Tuesday, February 7, 2017

Ni Wakati muafaka wa kulitumia Baraza la Taifa la Ujenzi katika ukaguzi na uendeshaji wa miradi.


Na Ismail Ngayonga,MAELEZO-Dar es Salaam


KATIKA mwaka 2014/15 Mamlaka ya udhibiti wa manunuzi ya umma (PPRA) ilifanya ukaguzi katika taasisi 70 za umma ili kuangalia iwapo taasisi hizo zilizingatia sheria na kanuni za manunuzi na matumizi ya nyaraka za miongozo iliyoandaliwa na PPRA.

Taasisi zilizoguswa na ukaguzi huo uliofanyika kati ya mwezi Aprili hadi Septemba ni pamoja na taasisi 15 zilizo katika kundi la Wizara, Idara na Wakala za Serikali, Mamlaka za Serikali za Mitaa 25 na mashirika ya umma 30.

Aidha jumla ya mikataba 21,313 ya manunuzi yenye thamani ya Tsh Trilioni 1.05 ilifanyiwa ukaguzi huo, ikiwemo mikataba 845 ya kazi za ujenzi, ambapo mikataba 130 yenye thamani ya Tsh 697 ikihusisha ukaguzi wa thamani halisi ya matumizi ya fedha.

Matokeo ya ukaguzi huo iliyohusisha miradi ya mbalimbali ya maendeleo yenye thamani ya Tsh. Milioni 964, ilibainika kuwa miradi 10 ya sekta ya ujenzi ilipata alama isiyoridhisha kutokana na thamani halisi ya fedha iliyotumika kushindwa kulingana na kiwango cha utekelezaji wa miradi iliyoainishwa.

Miradi iliyochaguliwa kwa ajili ya kufanyiwa ukaguzi wa kupima thamani ya fedha ilipatikana katika utekelezaji wa mikataba ya manununzi iliyothaminiwa kwa kutumia vigezo mbalimbali ikiwemo uandaaji, usanifu na uhifadhi wa nyaraka za zabuni, mchakato wa manunuzi pamoja na usimamizi wa kazi za ujenzi na mikataba.

Sekta ya Ujenzi ni miongoni sekta za kiuchumi zinaoongoza katika upotevu wa fedha za Serikali, na hivyo kuiingizia hasara Serikali kutokana na miradi mingi kutekelezwa chini ya kiwango na kukosekana kwa uwazi katika mikataba ya mkandarasi na taasisi.

Ili kukabiliana na changamoto hiyo, mwaka 2008 Serikali iliifanyia marekebisho sheria ya Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) ili kuhakikisha kuwa sharia hiyo inaenda sambamba mazingira yaliyopo katika sekta ya ujenzi nchini hususani katika usimamizi na uendeshaji wa miradi inayosimamiwa na mamlaka za Serikali za Mitaa ikiwemo Mikoa na Wilaya.

Hivi karibuni Baraza hilo lilitoa taarifa yake kwa umma kuhusu tathimini ya ukaguzi wa kiufundi katika miradi 163 ya ujenzi yenye thamani ya Tsh. Bilioni 2.8 ikihusisha barabara, majengo na viwanja vya ndege.

Ukaguzi huo uliofanyika kati ya mwaka 2005-2009 ulilenga katika kufanya mapitio ya michakato ya manunuzi, utekelezaji wa miradi, ongezeko la gharama za miradi, ubora wa kazi zilizofanyika na gharama za malipo ya zabuni.

Kaimu Mkuu wa Idara ya Uhandisi wa NCC, Mhandisi Wambura Wambura anasema ukaguzi wa kiufundi katika utekelezaji wa miradi ya ujenzi ni uchunguzi maalum wa hatua mbalimbali za mradi, ambazo huwawezesha mamlaka ya maamuzi na wafadhili kujiridhilisha kwa kupata mrejesho halisia wa masuala mbalimbali ya mradi.

“Ukaguzi huu uhusisha mwenendo wa hatua mbalimbali za mradi hususani hatua za mwanzo za matayarisho ya mradi, upembuzi yakinifu wa mradi, usanifu, manunuzi na utekelezaji wa mradi” anasema  Mhandisi Wambura.

Anasema ukaguzi wa kiufundi katika miradi ya ujenzi huzisaidia mamlaka kuchukua hatua stahiki za maamuzi na tahadhari kwa wakati ili kuhakikisha ufanisi uliokusudiwa upatikana katika mradi husika.

Kwa mujibu wa Mhandisi Wambura anazitaja aina za kaguzi za kiufundi kuwa ni pamoja na ukaguzi wa kiufundi wakati wa matayarisho ya mradi, ukaguzi wa kiufundi wakati wa utekelezaji wa mradi, pamoja na ukaguzi wa kiufundi baada ya utekelezaji wa mradi.

Akizungumzia kuhusu taratibu za ukaguzi huo, Mhandisi Wambura anasema Baraza hilo hutoa miongozo maalum kwa ajili ya ukaguzi wa kiufundi katika, ambayo ni pamoja na kupokea maombi ya ukaguzi, uteuzi wa timu ya wataalamu, pamoja na kuandaa taarifa ya ukaguzi wa kiufundi.

Kwa mujibu wa Mhandisi Wambura anasema katika mwaka 2015/16, Baraza hilo lilifanya ukaguzi wa kiufundi wa miradi ya matengenezo ya barabara kwa halmashauri zote nchini pamoja na ukaguzi wa miradi ya majengo yanayomilikiwa na Benki ya NMB katika wilaya za Mwanga, Chalinze, Pangani, Mbulu na Arusha.

“Mwaka 2011 tulifanya ukaguzi katika miradi 14 ya ujenzi na vituo vya afya 36, yenye thamani ya Tsh. Bilioni 2.3 ambayo ilikuwa inatekelezwa na Halmashauri 20 nchini” anasema Mhandisi Wambura.

Baraza la Taifa la Ujenzi ni kitovu cha uratibu wa sekta ya ujenzi kwa taasisi zote zinazoshughulika na shughuli za ujenzi pamoja na wadau mbalimbali, likiwa na jukumu kuu la kusimamia na kuonogza juhudi za kukuza na kuendeleza sekta ya ujenzi ili kwenda sambamba na maendeleo na ushindani wa kimataifa.

Ni wajibu wa taasisi za umma na binafsi kushirikiana na Baraza hilo katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya ujenzi hususani katika shughuli za ukaguzi wa kiufundi wa miradi hiyo ili kuhakikisha kuwa thamani ya fedha inalingana na ubora wa miundombinu iliyojengwa.

No comments:

Post a Comment