Gavana wa Jimbo la Kivu ya Kaskazini ameiambia BBC, kuwa waasi wa M23 hawana uwezo wa kuuteka mji wa Goma, Mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo, kufuatia mapigano makali.
Julien Paluku amesema wapiganaji hao wa waasi walikuwa wamempigia simu kumjulisha kuwa watawasili leo usiku mjini Goma.
Paluku amesema wanajeshi 150 wa waasi wameuawa lakini msemaji wa waasi hao amekanusha habari hizo.
Mapigano hayo ndiyo mabaya zaidi tangu mwezi Julai mwaka huu katika eneo hilo lenye utajiri mkubwa wa madini.
Zaidi ya watu laki tano wamehama makwao tangu mwezi Aprili mwaka huu, wakati wanajeshi kadhaa walipoasi kutoka kwa jeshi la Serikali.
Mapigano hayo yamekuwa yakiendelea karibu na kijiji cha Kibumba takriban kilomita 30 Kaskazini mwa Goma.
Gavana wa Jimbo la Kivu ya Kaskazini Julien Paluku ameiambia BBC kuwa mapigano hayo yanaendelea hadi leo siku ya Ijumaa.
Umoja wa Mataifa unazishtumu Rwanda na Uganda kwa kuwaunga mkono waasi, shutuma ambazo zinapingwa na nchi zote mbili.
Mwandishi wa BBC, Gabriel Gatehouse amesema kuzunguka kijiji cha Kibumba kiasi cha kilomita 30 Kaskazini mwa Goma hali imekuwa mbaya zaidi tangu mwezi Julai.
Amesema serikali imepeleka vikosi zaidi, katika eneo hilo ikiwa ni pamoja na helikopta za kijeshi, pia askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa wameonekana katika maeneo ya kijiji cha Kibumba.
Pande zote mbili wamelaumiana kwa kuanzisha mapigano hayo yaliyoanza mapema asubuhi Alhamisi.
Mwandishi wa BBC amesema wakati alipokuwa katika eneo linalodhibitiwa na waasi Jumatano, aliwaona waasi wa M23 ambao pia hujulikana kama Jeshi la Ukombozi la Congo wakisambaza askari wake na kujiandaa kwa vita.
Watu wanakimbilia kuelekea Kusini ambako majeshi ya serikali yanadhibiti maeneo hayo wakiwa wamebeba mizigo yao vichwani.
Baadhi yao wamekuwa wakienda katika kambi kubwa ya Kibai iliyopo katika vitongoji vya kaskazini mwa Goma.
Msema wa Umoja wa Mataifanchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Luteni Kanali Prosper Basse, amesema pia kumekuwa na mapigano kilomita 90 kaskazini mwa Goma, huku majeshi ya serikali yakitwaa mji wa Mabenga na kusonga mbele kuelekea mji wa Kiwanja ambao ni mji muhimu wa waasi.
No comments:
Post a Comment