Friday, December 12, 2014

Hofu ya TZ kunyimwa msaada na Marekani



Mbunge Zito Kabwe mwenyekiti wa kamati iliyowasilisha ripoti kuhusu sakata ya Escrow

Serikali ya Tanzania iko hatarini kukosa dola za Marekani milioni mia saba sawa na trilioni 1.1 kwa fedha za Tanzania kwa ajili ya mradi wa pili wa mfuko wa changamoto za Milenia (MCC) kutokana na kushamiri kwa vitendo vya rushwa nchini humo.
Marekani imebainisha kuwa mkataba wa pili wa miradi inayofadhiliwa na shirika lake la Changamoto za Milenia (MCC) utategemea hatua zitakazochukuliwa na serikali ya Tanzania dhidi ya wahusika wa kashfa hiyo.
Haya yanajiri wakati Rais Jakaya Kikwete akisubiriwa kutoa maamuzi ya mapendekezo yaliyofikiwa na Bunge kuhusiana na sakata la uchotwaji fedha zaidi ya Sh. bilioni 300 kutoka kaunti ya Tegeta Escrow wiki ijayo.
Katika tamko hilo kwa umma ambalo limewekwa kwenye tovuti ya MCC, bodi ilieleza kutambua umuhimu wa kusubiri na kuona utekelezaji kamilifu wa tamko lililotolewa na Ikulu ya Tanzania Desemba 9, mwaka huu kwamba itachukua hatua za haraka na kutoa maamuzi dhahiri na thabiti kuhusu maazimio ya Bunge juu la suala la IPTL.
Taarifa iliyotolewa na Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania ilieleza kuwa wakurugenzi wa MCC waliokutana katika mkutano wao uliofanyika Desemba 10, mwaka huu wamesikitishwa na hali ya rushwa nchini Tanzania.

Bunge la Tanzania kikaoni
Uamuzi huo wa Marekani ambayo inafadhili miradi mingi ya mabilioni ya fedha ni mtihani wa pili kwa Rais Kikwete baada ya ule wa maazimio ya Bunge yaliyotaka viongozi wakiwamo mawaziri waliotajwa katika kashfa hiyo kuwajibishwa.
Wanaotakiwa kuwajibishwa na Rais Kikwete ni Waziri wa Nishati na Madini, Profesa, Sospeter Muhongo na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka.
Wengine ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakimu Maswi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema.
Novemba mwaka huu, Serikali ya Marekani kwa kupitia MCC, ilikubali kutoa ruzuku ya hadi Dola za Kimarekani milioni 9.78 kwa ajili ya maandalizi ya miradi ya uwekezaji yenye matokeo makubwa katika sekta ya nishati nchini.
Tanzania ilikuwa mojawapo ya nchi kumi zilizojadiliwa na Bodi ya MCC iliyokutana kuangalia kama nchi hizo zimekidhi vigezo vya kuendelea na mchakato wa kuandaa mikataba mipya.
Wakati wa mkutano wa 16 na 17 wa Bunge, Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi), alidokeza kusudio la Marekani kukataa kutoa fedha kwa ajili ya miradi ya MCC, lakini Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alikanusha taarifa hizo.
Juhudi za BBC kumtafuta Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Mark Childress,aweze kuzungumzia juu ya ripoti hiyo ziligonga mwamba kutokana na sababu za kiprotokali .

No comments:

Post a Comment