Tuesday, June 5, 2012

Waunguja wawabagua Wapemba




ILE dhambi ya ubaguzi ambayo Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alionya kwamba huiwezi kuachwa sawa na kula nyama ya mtu, imeanza kujidhihirisha visiwani Zanzibar, baada ya kusambazwa vipeperushi vinavyotaka wananchi wenye asili ya Kisiwa cha Pemba kuondoka Unguja.
Ikiwa ni zaidi ya miaka 17 tangu Mwalimu kutoa onyo hilo, dhambi hiyo ya ubaguzi imeanza kuwatafuna Wazanzibari katika kipindi ambacho Jumuiya ya Uamsho Mihadhara ya Kiislamu (Jumiki), inazidi kuhamasisha Wazanzibari kuukataa Muungano.

Waakati kundi hilo la Jumiki likitaka Zanzibar iwe dola huru, limeibuka jingine linalojitambulisha kama ‘Watu wa Unguja’ likisambaza vipeperushi vinavyolishutumu kundi hilo la Uamsho, kwamba wahusika wake ni wananchi wanaotoka Pemba, wakitaka kuvuruga amani ya Unguja.
Huku wakihusisha baadhi ya viongozi waandamizi wa Serikali ya Mapinduzi  (SMZ), katika vipeperushi.Hivyo wamemwomba Rais Jakaya Kikwete ashauriane na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein wawaruhusu wapewe kisiwa chao cha Pemba.
“Watu wa Unguja tunatoa ujumbe mahususi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Kikwete…. Tumechoka kuishi na Wapemba katika kisiwa chetu cha Unguja, kwani ni watu wasio na fadhila ya aina yoyote ile,” inasomeka sehemu ya kipeperushi kimoja na kuongeza:,
“Hivyo, tunakuomba ufanye mazungumzo na Rais wa Zanzibar ili Wapemba wapewe kisiwa chao cha Pemba.”
Sehemu nyingine inasomeka, “Hapo siku za nyuma Wapemba walidai kisiwa chao, na ninyi viongozi mkang’ang’ania kuwa hatuwezi kuvunja umoja. Sasa mnaona hao tayari wameanzisha chama cha kisiasa cha ‘Uamsho’ kwa kisingizio cha dini.”
Kipeperushi hicho pia kimedai kwamba, asili ya wananchi wa Pemba ni Wamakonde kutoka Msumbiji wakati wenyeji wa Unguja wana asili ya Wasegeju kutoka Bara, ndiyo maana wanautaka Muungano.
“Kila siku mnajenga Unguja bila ridhaa yetu, nani mtu wa Unguja aliyejenga Pemba? Mnajenga mpaka ndani ya vyanzo vya maji, tunasema tokeni na hameni mara moja,” inasisitiza sehemu ya vipeperushi hivyo.
Huku wakilaumu marekebisho ya Katiba ya Zanzibar na kuitisha kura ya maoni iliyounda Serikali ya Umoja wa Kitaifa, wamesema wanahitaji Katiba Mpya ya Zanzibar ili kufuta mfumo huo.
Vipeperushi hivyo pia vimelaumu kundi la Uamsho kwa ubaguzi kwa wananchi wanaotoka bara na kusema, kuwa hata Wapemba wako kwa wingi upande huo wa pili wa Muungano.
Wamesisitiza pia kutaka Muungano kati ya Unguja na Tanganyika bila ya kuihusisha Pemba na kusisitiza:,
“Tunasema tena, sisi watu wa Unguja tunataka Muungano wa Serikali mbili ya Unguja na Tanganyika bila ya kuwapo Pemba. Kuwapo kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar isiyokuwa ya Umoja wa Kitaifa. Rais wa Zanzibar awe ndiyo Makamu wa Rais wa Muungano.”

Kauli ya Nyerere
Mwaka 1995 akiwa katika Hoteli ya Kilimanjaro  (sasa Hyatt Regency Dar es Salaam) , Mwalimu Nyerere akielezea nyufa kuu tano zilizokuwa zikiikabili nchi huku wa kwanza ukiwa ni Muungano.
Mwalimu alionya, “Watu wazima wameuzungumza Muungano, kwamba tuuvunje au tuendelee. Mtu mwenye akili hawezi kufikiri Uzanzibari ni fahari: Hana akili. Nje ya Muungano kuna Wapemba na Waunguja. Mtamaliza kutengana na Watanganyika, halafu mara mtakuta kumbe sisi si Wazanzibari.”
“Mtajikuta kuna Wapemba na Waunguja. Wapemba watapata msukosuko kidogo alololo! Mtakuta kumbe kuna Wazanzibari na Wazanzibara. Hamtakaa salama. Hamuwezi mkakaa salama baada ya kutenda dhambi ya kuwabagua watu wa nchi yenu ileile moja mkawaita wale wao na hao sisi. Dhambi ile haishii hapo. Ndivyo historia ilivyo; ni sheria ya historia siyo sheria ya Mwalimu Nyerere.”
Kinyume na onyo hilo la mwalimu, vipeperushi hivyo vimeorodhesha madai mengine, mojawapo likiwa kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano awe anapatikana kwa zamu ya kipindi kimoja kila upande wa Muungano.
Pia kundi hilo limedai kuwa Waziri Mkuu atoke bara, kila upande uwe na rasilimali zake kama vile mafuta na madini, ulinzi wa nchi uwe wa pamoja, kuwe na mgawo sawa wa mabalozi nje ya nchi na kuwa na mgawanyo sawa wa misaada ya maendeleo.
Tamko la Jumiki
Kwa upande wake Msemaji wa kundi la Jumik, Sheikh Faridi Hadi Ahmad amekosoa vipeperushi hivyo akisema vimejaa uzushi.
Akizungumza na waandishi wa habari katika msikiti wa Mbuyuni mjini Zanzibar juzi, Sheikh Faridi alisema kundi hilo halina uhusiano na Upemba wala Uunguja.
“Hao ni wapuuzi na wazushi, kama wanataka Wapemba warudi kwao, basi wamwambie na Rais Ali Mohamed Shein naye aondoke, Yule si ni mwenyeji wa Pemba?” alihoji Sheikh Farid.
Alisema kundi hilo lilianzishwa kwa ushirikiano na wananchi kutoka Pemba na Unguja kwa malengo ya kueneza dini na masuala mengineyo.
Kuhusu kujihusisha na siasa, alisema kuwa Katiba ya Zanzibar na dini ya Kiislamu inaruhusu waumini wake kushiriki siasa.
“Katiba ya Zanzibar inasema kuwa kila mtu ana haki ya kushiriki kwenye uongozi wa nchi. Hata Mtume Muhammad (S.AW), alikuwa ni rais wa eneo lake na alikuwa kiongozi wa dini… Siasa ni neno la Kiarabu likiwa na maana ya uongozi na uongozi una mambo mengi. Kwa hiyo tuna haki kabisa ya kushiriki siasa,” alisema Sheikh Farid.
Katika hatua nyingine, kundi hilo limepinga hatua ya Jeshi la Polisi kuwakataza kufanya miahadhara kama kawaida yao.
Katika barua yao waliyomwandikia Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Uamsho wamelaumu hatua ya jeshi hilo huku pia wakimlaumu Waziri wa Nchi Katika Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mohamed Aboud wakisema kuwa hana mamlaka ya kuwazuia kufanya hivyo.
Wameipongeza hotuba ya Rais Ali Mohamed Shein wakisema kuwa, haikukataza mihadhara badala yake alisisitiza amani.
Kamati ya Bunge
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Edward Lowassa amekemea vikali hali ya machafuko yaliyojitokeza hivi karibuni visiwani humo na kutamka kwamba amani ya nchi lazima ilindwe kwa gharama yoyote.

Lowassa, aliwapongeza Rais Jakaya Kikwete na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein kwa kukemea vitendo viovu vilivyofanywa na baadhi ya watu kisiwani humo pamoja na kulinda usalama wa taifa.

Akizungumza jana wakati wa harambee ya ujenzi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Elerai, Lowassa alionya kwamba amani ya nchi haiwezi kuchewa na watu wachache.

“Amani ya nchi italindwa kwa gharama yoyote ile, hatuwezi kuona amani ya nchi tuliyonayo inachezewa na watu wachache wenye nia mbaya,” alionya Lowasa.

No comments:

Post a Comment