Wednesday, May 23, 2012

Shibuda: Chadema si ya malaika






MBUNGE wa Maswa Magharibi, John Shibuda amesema Chadema si chama cha malaika na kuelezea kushangazwa na wanaokasirika chama hicho kinapokosolewa.

Kiongozi huyo wa Chadema mwenye ushawishi mkubwa katika siasa za Kanda ya Ziwa, alisema hayo juzi katika Kanisa la Wadventista Wasabato mjini hapa alikoalikwa kuwa mgeni rasmi katika harambee ya uzinduzi wa kwaya ya Ushirika katika Kanisa hilo.

Shibuda alisema ameshangaa anapokosoa Chadema na watu kukasirika akasisitiza nia yake ya kugombea urais mwaka 2015 kupitia chama hicho, huku akidai Meneja wake wa Kampeni akiwa Rais Jakaya Kikwete ambaye wakati huo atakuwa amemaliza muda wake wa urais.

“Hivi mtu akigombana na Askofu ina maana atakuwa ameikataa Biblia? Mimi sina ugomvi na Chadema, ingawa nikisema jambo wananisonga sana, mbona hata Mwalimu Julius Nyerere alimpigia kampeni mpinzani kutoka NCCR- Mageuzi lakini hatukusikia manung’uniko yoyote kwa kuwa yeye aliona ni bora kuliko walioko ndani ya chama chake.

“Sasa baada ya minong’ono ya chini chini kusikika, kwamba nitawania urais ifikapo mwaka 2015 sasa nia ninayo na wakati umefika …kama kuna mtu ana nia ya kugombea urais, ajitokeze bila woga na dhana ya kusema kabila kubwa halifai kupewa urais hiyo ondoeni,” alisema Shibuda.

Alitaka Watanzania wamwelewe kuwa ana nia ya kuwania urais na kuvitaka vyombo vya habari nchini vitangaze maovu yake yote bila kuficha.

Alifafanua kuwa hata Rais akiona Chadema imesimamisha mtu dikteta au asiye imara, hatafurahi, lakini chama hicho kikisimamisha mtu imara kuliko wa CCM, lazima atapiga kampeni achaguliwe aliye bora na ndiyo maana hakuna kosa.

Mbali na Shibuda, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto pia alishatangaza kuwa urais anautaka. Mbali na hao, wanasiasa wengine waliokwisha pendekezwa na kugombea urais ni Mwenyekiti Freeman Mbowe (2000) na Katibu Mkuu Dk. Willibrod Slaa (2010).

Shibuda, ambaye alipata kuwa Mbunge wa CCM na kisha kutangaza kuwania urais kwa tiketi ya CCM mwaka 2005 na 2010, alisema hapendi Chadema wala CCM vife.

Alifafanua kuwa anataka vyama hivyo viwepo ili vilete changamoto na kushauri viongozi wa Chadema wapewe semina elekezi ya kujitathmini kuhusu utawala bora na siasa safi kama ilivyo CCM.

“Kuhusu suala la posho kuongezwa kwa wabunge, kipindi hicho mimi niliona sawa ziongezwe… nikaibe? Lakini likawa gumzo kuwa nimekiuka taratibu za Chadema, likawa kosa kwangu, wakati walikuwapo waliosema iongezwe ndani ya chama hicho hawakuchukuliwa hatua yoyote ila ni mimi tu,“ alisema.

Akizungumzia uongozi wa chama hicho, Shibuda alitaka chama hicho kiachane na ubaguzi wa kupendelea baadhi ya viongozi ndani ya chama na kifanye siasa za kweli kwa kujitetea pamoja na wananchi ili kifikie malengo kusudiwa.

Alinyooshea kidole Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) kuwa halikutenda haki kutangaza kupitia vyombo vya habari kuwa lilimjadili, lakini sasa viongozi wake wanapingana.

"Sasa Bavicha iseme Chadema ikiingia madarakani itakuwa na kanuni gani? Wazitaje ili tufahamu zinazotakiwa au jinsi ya kuzungumza.

“Mbona sikuona Baraza hilo likitetea vijana wa Maswa walipokamatwa na kuwekwa gerezani miezi kumi? Sikuona hata kiongozi wa Bavicha akitembelea na kutoa msaada wa sabuni kama si pole, isipokuwa Mabere Marando niliyemwita tukashirikiana wakatoka," alisema.

Alisema Bavicha inataka chama hicho kiendeshwe kwa mfumo wa kimagereza wa kutaka kumjua mnyampara wa gereza ni nani atakayeamua anavyotaka yeye na kuonya kuwa tabia hiyo itavunja demokrasia ya chama hicho.

 

No comments:

Post a Comment