Sunday, July 14, 2013

Uchaguzi mdogo wa madiwani Arusha wageuka vurugu tupu

Masanduku ya kuhesabia kura uchaguzi mdogo wa madiwani Arusha 

Arusha. Uchaguzi mdogo katika kata nne za Jiji la Arusha unafanyika leo, huku Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ikiwapiga marufuku Mkuu wa Mkoa, Magessa Mulongo na Mkuu wa Wilaya ya Arusha, John Mongella kuingia kwenye vituo vya kupigia kura, wala kujihusisha kwa namna yoyote na zoezi la upigaji kura ikisema siyo jukumu lao kisheria.
Mbali ya NEC kupiga marufuku viongozi hao wa kisiasa kukaribia vituo hivyo, uchaguzi huo umekumbwa na matukio kadhaa likiwamo la Mbunge wa Jimbo la Arusha, Godbless Lema pamoja na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Taifa Chadema(Bavicha), John Heche, kunusurika kuswekwa rumande jana.
“RC na DC hawana haki wala mamlaka ya kujihusisha kwenye zoezi na shughuli za upigaji kura. Mwenye dhamana, wajibu na haki ya shughuli zote za upigaji kura ni Mkurugenzi wa Jiji ambaye ni mwakilishi wa NEC pamoja na maofisa wengine wanaotambuliwa kisheria,” alisema Mwenyekiti wa NEC Jaji Damian Lubuva jana.
Lema na Heche walinusurika kuswekwa rumande baada ya kufika Kituo Kikuu cha Polisi jijini Arusha, wakishinikiza jeshi hilo, kukamata magari matatu waliyodai kuwa ni ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) na kubadilishwa namba yakihofiwa kwamba huenda yakatumika kuvuruga uchaguzi wa leo.
Tukio hilo la aina yake, lilitokea jana asubuhi baada ya viongozi hao, kufika polisi na kutoa taarifa hiyo, wakieleza kuwa lakini waliambiwa waondoke kwa kuwa gari kubadili namba siyo kosa ambapo pia walitakiwa kumtaja aliyewaeleza kama magari hayo yatatumika kufanya uhalifu.
Aidha, viongozi wa vyama vyote vya siasa ambao sio mawakala wala wagombea, wamepigwa marufuku kuingia kwenye vituo vya kupigia kura, wala kujihusisha kwa namna yoyote na zoezi la upigaji kura badala yake wakiwa ni wakazi wa kata husika kupiga kura na kuondoka maeneo hayo.
Mwenyekiti wa NEC, alitoa tamko la kuzuia viongozi hao jana alipozungumza na waandishi wa habari kuelezea mipango na mikakati ya tume yake katika kufanikisha zoezi hilo linalofanyika baada ya kuahirishwa mara mbili.
Mbele ya makamu wake Jaji Mkuu mstaafu wa Zanzibar, Jaji Hamid Mohamoud Hamid, Jaji Lubuva alitaja orodha ya watu 12 wenye haki kisheria kuingia kwenye vituo vya kupigia kura na kujihusisha na zoezi la upigaji, kuhesabu, kujumlisha kura kuwa ni msimamizi wa kituo, msimamizi msaidizi wa kituo, mawakala wa vyama na wapiga kura.
Wengine ni Mkurugenzi wa Uchaguzi, mgombea, mjumbe wa NEC, Ofisa wa NEC, Mratibu wa NEC mkoa, askari polisi au mtu yeyote anayehusika na usalama katika kituo cha kupiga kura, mtu anayemsaidia mpigakura asiyejiweza na mwangalizi wa uchaguzi aliyeidhinishwa na NEC kimaandishi na katika utaratibu uliowekwa.
Uchaguzi huo unafanyika leo baada ya kuahirishwa Juni 16, mwaka huu, baada ya bomu la kutupa kwa mkono kulipuka kwenye mkutano wa Chadema wa kufunga kampeni kwenye Viwanja vya Soweto, Arusha.
Agizo la kupiga marufuku kujihusisha na Uchaguzi Mkuu wa Mkoa(Mulongo) na Mkuu wa Wilaya(Mongella) ambao ni makada na wajumbe wa Kamati za Siasa na Halmashauri za Mkoa na Wilaya za CCM, limekuja wakati kukiwa na tuhuma kutoka kwa vyama vya upinzani, hasa Chadema kuwa wanatumia nyadhifa zao kukibeba chama tawala.
Akizungumzia kunusurika kuwekwa rumande, Heche alisema kutokana na majibu ya polisi wao wakiomba wapewe hata fursa ya kuandika maelezo kuhusu tukio hilo au wapewe polisi kwenda kuzikamata gari hizo, lakini waligomewa, ndipo likatolewa agizo la kukamatwa kuwekwa rumande kwa Lema.

HABARI KUTOKA MWANANCHI

No comments:

Post a Comment