Tuesday, June 5, 2012

Naibu Spika wa Bunge wa zamani afariki dunia

Naibu Spika wa Bunge wa zamani, Mathias Michael Kihaule, amefariki dunia katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), jijini Dar es Salaam, alikokuwa amelazwa.

Kwa mujibu wa taarifa Idara ya Habari, Elimu kwa Umma na Ushirikiano wa Kimataifa, Ofisi ya Bunge, jijini Dar es Salaam iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana, alifariki Jumapili ya Mei 3, mwaka huu.


Kihaule ambaye aliwahi kuwa Mbunge wa Ludewa, mkoani Iringa, alizaliwa Julai 19, 1933 na amefariki akiwa na umri wa miaka 79.



Licha ya kuwa mbunge wa jimbo hilo kwa kipindi cha miaka 15, kuanzia mwaka 1980-1995, Kihaule alilitumikia taifa katika wadhifa wa Naibu Spika wa Bunge.


Alikuwa na wadhifa huo katika kipindi chake cha tatu cha ubunge, kuanzia mwaka 1990 mpaka mwaka 1995.


Baada ya kipindi chake cha ubunge, aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, mkoani Mbeya, kuanzia mwaka 1995 hadi 2004.


Katika utumishi wake wa umma, Kihaule amewahi pia kushika nyadhifa kadhaa kitaaluma, ikiwamo Mkufunzi wa Vyuo mbalimbali vya Ualimu nchini.


Hadi alipofariki, alikuwa akijihusisha na shughuli mbalimbali za kilimo na ufugaji, na atakumbukwa na wananchi wa Ludewa kwa jinsi alivyokuwa akishirikiana nao katika  maendeleo ya jimbo na wilaya yake kwa kipindi chote alichokuwa bungeni na mara baada ya kumaliza muda wake wa ubunge.

 
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mipango ya mazishi inafanywa nyumbani kwa mtoto wake, Dk Anold Kihaule, Ilala Maghorofani, ambako ibada ya kuaga mwili itafanyika leo Msimbazi Centre kuanzia saa 6 mchana, kabla ya kusafirishwa kesho kwa ndege kwenda Ludewa kwa mazishi.
Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahala pema peponi. Amin.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment