DIWANI wa kata ya Endiamtu mji mdogo wa Mirerani Wilaya ya Simanjiro
Mkoani Manyara,Lucas Zacharia amezindua michezo ya shule za sekondari
Umiseta wilayani humo kwa kujitolea seti ya sare za michezo na mipira.
Akizindua michezo hiyo inayoendelea kwenye viwanja vya Barafu Mirerani
na shule ya sekondari Mirerani Benjamin Mkapa,Zacharia alisema michezo
ni ajira inajenga mwili na kuongeza marafiki na mwanzo wa mafanikio ni
kujituma.
Aliwataka wachezaji watakaochaguliwa kuunda timu ya Umiseta ya wilaya
hiyo kuiwakilisha Simanjiro kwa nguvu zote kwenye michezo ya Umiseta
ya mkoa huo itakayofanyika wiki ijayo wilayani Mbulu.
“Michezo mashuleni ilifutwa kipindi cha Rais Benjamin Mkapa waziri
akiwa Joseph Mungai sasa Rais Jakaya Kikwete amerudisha michezo
mashuleni hivyo tumieni fursa hiyo huku mkisoma kwa bidii bila
kuchoka,” alisema Zacharia.
Ofisa Elimu wa sekondari(Taaluma) wa wilaya hiyo Jilanga Mwantandu
alisema timu ya soka ya Kanda B iliifunga Kanda A bao 3-0 yaliyofungwa
na Venance Joseph na timu ya Kanda C iliifunga Kanda D bao 3-1.
Mwantandu alisema kwa upande wa mpira wa pete timu ya Kanda A
iliifunga Kanda B bao 22-0 hivyo kuwafuta machozi kaka zao na timu ya
Kanda D iliishinda Kanda C bao 12-8.
Alisema mchujo wa majina ya wachezaji wa timu ya wilaya hiyo
itakayowakilisha Simanjiro kwenye michuano ya Umiseta mkoa wa Manyara
itakayofanyika wilayani Mbulu wiki ijayo yanatarajiwa kutangazwa
kesho.
No comments:
Post a Comment