DAKIKA CHACHE KABLA YA KIFO CHA DAVID MWANGOSI
ASKARI
polisi aliyefyatu bomu lililomlipua na kumuua kinyama mwandishi wa
habari wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, David Mwangosi (40),
amejulikana.
Tayari
mazishi ya masalia ya mwili wa Mwangosi yamefanyika jana katika
Kijiji cha Busoka, Kata ya Itete, Wilaya ya Rungwe, mkoani Mbeya, huku
ndugu, waandishi wa habari, wachungaji na wananchi wengine
wakililaumu Jeshi la Polisi kwa mauaji hayo, na kwa kushindwa
kuwachukulia hatua askari polisi waliosababisha kifo hicho na jina
baya la jeshi hilo.
Picha
zilizopigwa kwenye tukio la mauaji hayo, zinaonyesha askari wakiwa
wamemzingira na kumpiga Mwangosi, baadhi yao wakiwa na virungu, na
wengine bastola. Mmoja miongoni mwao, ameshikilia bunduki na kuielekeza
tumboni.
Kutoka mazikoni,
habari zinasema kuwa haikuwa kazi ndogo kuzuia vilio na simanzi
zilizoonyeshwa na umati mkubwa wa waombolezaji waliofika kushuhudia
mwili wa marehemu Mwangosi ulioharibiwa vibaya ukionyeshwa baada ya
Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Usharika wa
Busoka, Mathayo Mwantemanie kuongoza ibada ya mazishi.
Kifo
cha mwandishi huyo ambacho kimevuta hisia za wananchi wengi ndani na
nje ya nchi, hususani wakazi wa Wilaya ya Rungwe, kilimgusa kila mmoja
akiwemo Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),
Dk. Willibrod Slaa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais asiye na wizara
maalum, Profesa Mark Mwandosya na mkewe, Lucy Mwandosya waliofika
nyumbani kwa marehemu.
Profesa
Mwandosya alieleza jinsi msiba wa Mwangosi ulivyomgusa, kumuumiza
moyo na kumfanya ashindwe kujizuia kutoa machozi kwani tayari
alishapoteza wazazi wake wote wawili miaka michache iliyopita.
“Ni
vigumu sana kwangu kuzungumzia hali hii, Mwangosi ameniuma sana,
nimezunguka naye sana, nimefanya naye kazi kwa karibu sana, nimepotelewa
na kijana wangu, mtoto wangu, mwenzangu katika kazi, kila nilipokuwa
naye alinipiga sana maswali na mengi yalikuwa ya msingi,” alisema Profesa Mwandosya.
Kwa
upande wake, Dk. Slaa ambaye alikuwa kwenye msafara wa kusafirisha
mwili wa marehemu, alieleza mazingira ya kifo hicho na kusema msiba
hauna itikadi, dini wala rangi, na kubeza kauli za ubaguzi dhidi ya
msiba wa mwanahabari huyo.
Alisema
CHADEMA itahakikisha haki ya Mwangosi haipotei na kuongeza kuwa
binadamu si kuku, kwani damu yake lazima ipiganiwe kwa haki na kueleza
jinsi chama hicho kinavyoshtushwa na vitendo vinavyofanywa na serikali
dhidi ya vyombo vya habari, hususani kulifungia gazeti la MwanaHALISI
na sasa wameamua kupoteza maisha ya mwanahabari huyo.
Naye
Mchungaji wa Kanisa la Kilutheri, Dk. Steven Kimondo na Mhadhiri wa
Chuo Kikuu cha Tumaini Idara ya Thiolojia, aliuliza umati huo baada ya
kusema kuwa Jeshi la Polisi linahusika na mauaji ya Mwangosi.
“Akili
yangu inakataa kusema uongo kuwa Jeshi la Polisi halihusiki na tukio
la kifo hiki, vitendo hivi vya mauaji ya raia wasiokuwa na hatia
vinajenga chuki kwa wananchi dhidi ya serikali yao na kwamba lazima
uchunguzi ueleze ukweli kuwa marehemu hajafa kifo cha Mungu isipokuwa
binadamu wamehusika,” alisema Dk. Kimondo.
Dk.
Slaa alitoa ubani wa sh milioni 2, Mbeya Press Club (sh 700,000),
Iringa Press Club (sh 1,750,000), MISA-Tan (sh 500,000), huku Profesa
Mwandosya akiahidi kumsomesha mtoto mkubwa wa marehemu ambaye yupo
kidato cha nne na wadogo zake, na alitoa ubani wa sh 500,000.
No comments:
Post a Comment