Wednesday, June 18, 2014

Makala: Watanzania wengi bado wanategemea kilimo kwa maendeleo ya maisha yao



Mkulima akifafanua jambo kwenye moja ya mafunzo ya kilimo. (Picha zote na John Banda)
Mtaalamu wa masuala ya nyuki akitoa maelezo kwa wakulima (hawapo pichani), wakati wa mafunzo ya kilimo.
Wakulima wakiwa katika mafunzo ya kilimo cha alizet, mtama na    ufugaji nyuki
Na John Banda, Dodoma
KILIMO ni moja ya sekta ambazo zinategemewa kwa kiasi kikubwa hapa nchini na watanzania waliowengi ikiwa kama ni sehemu yao ya kipato ili waweze kujikwamu kiuchumi, Makala hii inaeleza.


Pamoja na idadi kubwa ya wananchi kukitegemea kilimo kama ni sehemu yao ya kujikwamua kiuchumi  bado kuna changamoto mbalimbali zinazowakabili wakulima.


Changamoto hizo ni pamoja na ukosefu wa elimu ya kutosha katika suala zima la kilimo inatokana na wakulima wengi kuendelea kulima kilimo cha kienyeji hivyo kuwafanya washinde kujikwamua kiuchumi.


Nyingine ni serikali bado haijaweka mkazo katika kuwasaidia wakulima wadogo ili kuboresha namna ya kilimo chao kwa kuwawezesha pembejeo za kisasa na kwa wakati mwafaka.


Hali hii imechangia kwa kiasi kikubwa wakulima wadogo kuendelea kulima kilimo kisicho kuwa na tija na kuendelea kuwa masikini pamoja na kutumia muda wao mwingi kulima maeneo makubwa na kupata mavuno kidogo tofauti na gharama walizo tumia.


Kutokana na hali hiyo inaisukuma kampuni ya wasindikaji wadogo wa mafuta ya alizeti mjini Dodoma ya Three sisters, kwa kushirikiana na Shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha na wakulima wadogowadogo(Rldc) kuanzisha utaratibu wa kutoa mafunzo kwa wakulima ili kuweza kuwasaidia kuboresha kilimo chao.


Mmoja wa wakurugenzi wa Kampuni hiyo Mariam Majengo, anasema kuwa wakulima wadogowadogo zaidi ya 6,000 katika wilaya za Chemba na Chamwino mkoani Dodoma watanufaika na mafunzo ya kilimo cha kisasa cha mtama, alizeti,ufugaji nyuki na upandaji wa miti utakaowasaidia kujikwamua katika hali duni ya maisha.


Anasema kuwa mafunzo hayo yanatolewa kwa ushirikiano wa shirika hilo na kampuni ya kukamua mafuta ya alizeti ya Three Sisters Company Ltd.


Anasema kuwa mradi huo utahusisha jumla ya vijiji 36 ambapo wakulima watapatiwa mafunzo ya kilimo cha kisasa ili kuweza kuzalisha mavuno mengi tofauti na ilivyo hivi sasa.


Majengo anasema kuwa mafunzo hayo yamelenga kuwawezesha wakulima wenye maisha duni ili kuweza kujikwamua kiuchumi na kuboresha maisha yao kupitia kilimo na ufugaji wa nyuki.


Anasema kuwa pamoja na mafunzo hayo pia watawapatia mikopo ya pembejeo mbalimbali za kilimo ambazo watazitumia katika kufanikisha kilimo bora na cha kisasa ili kuweza kujikwamua kiuchumi.


Anafafanua kuwa katika mafunzo hayo yatawasaidia wakulima kulima alizeti yenye kiwango bora na kukidhi viwango vya kimataifa ili kuwauzia watu wenye viwanda vya kukamua mafuta.


“Kama wakulima watakuwa na elimu ya kutosha juu ya kilimo cha alizeti watatoa alizeti iliyo bora hali ambayo itasaidia hata viwanda vyetu kutoa mafuta yenye ubora na kukidhi viwango pia na wao kujipatia kipato kwa kuuza mazao yaliyo bora,” anasema.


Anaongeza kuwa  kilimo cha zao la mtama kitawasaidia kupata chakula cha kutosha.


Kuhusu ufugaji nyuki anasema wataweza kuuza zao la asali wakati msimu wa kilimo ukiwa umekwisha hivyo kuwafanya kila wakati kuwa na uhakika na maisha yao.


Anasema kuwa katika mafunzo hayo wanawasisitiza sana wakulima kuhakikisha pia wanafuga nyuki ambao watawasaidia katika kuchavusha maua ya alizeti katika mashamba yao.


Anasema kuwa mazao yanayochavushwa na nyuki huwa yanaubora tofauti na yale yanayochavushwa kwa upepo hivyo itawasaidia kuuza mazao yenye ubora na kwa bei nzuri tofauti na sasa.


“Pamoja na nyuki kutumika katika kuchavushwa pia wakulima wakishavuna asali watauza kwa bei nzuri ambayo itawawezesha kujipatia kipato na kuondokana na suala la uharibifu wa mazingira kwa kuendekeza tabia ya ukataji wa mkaa unachangia kwa kiasi kikubwa kuharibu mazingira,”alisema Majengo.


Anabainisha kuwa toka waanze kutoa mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa zaidi ya miaka mitatu iliyopita hali ya ubora wa mazao imebadilika tofauti na ilivyo kuwa awali kwakuwa wakulima wanazalisha mazao yenye ubora na kujipatia soko la kutosha kwa watu wenye viwanda vidogovidogo vya kusindika mafuta ya alizeti.


“Zamani mkulima alikuwa analima heka nne na kupata gunia mbili hadi tatu lakini hivi sasa anao uwezo wa kupata gunia nane hadi 15 kupiti kilimo cha kisasa na matumizi ya mbegu bora,” anasema Majengo.


Anasema pamoja na kutoa mafunzo hayo ya kilimo lakini bado wamekuwa wakikabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo kutoka kwa wakulima wenyewe kutotoa ushirikiano kwa asilimia kubwa.


Anasema kuwa wakulima wengi wamekuwa wakienda kinyume na mafunzo yanayotolewa kwa kuendelea kulima kienyeji bila ya kufuata utaratibu hivyo kusababisha kushindwa kufikia malengo yao ya kupata mazao yenye ubora kwenye soko.


Aidha anasema kuwa changamoto nyingine ni kukosa ushirikiano kutoka kwa viongozi wa vijiji ambao wamekuwa wakishindwa kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi katika kupata mafunzo hayo.


Changamoto nyingine anasema ni katika kupatikana kwa masoko ya mazao hayo pamoja na bidhaa yake ya mafuta ambayo imekuwa ikikabiliana na changamoto ya uingizaji wa kiwango kikubwa cha mafuta kutoka nchi nyingine.


“Mafuta mengi yamekuwa yakiagizwa kutoka nchi jirani hali inayo changia ushindani katika soko kutokana na kutokuwepo kwa ushuru wa uingizaji bidhaa hiyo...lakini pia gharama za uzalishaji hapa kwetu ziko juu,”anasema.

Naye mmoja wa wakulima waliopatiwa mafunzo ya kulima kwa kisasa, Abuu Mickdadi, anasema kuwa kiasi cha mavuno kimeongezeka sana ukilinganisha na hapo awali.

Anasema kuwa awali walikuwa wakitumia nguvu nyingi kwa kulima mashamba makubwa na kupata kiasi kidogo cha mavuno ambacho kilikuwa hakikidhi kabisa gharama waliyokuwa wakiitumia katika kulima.


“Toka tumeanza kulima kwa kufuata mafunzo ya kilimo cha kisasa hata kipato kimebadilika sana tunavuna mazao mengi lakini pia yenye ubora ambayo hatuna shaka ya kupata wanunuzi,” anasema Abuu.

Mwenyekiti wa chama cha wasindikamafuta kanda ya kati (Cezosopa) Ringo Iringo, anasema kuwa mafunzo hayo yamesaidia wakulima wengi wa zao la alizeti kuongeza kiwango cha uzalishaji wa mafuta kutokana na kutumia mbegu zenye ubora na kulima kwa kisasa.

Ringo anasema kuwa moja ya changamoto zilizokuwa zikiwakabili wakulima wa zao hilo ni kutumia mbegu zisizo na ubora hivyo kusababisha kiwango cha uzalishaji kushuka.

“Wakulima wanatakiwa kubadilika na kuanza kutumia mbegu bora ambazo zinatoa mafuta kwa wingi na yenye ubora tofauti na ilivyo wakati huu,” anasema Ringo.

Anasema kuwa kwakutumia mbegu bora wakulima watanufaika kwa kupata mafuta mengi pamoja na mashudu bora kwaajili ya matumizi mengine.

Anaeleza kuwa kiwango cha uzalishaji wa mafuta nchini bado kiko  chini kutokana na utumiaji wa mbegu za kienyeji ambazo hazitoi mafuta mengi na yenye ubora.

“Mahitaji ya mafuta nchini ni takribani tani 300,000 lakini sisi kwa kiwango cha ndani tunazalisha tani 90 elfu na asilimia nyingine yote inatoka nje hivyo hatuna budi kujipanga katika kuzalisha mafuta mengi na yenye ubora na ni matumaini yangu kupitia mafunzo haya kwa wakulima kiwango kitaongezeka” anasema.

Aidha anabainisha kuwa wadau wa mafuta na serikali kwa pamoja wamekutana na kuweka mikakati madhubuti ambayo itasaidia kwa miaka michache ijayo kuongeza uzalishaji.

“Miaka michache ijayo tutaweza kuwa tunazalisha kwa kiwango cha juu kiasi ambacho tutakuwa hatuna haja ya kuagiza mafuta kutoka nchi za nje” anasema.

Hatahivyo anatoa wito kwa serikali kuwasaidia wasindikaji wadogo katika kupata viwanja kwajili ya kuwekeza viwanda vyao pamoja na kuongeza mafunzo kwa wakulima wengi walioko vijijini ili kuongeza uzalishaji.

No comments:

Post a Comment