Tuesday, February 19, 2013

Nusu kidato cha nne wapata div 0

ZAIDI ya nusu ya wanafunzi waliofanya mtihani wa Taifa wa kidato cha nne, wamepata daraja sifuri katika matokeo ya mtihani huo. Akitangaza matokeo hayo Dar es Salaam jana, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa, alisema kati ya wanafunzi wa shule za sekondari 397, 136 waliofanya mtihani huo, wanafunzi 240,903, wamepata daraja sifuri.
Akifafanua hali halisi, Dk Kawambwa alisema waliopata daraja la kwanza ni wanafunzi 1,641 tu, daraja la pili wanafunzi 6,453 na daraja la tatu watahiniwa 15,426.
Kwa mujibu wa matokeo ya mtihani huo, uliofanyika kati ya Oktoba 8 hadi 25 mwaka jana, wanafunzi waliopata daraja la nne ni 103,327.
Wanaojitegemea Dk Kawambwa alisema kati ya wanafunzi wa kujitegemea 68,806 waliosajiliwa, ni wanafunzi 61,001 tu waliofanya mtihani huo na kati ya hao, waliofaulu ni 16,112 tu; wasichana wakiwa ni 6,751 na wavulana 9,361.
Aidha, Dk Kawambwa alizitaja shule 20 bora zilizofanya vizuri, tatu zikiwa zinazomilikiwa na Serikali na zilizobaki zikimilikiwa na watu binafsi na taasisi za dini.
Shule vinara Dk Kawambwa alitaja shule zilizoongoza katika kundi la wanafunzi zaidi ya 40 kuwa ni St Francis Girls (Mbeya), Marian Boys 9 (Pwani), Feza Boys (Dar es Salaam), Marian Girls (Pwani) na Shule ya Sekondari Rosmin (Tanga).
Nyingine ni Shule ya Sekondari Canossa (Dar es Salaam), Shule ya Sekondari Jude Moshono (Arusha), St. Mary’s Mazinde Juu (Tanga), Anwarite Girls (Kilimanjaro) na Kifungilo Girls (Tanga).
Shule ya 11 ni Feza Girls (Dar es Salaam), Kandoto Sayansi Girls (Kilimanjaro), Don Bosco Seminary (Iringa), St. Joseph Millennium (Dar es Salaam) na St. Joseph’s Iterambogo (Kigoma).
Shule ya 15 ni St. James Seminary (Kilimanjaro), Mzumbe (Morogoro), Kibaha (Pwani), Nyegezi Seminary (Mwanza) na Tengeru Boys (Arusha).
Mkiani, wadanganyifu Shule zilizofanya vibaya kwa mujibu wa Dk Kawambwa ni Mibuyuni ya Lindi iliyoshika mkia kabisa. Juu yake ziko Ndame ya (Unguja), Mamdimkongo (Pwani), Kitekete (Mtwara) na Maendeleo (Dar es Salaam).
Nyingine ni Kwamdolwa (Tanga), Ugulu ( Morogoro), Kikale (Pwani), Nkumba na Tongoni za Tanga. Hata hivyo, Dk Kawambwa alisema watahiniwa 789 wamefutiwa matokeo yao yote baada ya kubainika kufanya udanganyifu katika mitihani yao. Kati ya hao, watahiniwa wa shule ni 624, watahiniwa wa kujitegemea 148. Alisema udanganyifu wa kwanza kubainika ni katika miandiko.
Alifafanua kuwa wanafunzi hao wanne, kila mmoja alikutwa na miandiko tofauti katika mitihani tofauti aliyofanya. Wengine 170 walikamatwa wakiwa na nyaraka kwenye chumba cha mtihani na 590 waliokutwa na majibu yaliyofanana katika hali isiyo wa kawaida.
Dk Kawambwa alisema wanafunzi wanne walikamatwa wakifanyiwa mitihani, sita walikutwa na simu na watahiniwa 15 walikutwa wakibadilishana karatasi wakati wa mtihani. Matusi “Kuna wanafunzi 24 ambao matokeo yao yamefutwa kwa kuandika matusi kwenye masomo mbalimbali. Huu ni utovu wa nidhamu wa hali ya juu na Serikali haitavumilia.
“Tunaangalia hatua za kisheria za kuchukua dhidi yao. Kwa wale waliofanya udanganyifu wanaweza kufanya mitihani tena baada ya mwaka mmoja,” alisema.
Akizungumzia tathimini ya mtihani huo, Kawambwa alisema shule zilizofanya vizuri ni zile zenye mahitaji ya msingi, ikiwamo walimu wa kutosha, miundombinu na vifaa vya kufundishia na kujifunzia.
“Ukiangalia zile zilizofanya vibaya, ni zile zenye changamoto ya kukosa walimu hususani wa sayansi na hisabati, kutokuwapo kwa maabara za shule na upungufu mkubwa wa vitabu vya kiada na ziada na kuwa na uwiano wa kitabu kimoja kwa wanafunzi 10,” alisema.
Kawambwa alisema kutokana na hali hiyo, Serikali imejipanga kupunguza changamoto hizo kwa kuajiri walimu ambapo mwaka huu wa fedha, walimu 13, 246 waliajiriwa ikiwa ni wastani wa walimu kati ya wawili na watatu katika shule moja.
Alisema pia wanapanga kuboresha miundombinu ikiwa ni pamoja na kujenga nyumba za walimu, maabara na kuendelea kutoa ruzuku ya Sh 25,000 kwa mwanafunzi kwa mwaka.
Udhaifu katika utangazaji Mabadiliko ya utangazaji wa matokeo hayo yaliyoanza mwaka huu kwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi kuyatangaza, yameonesha udhaifu ikilinganishwa na ilivyokuwa zamani, ambapo Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA), aliyatangaza.
Kwa mfano katika taarifa ya Waziri, haikuonesha wanafunzi bora kumi kitaifa, wanafunzi bora kumi kitaifa wasichana, wala wanafunzi bora kumi kitaifa wasichana. Kawambwa alipoulizwa kuhusu kukosekana kwa orodha hiyo, alisema amekabidhiwa kabrasha kubwa ndio maana ameshindwa kutaja kila kitu.
Hata hivyo, taarifa iliyokabidhiwa kwa vyombo vya habari, nayo hakionesha orodha hiyo tofauti na taarifa ambayo imekuwa ikiandaliwa na NECTA.

CHANZO HABARI LEO

No comments:

Post a Comment