Thursday, November 7, 2013

MAMLAKA ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) yatoa ufafanuzi kwa wananchi


Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Habari na Uhifadhi Hati wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Thomas Willium akieleza kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu zoezi la uchukuaji wa alama za kibaiolojia linaloendelea katika jiji la Dar es Salaam, zoezi hili limeshakamilika katika Wilaya ya Ilala na pia lipo katika hatua za mwisho katika wilaya ya Temeke na baada ya hapo litahamia wilaya ya Kinondoni,Kulia ni Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Bi. Zamaradi Kawawa.
Meneja Mifumo ya Uchambuzi ya Kompyuta wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Bw. Mohamed Mashaka akieleza kwa waandishi wa habari(hawapo pichani) utaratibu wa kuweka majina kwenye mbao za matangazo ya vituo vya usajili ili wananchi waweze kuhakiki usahihi wa majina yao.Kulia ni Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Habari na Uhifadhi Hati toka Mamlaka hiyo Bw. Thomas Willium.
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Habari na Uhifadhi Hati wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) Thomas Willium akiwaonesha waandishi wa habari (hawapo pichani) ,kifaa cha kuchukulia alama za vidole (mobile enrolment unit). Wakati wa mkutano uliofanyia katika ukumbi wa Idara ya Habari(MAELEZO) Leo Jijini Dar es Salaam. (Picha zote na Hassan Silayo-MAELEZO)

Uchukuaji alama za kibailojia waendelea Dar
MAMLAKA ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) inaendelea na zoezi la uchukuaji alama za kibailojia katika mkoa wa Dar es Salaam.
Zoezi hili linafanyika kiwilaya, hadi sasa NIDA imefanikiwa kumaliza wilaya ya Temeke na ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha zoezi hili katika wilaya ya Ilala. Baada ya hapo itafuatia wilaya ya Kinondoni.
Mamlaka inatambua kwamba wapo waliokosa fursa ya kujiandikisha kwa wakati uliopangwa hivyo, imefungua ofisi zake Kigamboni na Chang’ombe katika wilaya ya Temeke ili watu hao waweze kupata huduma hiyo. Aidha, Mamlaka itafungua ofisi zake katika wilaya za Ilala na Kinondoni kuhakikisha huduma inasogea karibu zaidi na wananchi.
Mbali ya uandikishaji ofisi hizi pia zitahusika kutoa huduma nyingine kama uchukuaji alama za kibaiolojia, kupokea na kutatua malalamiko na matatizo mbalimbali ya wananchi yanayohusu Vitambulisho vya Taifa.
Hatua inayofuata baada ya kukamilika kwa zoezi la uchukuaji wa alama za kibailojia ni kupokea maoni ya wananchi yanayohusu maombi ya vitambulisho yaliyopokelewa na baada ya hapo ugawaji wa vitambulisho utaanza.
Ugawaji wa Vitambulisho vya Taifa unatarajia kuanza Desemba 2013 kwa waombaji waliokamilisha hatua zote.
Waombaji wanatakiwa kufika kwenye vituo vya usajili kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 11:00 jioni na nyaraka halisi za kuthibitisha uraia na umri mathalan, cheti cha kuzaliwa, pasipoti, vyeti vya elimu ya msingi na sekondari, leseni ya udereva, kitambulisho cha bima ya afya au kitambulisho cha mpigakura.
Majina ya waombaji na tarehe ya kuchukuliwa alama za vidole na picha yanabandikwa kwenye mbao za matangazo katika vituo vya usajili.
Kwa ajili ya ubora na mwonekano mzuri wa picha kwenye kitambulisho, mwombaji anashauriwa kutovaa nguo nyeupe, kijivu au bluu mpauko na kofia anapokuja kupiga picha.
Kitambulisho cha Taifa ni haki ya msingi ya kila raia, mgeni mkaazi na mkimbizi halali mwenye umri wa miaka 18 na zaidi. Aidha, hakuna malipo yoyote atakayotozwa mwombaji katika zoezi hili.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano na Hifadhi Hati,
Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa-NIDA 

No comments:

Post a Comment