Tuesday, July 21, 2015

Kenya kumkaribisha Obama katika bara linalohisi kubaguliwa


Wakati Rais wa Marekani atakapokuwa ziarani barani Afrika, atapokewa na bara lililotarajia kuwa na mahusiano ya karibu na mtu waliyedai ni kijana wa nyumbani, katika kijiji alikozikwa baba wa rais wa 44 wa Marekani.
Rais wa Marekani Barrack Obama
Rais wa Marekani Barrack Obama
"Tulidhani serikali ya Marekani angalau italeta usaidizi katika eneo hili," alisema Stephen Okumu Obewa, mwalimu katika shule ya msingi ya Senator Barack Obama mjini Kogelo. Shule hiyo ilipewa jina hilo hata kabla ya rais Barrack Obama kuingia ikulu. "Labda bado ana nia hiyo lakini sisi hatujui," alisema Okumu alipokuwa katika shule hiyo ambapo madawati na viti vingi vilikuwa vimevunjika.
Obama aliwahi kuandika juu ya ziara yake kijijini Kogelo katika kitabu chake mwaka 1995 kilichopewa jina "Dreams from My Father", yaani "Ndoto kutoka kwa Baba yangu" kilichomsaidia kuanzisha safari yake ya kisiasa.
Kijiji hicho pole pole kikaanza kupata umaarufu, watalii wakaanza kukitembelea huku wageni wa kila aina wakionekana kubisha hodi mlangoni mwa bibi yake wa kambo, Mama Sarah.
Bibi yake Barrack Obama, Mama Sarah
Bibi yake Barrack Obama, Mama Sarah
Karibu sana na kijiji hicho, kuna kaburi la baba yake Barack Obama mwenyewe, mwanauchumi katika serikali ya Kenya aliyefariki kutokana na ajali ya barabarani mwaka wa 1982, ikiwa ni miaka 21 baada ya rais kuzaliwa wakati alipokuwa akiishi Hawaii kama mwanafunzi.
Hata hivyo, Wakenya wengi wanashangaa ni kwa nini Rais Obama hajatoa kipaumbele katika maendeleo ya bara la Afrika kwa mihula miwili ya uongozi wake.
"Wakati alipochaguliwa kulikuwa na hamu kubwa na matumaini kuwa mahusiano ya Marekani na bara la Afrika yataimarika kwa kiwango kikubwa na kwamba Marekani itaelekeza nguvu zake katika bara hilo, lakini rekodi ya mambo hayo ni ndogo mno," alisema David Zounmenou, mtafiti katika taasisi moja ya masuala ya Usalama nchini Afrika Kusini.
Obama asema anatoa kipaumbele kwa eneo zima na sio tu Kenya
Rais Barrack Obama
Rais Barrack Obama
Obama ataitembelea Kenya na Ethiopia mwezi Julai ikiwa ni ziara yake ya tatu kubwa katika eneo hilo la jangwa la Sahara, baada ya kusafiri Ghana mwaka wa 2009 na nchini Tanzania, Senegal, na Afrika Kusini mwaka wa 2011. Obama pia aliwahi kuitembelea Misri, na Afrika Kusini wakati wa maziko ya moja ya shujaa wa Afrika Marehemu Nelson Mandela.
"Matumaini yangu ni kutoa ujumbe kuwa Marekani sio tu mshirika mkubwa nchini Kenya bali kwa eneo zima la Jangwa la Afrika," alisema Obama wiki iliyopita. Aliongeza kuwa anatumai kujenga maendeleo katika masuala ya afya, elimu, kukabiliana na Ugaidi na kuhimiza demokrasia na kupunguza rushwa.
Kwa upande wao maafisa wa Marekani wamesema muonekano wa kuwa Rais Obama amelitelekeza bara la Afrika sio jambo zuri la kusemwa, wakitiliana maanani juhudi za marekani za kukabiliana na ugonjwa hatari wa Ebola, katika mataifa ya Afrika Magharibi na mpango uliozinduliwa mwaka wa 2013 wa dola bilioni 7 wa kusambaza umeme barani Afrika.
Wakaazi mjini Kogelo alikozaliwa babake rais Obama
Wakaazi mjini Kogelo alikozaliwa babake rais Obama
Lakini huku hayo yakiarifiwa balozi wa Marekani Robert Godec amesema rais Obama hatokitembelea kijiji cha Kogelo, na kuwa badala yake atawahutubia watu wa Kenya katika uwanja wa Nairobi mnamo Julai 26.
Lakini licha ya hayo wakaazi wa Kogelo bado wanajitayarisha kumpokea kijana wao iwapo ataamua kuwatembelea. Wakaazi wa eneo hilo bado wako katika harakati pia za kusafisha kaburi la babake rais huyo wa Marekani.
"Milango yako wazi usiku na mchana kwa rais Obama," alisema Mashart Onyango, anayeishi katika boma la familia ya Obama aliyesema ni mmoja wa shangazi zake baba yake Obama.
Muandishi: Amina Abubakar/Reuters

No comments:

Post a Comment