Wednesday, November 14, 2012

DRC inataka UN kuadhibu Rwanda



Sultani Makenga.
Sultani Makenga.
Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo imetoa wito kwa Umoja wa Mataifa kuichukulia hatua Rwanda, kwa madai ya kusaidia waasi nchini Congo badala ya kumfuatilia mtu mmoja kama vile kanali Sultani Makenga.
Waziri wa habari wa serikali ya Congo amesema hayo siku moja baada ya Umoja wa Mataifa na Marekani kutangaza vikwazo dhidi ya kiongozi wa waasi wa M23, Jenerali Makenga, vikiwemo vya usafiri na kukamata mali yake.
Serikali ya Marekani pia imewazua Wamarekani kujihusisha kwa namna yoyote na Sultan Makenga, ambaye alikuwa afisa wa ngazi ya cheo cha Jenerali katika jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Hata hivyo haijaeleweka iwapo hatua ya kukamata mali itakuwa na athari kwani inadhaniwa kuwa Makenga huenda hana mali ya kiasi cha kumtisha ambayo iko nchini Marekani.
Taarifa ya Umoja wa Mataifa, imesema waasi wamekuwa wakipata silaha kinyume na amri ya Umoja wa Mataifa inayozuia biashara ya silaha kuingia nchini humo.
Taarifa hiyo pia imemtaja Jenerali Makenga kuhusika na vitendo vya mauaji, ukataji viungo vya binadamu, ubakaji, utekaji nyara dhidi ya raia na kuwalazimisha watu kuyakimbia makaazi yao.
Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Susan Rice, amesema vikwazo vipya vinaonyesha kuwa dunia haitavumilia vitendo vya uhalifu vilivyofanyika chini ya amri ya Jenerali Makenga.
Uasi ulianza mwezi March wakati wanajeshi waasi walipojitoa kutoka jeshi la Congo na kutwaa miji karibu na Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini mashariki mwa Congo.
Maafisa walioasi walipinga kuhamishiwa katika maeneo mengi ya nchi wakisema wanataka kubakia katika eneo la mashariki kwa madai ya kuwalinda wananchi wa eneo hilo.
Pia wanasema wanataka wakimbizi wanaoishi Rwanda, Uganda na Burundi, kupelekwa katika eneo hilo.
Umoja wa Mataifa umezishutumu Rwanda na Uganda kwa kuwaunga mkono waasi, shutuma ambazo nchi zote mbili zimekana kuhusika.

habari kwa hisani ya bbc swahili

No comments:

Post a Comment