Monday, June 6, 2016

MAREKANI KUIPA TANZANIA DOLA MILIONI 800KWAAJILI YA MIRADI YA MAENDELEO



Marekani itatoa dola milioni 800 kwa Tanzania kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
Balozi wa Marekani nchini Tanzania Mhe. Mark Childress aliyekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amesema kutolewa kwa fedha hizo ni uthibitisho kuwa kutotolewa kwa fedha za awamu ya pili ya mradi wa changamoto za milenia (MCC-2) hakujaondoa uhusiano na ushirikiano wa Tanzania na Marekani ikiwemo utoaji wa misaada ya maendeleo.
"Tumezungumza mambo kadhaa, na wiki hii Tanzania na Marekani kupitia shirika letu la misaada la USAID tunatarajia kutiliana saini mkataba wa zaidi ya dola milioni 400 kwa ajili ya mwaka ujao, pia tumezungumza kuwa kutakuwa na dola milioni 800 zitakazotolewa na Marekani kwa ajili ya miradi mbalimbali na hii haihusiani na MCC.
"Ukweli ni kwamba tunayo mengi ya kufanya pamoja katika sekta mbalimbali zikiwemo afya, elimu na kilimo na tutafanya kila juhudi kuhakikisha haya yanafanikiwa" Amesema Balozi Mark Childress muda mfupi baada ya kumaliza mazungumzo na Rais Magufuli.
Kwa upande wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amesema serikali yake ya awamu ya tano itaendeleza na kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano na Marekani na kwamba fedha za msaada kutoka Marekani ni muhimu kwa maendeleo ya Tanzania.
"Amekuja kutuhakikishia kwamba watatoa hela kwa ajili ya Tanzania na anasema sasa hivi watatoa zaidi ya dola milioni 800, na mkataba mwingine tunaweza tukasaini hata kesho wa dola milioni 410, anasema kutotoa hela za MCC hakuna maana kupotea kwa urafiki wa Tanzania na Marekani, urafiki wa Tanzania na marekani upo pale pale na sasa wanaongeza hela nyingi zaidi katika kuonesha kwamba juhudi za HAPA KAZI TU zinaendelea" amesema Rais Magufuli.
Wakati huo huo Rais Dkt. John Pombe Magufuli leo amekutana na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ubelgiji Mhe. Didier Reynders Ikulu Jijini Dar es salaam, ambapo viongozi hao wamezungumzia kuendeleza na kuimarisha uhusiano baina ya nchi hizi mbili hususani katika maendeleo.
Pamoja na kuzungumzia miradi ya ushirikiano inayotekelezwa kati Tanzania na Ubelgiji katika mkoa wa Kigoma, viongozi hao pia wamekubaliana kuongeza ushirikiano katika biashara na uwekezaji ambapo Mhe. Didier Reynders ameahidi kushawishi kampuni nyingi za Ubelgiji kuja kuwekeza hapa nchini.
Katika hatua nyingine Rais Magufuli ameagana na Balozi wa Italia hapa nchini Mheshimiwa Luigi Scotto ambaye amemaliza muda wake wa miaka mitatu.
Balozi Luigi Scotto amesema katika kipindi chake amewezesha kuongezeka kwa biashara kati ya Italy na Tanzania kwa asilimia 35 na ameielezea Tanzania kuwa ni nchi nzuri aliyoipenda na kwamba ataendelea kutangaza fursa zilizopo Tanzania huko Italia na kwingineko.
Mapema leo asubuhi, Rais Dkt. John Pombe Magufuli ametia saini kitabu cha maombelezo katika Ofisi ya Ubalozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Nchi za Kiarabu ya Saharawi iliyopo Mikocheni Jijini Dar es salaam, kufuatia kifo cha Rais wa nchi hiyo Mohamed Abdelaziz aliyefariki dunia Jumanne iliyopita tarehe 31 Mei, 2016.
Rais Magufuli ambaye amepokelewa na Balozi wa Saharawi hapa nchini Mhe. Brahim Salem Buseif amesema Marehemu Mohamed Abdelaziz ambaye pia alikuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Polisalio Front, atakumbwa kwa juhudi zake za kupigania ukombozi na uhuru wa Saharawi.
"Kwa niaba ya Serikali na wananchi wa Tanzania napenda kutoa salamu zangu za pole kwa Serikali na wananchi wa Saharawi kwa kumpoteza kiongozi ambaye alijitoa kwa ajili ya kupigania ukombozi na uhuru wa Jamhuri ya Saharawi.
"Namuombea kwa Mwenyezi Mungu, aipumzishe roho yake mahali pema peponi, Amina" Amesema Dkt. Magufuli katika salamu hizo.

No comments:

Post a Comment