Akizungumza kwenye mahojiano na waandishi wa habari jana, mtoto Aaryan alisema amejipanga vizuri kufika kileleni ingawa anatambua atakumbana na hali ngumu ya hewa, kama ilivyokuwa kwa Mlima Everest.
Aaryan alisema sio kazi rahisi kupanda mlima ambao ni mrefu kuliko yote barani Afrika, lakini kutokana na nia aliyonayo, atajitahidi kadri atakavyoweza, ili kufanikisha malengo yake ya kufika kileleni.
Alisema anataka kuweka historia kama alivyoandika historia ya kuwa mototo wa kwanza kupanda mlima Everest na kufika kileleni.
Alisema safari ya Mlima Everest, ilikuwa na changamoto mbalimbali ikiwemo barafu na kupanda miamba mikubwa na kulala kwenye mahema, lakini alifanikiwa kufika kileleni.
Alidai kuwa mafanikio hayo yametokana na mchango mkubwa aliokuwa akipata kutoka kwa wazazi wake, hususani kupewa mazoezi pamoja na kutiwa moyo.
“Nina furaha kubwa kuona nikiwa na umri wa miaka saba tuu nimeandika historia ya duniani kwa kupanda Mlima Everest ambao ni mrefu kuliko yote duniani. “Lakini furaha yangu nyingine ni kupanda Mlima Kilimanjaro na sasa napenda kila mtoto atambue wanaweza kila kitu endapo wazazi wao wakiwasaidia,” alisema Aaryan.
“Baba yangu Balaji, alikuwa akinifundisha mazoezi mbalimbali kabla sijapanda Mlima Everest na sasa kabla ya kupanda Mlima Kilimanjaro, nimefanya mazoezi ya kutosha pamoja na mama yangu kunitia moyo kuwa kila kitu kizuri ninachofanya na kuona kuna njia za mafanikio,” aliongeza Aaryan.
Mama mzazi wa Aaryan, Riki Balaji aliyeongozana naye kwa ajili ya safari ya kupanda Mlima Kilimanjaro, alisema kuwa lengo la mtoto wake ni kuhamasisha wazazi wengine kuona watoto wao wanaweza kufikia malengo ya vipaji vyao.
Riki alisema baadhi ya wazazi wengi hawana muda wa kukaa na watoto wao na kusikiliza mahitaji na malengo yao, ikiwemo kuwatia moyo katika nyanja mbalimbali ili wafikie yale yote wanayoyatarajia kwenye maisha yao.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Utalii ya Easy Travel ya mjini Arusha, Musaddiq Gulamhussein, alisema safari hiyo imeratibiwa na kampuni hiyo kwa kushirikiana na kampuni ya G.Adveture iliyopo nchini Canada.
No comments:
Post a Comment