Monday, August 25, 2014

UTALII KUTANGAZWA KUPITIA TONE RADIO

Baada ya kuona kuwa kuna maeneo mbalimbali ya vivutio vya kitalii muhimu na ambavyo vimesahaulika kwa njia moja au nyengine na pengine hakuna pa kuvitangaza ili watanzania na Dunia kwa ujumla wapate kuvifahamu kwa ukaribu , Tone Multimedia Group kupitia mtandao wake wa Mbeya yetu Blog wameamua kuanza rasmi kuvitembelea na kutangaza kwa Jamii kwa ujumla  wapate kuvifahamu ili nao waje kuvitembelea.

Safari hiyo ambayo moja kwa moja ilianzia Mkoa wa Mbeya Wilaya ya Rungwe-Tukuyu kwenda kujionea vivutio hivyo mbalimbali kikiwepo cha kwanza kabisa ambacho ni Kijungu eneo ambalo ni la kipekee na lenye historia ya aina yake.

Hivi ndivyo safari ilivyokuwa Fuatilia hapa kwa makini.
Kwanza kabisa tulifika katika kibao hiki ambacho kimetoa maelezo ya awali ikiwa ni pamoja na Bei ambazo mtu anatakiwa kutozwa wakati anapotaka kuingia katika eneo hilo, Bei hizo zimewekwa na uongozi wa Serikali ya Kijiji ambapo fedha hizo zinasaidia katika mambo mbalimbali za kuendeleza kijiji hicho ingawa hata hivyo kuna changamoto kadha wa kadha ambazo zinawakabili ikiwa ni pamoja ni Gharama kubwa za kuingia katika eneo hilo kwa wazawa ambapo haichagui kwamba umetoka nje ya nchi au ndani  Jambo ambalo Serikali inapaswa kutazama kwa sababu ni zaidi hata ya kuingia katika Hifadhi za Taifa.
Picha hii ilipigwa kwa juu kabisa kuonesha Jinsi eneo la Kijungu linavyo onekana 
Hapa ni eneo ambalo Maji ya mto huo yanatokea katika eneo linaitwa Namba One eneo la ukanda wa juu kabisa wa eneo hilo, Majihayo pamoja na mengine mengi hata wakati wa mvua kubwa ni lazima yazunguke yanapo kwenda lakini mwisho wa siku ni lazima yaishie hapa, Pia hapa ndipo maji haya yanapoanza kutililikia moja kwa moja katika kijungu.
Maji hayo sasa huingia katika eneo hili la kijungu, Wamekiita jina la kijungi kwa sababu kubwa kuwa eneo hilo lipo kama chungu, Maji hayo hata yakiwa na kasi kiasi gani, hata yawe mengi kwa namna gani hayawezi kujaa katika Kijungu hiki, Pia kijungu hiki hakuna mtu aliyekijenga bali ni maajabu tuu ya uumbaji wa Mwenyezi Mungu, hilin eneo limeumbwa kwa miamba ya mawe yanayofanana na Chuma kigumu. Maji haya yakishafika hapa huwa si mwisho kuna eneo yanaelekea..kwa hakika ni maajabu na kama huna wazo la kutembelea ni wakati wako sasa.
Kulia ni upinde unao onekana kutokana na kasi ya maji, upinde huu ni kivutio kikubwa hasa wakati wa jua kali huonekana vizuri
Tulipo wasili katika eneo hilo la kijungu tulipata wasaa wa kuongea na Mzee mmoja wa zamani sana ambaye kwa hakika yeye alikiona kijungu zamani sana miaka yani miaka ya 1933 , mzee huyo ambaye anatambulika kwa jina la Elia Kabadhasya aliye  zaliwa mwaka 1927 alieleza kwamba alikijua kijungu hiki wakati alipokuwa akitafuta sehemu ya Kunyweshea Ng'ombe Maji ndipo aliposhuka eneo hili na kukiona Kijungu hiki, hata hivyo wakati anawanywesha maji Ng'ombe wake kwa bahati mbaya moja kati Ng'ombe hao alitumbukia ndani ya kijungu hicho na kupotea moja kwa moja. Wa kwanza kutoka kushoto ni Joseph Mwaisango Mwandishi mkuu wa Mbeya yetu Blog na wa Kwanza kutoka kulia ni Fredy Anthony Njeje kutoka Tone Multimedia group akiwa anachukua maelezo kwa makini ya Mzee Elia Kabaghasya wa kati kati.
Baada ya maji hayo yenye kasi ya ajabu kuingia katika kijungu hicho hutokea katika eneo hili ambapo yanaonekana meupe na yenye mapovu . hii ni kutokana na sababu ya kwamba yanakuja kwa kasi na kufikia hapa, baada ya kufika hapa mbele kunaonekana kwamba kuna  uwazi, uwazi huu kwa mujibu wa wanakijiji wanaotokea eneo hili wanasema kwamba maji haya huingia hapa katika uwazi ambao unakadiliwa kuwa  na urefu kwa Kilometa moja husafiri huko na baadae hutokea katika upande mwengine ambapo ukitazama vizuri katika picha hiyo kwa mbele ya haya maji kuna maji yamepoa hayana kasi hapo ndipo yanapo tokea, hakuna yanapo kutana haya maji mpaka yaingie pangoni ndio yatokee upande wa pili, hii itaonekana katika picha inayofuatia, hili ni moja ya ajabu kwa sababu waweza dhania haya maji yanakutana kumbe hayakutani hata kidogo.
Picha hii inaonesha vizuri na ni mwendelezo ya wa maelezo ya maji hayo hapa kama inavyo onekana upande wa juu ni kijungu maji ambapo yanaingilia hapo kisha yanatokea upande huo wa pili yanapoonekana meupe sana na povu kutokana na povu kisha yanaingia katika pango hilo linalokadiliwa kuwa na Kilometa moja kisha yanatokea upande wa pili hapo yanapo onekana kama yamepoa kisha kuendelea na safari , Cha ajabu maji hayo hayakutani hata kidogo.
Fredy Anthony Njeje Kutoka Tone Multimedia Group ambao ni wamiliki wa Mtandao huu wa Mbeya yetu  wa upanda wa kulia akipata maelezo zaidi ya Kina kuhisiana na Kijungu hiki kutoka kwa Mzee Elia Kabaghasya mwenye umri wa Miaka 87 sasa mzee mwenye nguvu na  ambaye anajua historia nzima ya eneo hili la kijungu alieleza kwamba hili ni eneo zuri sana la utalii ambapo aliwataka watu wengi zaidi waje kutembelea katika eneo hili na kujionea mambo mengi zaidi na Maajabu ya Mungu ya eneo hilo la kipekee ambalo kwa Tanzania hata kwa Dunia ni hapo tuu ndipo papo hivyo, Alieleza zaidi kwamba maji hayo ya mto huo hutumika zaidi kwa ajili ya kunyweshea mifugo, na kufulia tuu hayatumiki kwa kazi zengine. Alitoa wito kuwa watu wanatakiwa kuwa makini wanapokuja kutembelea eneo hilo na kuchukua tahadhali kama maeneo mengine kwa kuwa mtu anaweza teleza ingawa eneo hilo kuna wataalam na watu maalum wa kuwaongoza. alimalizia kwa kusema kuwa kuna haja ya Serikali kukiboresha Kivutio hiki cha Kijungu.
 Mmoja wa wanakijiji ambao wanaishi katika eneo hilo akipita njia kati kati ya Kijungu hicho na kusema  kwamba zamani kutokana na imani za mababu zetu ilikuwa ili upite ni lazima utumbukize kitu chini ndio upate kupita hapo, lakini kadili siku zinavyozidi kwenda na hivi miaka ya karibuni imani hiyo imetoweka na mtu anaweza kupita bila shida, pia alisema kwamba katika eneo hilo mtu anapokatiza katika mwamba huo katikati anatakiwa aanze kutanguliza mguu wa kulia kwanza ndio anaweza akavuka. Mwisho alisema kwamba ukivuka upande wa pili unatokea moja kwa moja mpaka Uporoto ingawa ni parefu hivyo mababu zetu ndio njia walikuwa wakipita enzi hizo.
Kikosi kazi cha Mbeya yetu kazini
 Mzee Elia Kabaghasya (87) akionesha eneo ambalo anaishi halipo pichani kuwa maji hayo yamefika mpaka eneo hilo nyumbani kwake.
Kutoka kushoto ni Joseph Mwaisango akiwa katika picha ya pamoja na Baadhi ya waliofika eneohilo ambao ni Doreen, Ruby, Happy na Eric  kufanya utalii wa ndani.

******
Inawezekana umehamasika na unataka na wewe kufika katika eneo la Kijungu kujionea wewe mwenyewe kwa macho yako na haya ndio maelekezo.

Namna ya kufika
Kutoka Mbeya Mjini hadi Sehemu moja inaitwa KK Wilaya ya Rungwe-Tukuyu ni zaidi ya Kilometa 50 , Baada ya hapo kuna njia ambayo inakatiza upande wa kulia kuelekea Chuo cha Magereza, Ukifika Chuo cha Magereza ndani utapata maelekezo yote ya namna utakavyofika, Muhimu kufuata taratibu maana ni eneo la Jeshi la Magereza kuna sheria zake. 

MAONI 
Baada ya kutembelea na kujionea wenyewe tulikuwa tunaomba Serikali iangalie swala zima kwanza la Afya za hawa wanaotembelea katika Kivutio hiki cha kitalii, kwamba hakuna sehemu ya watu kijisaidia-Choo hivyo inawalazimu watu wajisadie hovyo hovyo katika vichaka jambo linalosababisha uchavuzi wa mazingira na pengine inaweza sababisha mripuko wa magonjwa, Hilo ni swala muhimu.

Pili ni swala la mapato tumejionea kwamba kwanza hakuna Risiti inayotolewa wakati watu mbalimbali wanaenda kutembelea katika kivutio hicho cha Kijungu, Kila mtu anajiwekea bei zake ingawa wameweka Bei ya kutazama pale ni Tsh 5,000 kwa mtu ambapo hicho ni kiasi kikubwa kwa wazawa na inabidi hapa paangaliwe, na kwamba mwanakijiji yoyote ambaye yupo eneo hilo ndiye anayetoza watu, utaratibu huo unatakiwa kuangaliwa na kutengenezwa vizuri na kurekebisha viwango hivyo kwani watu wanapenda kuona lakini wanashindwa, Pia mapato hayo yanaonekana hayana msaada wowote kwa wakazi wa eneo hilo.

Tatu ni Miundombinu ya eneo hilo, ambayo inatakiwa kuboreshwa zaidi hasa eneo la kuingilia hapo Serikali itazame waweke hata ngazi kuanzia eneo la kuingilia mpaka hapo katika Kijungu ili watu waweze kufika kiurahisi 

Mwisho Serikali iangalie jinsi gani wanaweza kuweka Ofisi ili hata watu wanapofika waelewe kabisa kwamba sasa wamefika katika kijungu na kupata maelekezo yote ya awali kabla ya kwenda katika eneo la tukio.

Ikiwa unapenda kujua na kuungana nasi katika mpango huu wa kutangaza vyanzo hivi muhimu wasiliana nasi kwa namba +255 754 374 408 au +255 765 056 399

Imeandaliwa na Tone Multimedia Group kupitia Mtandao wake wa Mbeya yetu Blog, Huu ni Mwanzo bado kuna Mengi sana  usikose Kujua juu ya Maporomoko ya Kaporogwe  ambapo ndipo tutawaletea hapa usikose.

No comments:

Post a Comment