwa nakamilisha albamu yangu ya tano iitwayo ‘Kingdom’ ambayo itakuwa na jumla ya nyimbo 14 badala ya 10 nilizopanga kutoa awali,” alisema Afande Sele. Msanii huyo ambaye mwaka 2004 aliibuka Mfalme wa Rhymes, alizitaja baadhi ya nyimbo za albamu hiyo aliyowashirikisha wasanii mbalimbali nyota nchini kuwa ni ‘Kingdom’, ‘Maskini Hafulii’, ‘Soma Ule’, ‘Machozi ya Suzy’, ‘Nguvu na Akili’, ‘Dume’ na ‘Nikupendeje’. Albamu za mwanzo alizopata kuzitoa mkali huyo na ambazo zote zilitikisa katika ulimwengu wa muziki huo ni, 'Mkuki Moyoni' aliyoitoa mwaka 2001, 'Darubini Kali' mwaka 2004, 'Nafsi ya Mtu' mwaka 2006 na 'Karata Dume' ya mwaka 2008.

No comments:

Post a Comment