Saturday, December 1, 2012

HIVI NDIVYO VITU VYA MAREHEM SHARO MILLIONAIRE VILIVYOPATIKANA NA JESHI LA POLISI LAAPA KUKAMATA VILIVYOBAKI KWA WATU WENYE ROHO ZA KUTU



SHARO ENZI ZA UHAI WAKE
Kamanda Mkuu wa polisi Tanga Costantine Massawe
JESHI la Polisi mkoani Tanga limefanikiwa kukamata vitu mbalimbali vya marehemu Hussein Ramadhan, ‘Sharo Milionea’ vilivyoibwa na watu wasiojulikana, muda mfupi baada ya msanii huyo wa filamu na muziki nchini kupata ajali katika Kijiji cha Songa Kibaoni, wilayani Muheza na kufariki dunia papo hapo.


Baadhi ya vitu vya marehemu Sharo milionea vilivyokamatwa baada ya msako mkali baina ya Polisi na wananchi wa Kijiji Songa Kibaoni.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi mkoani Tanga, Costantine Massawe alisema Jeshi la Polisi limefanikiwa kukamata begi la nguo, simu ya mkononi aina ya blackberry, betri ya gari, redio, tairi la gari na saa ya mkononi ya marehemu.


Alitaja vitu vingine vilivyopatikana kuwa ni nguo ambazo marehemu alivuliwa baada ya kupata ajali, ambazo ni fulana na suruali ya jeans.


Alisema kuwa,vitu hivyo vilipatikana baada ya wakazi wa kijiji ilipotokea ajali hiyo kuvisalimisha vitu hivyo kwa Mwenyekiti wa Kijiji cha Songa kibaoni, Abdi Zawadi .


“Vitu viliwasilishwa na wasamaria wema kwa Mwenyekiti wa Kijiji cha Songa Kibaoni, Abdi Zawadi ambaye alitoa taarifa polisi kwa ajili ya utambuzi na taratibu nyingine,” alisema Massawe.


Aliwataka wananchi wa Kibaoni kuendelea kutoa ushirikiano ili viweze kupatikana vitu vingine vya marehemu na kuongeza kuwa, jeshi hilo linaendelea na uchunguzi, ili kubaini pesa na vitu vingine vilivyokuwamo ndani ya gari hilo ambavyo havikupatikana.




“Hivi vitu mnavyoviona hapa vimesalimishwa na watu ambao huenda walishiriki katika wizi, au waliviona mahali na kwa mapenzi yao kwa marehemu wakaamua kuvirejesha,” alisema Massawe


Alisema baadhi ya vitu hivyo vilikamatwa nje ya wilaya ya Muheza katika gereji na kwenye nyumba za watu.


Kamanda alifahamisha zaidi kuwa, hadi sasa watu kadhaa wanashikiliwa na jeshi hilo kwa kuhusika na tukio hilo.


“Tunaamini kuna vitu vingi vya thamani havijapatikana, bado tunaendelea na uchunguzi kwa kushirikiana na wananchi na mtu atakayekutwa na kitu chochote cha marehemu atashtakiwa,” alisema Massawe.


Alisema Jeshi la Polisi linawashikilia watu kadhaa waliokutwa na vitu hivyo, lakini hakutaja idadi yao kwa kuwa vitu vingine havijapatikana.


“Pamoja na hayo, vitu vilikuwa vinasalimishwa usiku na wengine walivileta mchana kwa mwenyekiti wao. Hata hivyo, si kwamba mtu aliyeleta anakamatwa papo hapo, ila wale watakaokutwa navyo tutawakamata na kuwashtaki,” alisema Kamanda Massawe.

habari kwa hisan ya http://haazu.blogspot.com/

No comments:

Post a Comment