Tuesday, June 5, 2012

Anayetuhumiwa kumuua kigogo Chadema akamatwa

 
ANAYETUHUMIWA kuwa kinara wa mipango ya kumuua kwa kumchinja, aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema, Msafiri Mbwambo, amekamatwa na polisi akiwa kwa mganga wa kienyeji wilayani Kondoa, mkoani Dodoma.

Habari zilizopatikana kutoka Kondoa na baadaye kuthibitishwa na viongozi wa Chadema Wilaya ya Arumeru na Mkoa wa Arusha pia jeshi la polisi, zinasema kuwa mtuhumiwa huyo ambaye alikuwa mpangaji kwenye nyumba ya marehemu Mbwambo alikamatwa mwanzoni mwa wiki hii baada ya msako wa muda mrefu.



"Ni kweli huyo mtuhumiwa tunamshikilia na tunaendelea kumhoji, ingawa siwezi kukupa habari zaidi kwa sababu niko nje ya ofisi na sina kumbukumbu muhimu kuhusu tukio hilo.

Niko kwenye msafara wa mapokezi ya Mheshimiwa Rais," alisema Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Lebaratus Sabas. Kamanda huyo aliahidi kutoa taarifa zaidi kuhusu suala hilo baada ya kukusanya habari zote muhimu.

Lakini taarifa zilizopatikana kutoka ndani ya jeshi hilo zilimtaja aliyekamatwa kwa jina (tunalihifadhi kwa sasa) ambaye inadaiwa kuwa ndiye aliyemuunganisha marehemu na wauaji baada ya kumdanganya kuwa walitaka kujiunga Chadema.

Habari zinasema mtuhumiwa huyo alikuwa amejificha kwa mganga kwa nia ya kupewa dawa  ili asikamatwe na kwamba baada ya kutiwa mbaroni alisafirishwa hadi Arusha ambapo juzi Jumatano aliwapeleka polisi eneo ambalo alikuwa ameficha silaha zilizotumika kutekeleza mauaji.

Miongoni mwa silaha zilizokutwa zikiwa zimefichwa kwenye shamba la mmoja wa watuhumiwa ambaye tayari wamefikishwa mahakamani, ni bunduki, visu, panga na mashine ya mkono ya kukata na kupasua mbao, maarufu kama chenso inayosadikiwa kutumika kumchinja marehemu Mbwambo.

Habari zimeeleza kuwa ilibidi polisi kuimarisha ulinzi kukabiliana na hasira na nguvu ya wananchi waliokusanyika kwa wingi kwa nia ya kumdhuru mtuhumiwa huyo baada ya kukamatwa.

"Polisi tulilazimika kupelekea magari mawili ya askari wenye silaha kuepuka mtuhumiwa kuuawa na wananchi walioonekana kuwa na hasira, waliojitokeza kwa wingi wakiwa na silaha kwa nia ya kumdhuru mtuhumiwa," alisema mmoja wa polisi aliyekwenda kuonyeshwa zilikokuwa zimefichwa silaha hizo.

Habari zilieleza kuwa baada ya mahojiano mtuhumiwa huyo alikiri kujua na kuhusika kwenye mipango na utekelezaji wa mauaji hayo kwa malipo ya zaidi ya Sh1.5 milioni kutoka kwa watu ambao wanaendelea kuchunguzwa.

Katibu wa Chadema Wilaya ya Arumeru, Totinan Ndonde alisema  kuwa mtuhumiwa huyo ndiye aliyemwomba Katibu wa Chadema Kata ya Usa River, Said Mkwera amwambie marehemu (Mbwambo) atafute kadi nyingi za chama hicho ili amuunganishe na watu waliotaka kujiunga upinzani.

"Huyu ndiye aliyekuwa akimhimiza katibu wetu pale Usa ampatie marehemu kadi nyingi za Chadema na muda mfupi kabla ya mauaji aliulizia iwapo tayari Mbwambo amekabidhiwa kadi hizo," alisema na kuongeza:

"Huyo ndiye anayejua mipango yote ya mauaji na tayari tulishatoa taarifa polisi ambao badala ya kufanya uchunguzi waliamua kumkamata Mkwera ambaye ni shahidi muhimu," alisema Ndonde.

Pamoja na mtuhumiwa huyo, polisi pia wanamshikilia mtu mwingine (pia jina tunalihifadhi) wakimhusisha na mauaji hayo yaliyotikisa Wilaya ya Arumeru, kutokana na kufanana, kwani Mbwambo alikatwa shingo kwa nyuma hadi kichwa kubaki kikining'inia na kushikiliwa kwa ngozi.

Tayari watu watatu wamefikishwa mahakamani kwa mashtaka ya mauaji hayo miongoni mwao, wawili wakiwa wenyeviti wa vitongoji, wote kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kiongozi mmoja wa Chadema aliyesaidia kutoa taarifa za uhusika wa mtuhumiwa aliyekamatwa Kondoa.

Waliofikishwa mahakamani ni Jonathan ambaye ni Mwenyekiti wa Kitongoji cha Magadini na mwenzake, David Mmkumbwa wa Kitongoji cha Kisambare-Majengo.

No comments:

Post a Comment