TAARIFA KWA UMMA/VYOMBO VYA HABARI
Tasisi
ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Nchi za Kusini mwa Afrika (MISA Tan)
imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha mwandishi na
kiongozi mahiri wa waandishi hapa nchini.
Aidha
tunaungana na waandishi na wafanyakazi katika tasnia ya habari nchini,
Jumuiya ya Klabu za Waandishi nchini (UTPC) pamoja na familia ya
marehemu Mwangosi katika kipindi hiki kigumu ambacho tasnia yetu ya
habari imelazimika kuingia matatani kutokana na matumizi ya mabavu ya
Jeshi la Polisi.
Tunalaani
kwa nguvu zote matumizi ya mabavu ya polisi ambayo yamesababisha kifo
cha mwandishi wa habari akiwa kazini na pia akiwa chini ya ulinzi wa
Polisi. Tunatambua uhasama kati ya Polisi wa mkoa wa Iringa dhidi ya
waandishi wa habari uliodumu kwa muda mrefu.
Uhasama
huu kiini chake ni kutokana na matumizi ya nguvu kupita kiasi
yanayotekelezwa mkoani Iringa na hivyo kila mara waandishi wanaporipoti
habari wanaingia katika mlolongo wa uhasama na vituko vya mara kwa mara.
Hatimaye polisi kwa makusudi wameamua kuua mwandishi. Hili ni doa
ambalo litaichukua Tanzania kujisafisha machoni pa jumuiya ya kimataifa.
Huu ni mwendelezo wa matumizi ya nguvu kupita kiasi yanayofanywa na polisi kwa raia wa nchi hii.
Ni lini polisi watasimamia ulinzi wa raia na mali zao badala ya kugeuka
kuwa jeshi la mauaji kila wananchi wanapokusanyika kwa minajili ya
kutimiza ndoto zao?
Kifo
cha Mwangosi kimegubikwa na sintofahamu hasa ukijua kuwa Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Iringa Bwana Michael Kamuhanda alikuwa anamtambua kama
kiongozi wa waandishi wa habari mkoa na alikuwepo kwenye tukio wakati
Mwangosi akiwa mikononi mwa polisi, na kuuliwa mbele yake.
Lakini
ikumbukwe kuwa siku zote hata katika vita waandishi wanafanya kazi bega
kwa bega na askari ili kuwajuza wananchi nini kinachotokea kwenye
uwanja wa mapambano. Kwa jeshi la polisi hapa nchini limedhihirisha kuwa
baada visa na mikasa kuwatokea raia wa kawaida sasa wamewageukia
waandishi wa habari na kukatisha maisha yao kikatili.
Sasa
Polisi wamevunja daraja lililokuwa linawanganisha wananchi na serikali
yao. Hii itazidisha chuki ya wananchi dhidi ya serikali yao kuliko
kipindi kinginecho chote.
Ikumbukwe
pia kuwa wakati mauaji haya yanatokea kuna mkutano mkuu wa UTPC
unaoanza wiki hii huku wawakilishi wa vyama vya waandishi wa mbalimbali
wa kimataifa wakitegemea kushiriki katika mkutano huo wa mwaka. Na hii
itatoa taswira halisi ya jinsi Jeshi la Polisi linavyofanya kazi hapa
nchini.
Jumuiya
ya kimataifa itaweza kujionea hali halisi jinsi waandishi wa habari
hapa nchini wanavyofanya kazi katika mazingira hatarishi na kwamba sasa
Tanzania inawezekana isiwe mahali salama pa kuishi kama walivyokuwa
wakisikia kwenye vyombo vya habari vya kwao. Mfano halisi ni mhanga
Daudi Mwangosi ambaye ataingia katika vitabu vya kumbukumbu duniani kwa
mwaka 2012.
Tunaiomba
serikali ichukue maamuzi makini ya kukaa pamoja na vyama vya siasa ili
kutafuta njia muafaka ya kutuliza mikusanyiko ya wananchi kwa njia za
amani na sio kutumia mabavu katika kuwatawanya.
Ni
imani yetu kuwa historia imeonyesha kuwa nguvu kupita kiasi kwa
wananchi inaongeza chuki dhidi ya serikali yao ya wakati huo na kamwe
hainyamazishi dukuduku zilizoko mioyoni mwa wananchi. Kokote kule
duniani matumizi ya polisi yalipovuka mipaka yakaamsha hasira za
wananchi na kuzifanya nchi hizo zisikalike.
Matumizi
ya mabavu, nguvu kupita kiasi kuzima vuguvugu za wananchi kwa kile
wanachokiamini pamoja na mauaji na hasa kwa wanahabari na raia wasio na
silaha hayajawahi kufanikiwa kokote kule duniani.
Tunaamini
kuwa serikali yetu ni sikivu na itachukua hatua stahiki. Pamoja na
kwamba uchunguzi huru sio utamaduni wa serikali yetu lakini katika hili
la mwandishi akiwa na kalamu na kamera yake afie mikononi mwa polisi
tunahitaji uchunguzi huru na wa kina.
Taasisi
yetu imetoa ubani wa shilingi laki tano (500,000/-) kwa familia ya
marehemu Mwangosi. Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi. Amen!
Tumaini Mwailenge
Mkurugenzi,
MISA Tanzania
No comments:
Post a Comment