Naibu Kamishna, Peter Kivuyo
Madai hayo ni kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Shirika la Maendeleo la Uingereza (DFID) katika Jeshi la Polisi nchini.
Mkuu wa Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Naibu Kamishna, Peter Kivuyo, alisema hayo alipokuwa akifungua mafunzo ya wakuu wa upelelezi wa wilaya nchini.
Alisema kutokana na utafiti huo, DFID imekubali kufadhili mafunzo kwa jeshi hilo ili kukabiliana na vitendo hivyo.
Alisema mambo yaliyoanishwa katika taarifa hiyo, ni pamoja na mapokezi duni kwa wateja, ucheleweshaji wa upelelezi wa mashauri ya jinai, ubambikizaji wa kesi, wizi wa mali za mahabusu na kuombwa rushwa ili kupatiwa huduma wanayohitaji wananchi wanapofika vituo vya polisi.
Kuhusu mafunzo hayo ya siku tano, alisema yanalenga kuimarisha mifumo iliyopo ya kupambana na vitendo vya ukiukwaji wa maadili hususan rushwa ndani ya jeshi hilo.
Alisema pia jeshi hilo limefanikiwa kupeleleza kwa ufanisi kesi za walemavu wa ngozi kwa watuhumiwa wengi kutotiwa hatiani na pia kubaini kwa kiwango kikubwa mitandao ya wasambazaji na watumiaji wa dawa za kulevya na wasafirishaji haramu wa binadamu.
“Ubambikizaji kesi kwa wananchi bado ni tatizo kwa upande wa Jeshi la Polisi na unaleta malalamiko mengi kutoka kwa wananchi,” alisema.
Alisema kutokana na usimamizi usio thabiti wa viongozi, askari wamekuwa wakiomba na kupokea rushwa kwa ajili ya kutoa dhamana kwa watuhumiwa kitu ambacho ni haki yao kisheria bila tozo ya aina yoyote.
Alitoa mfano mwingine kuwa ni askari kutumia lugha chafu na ya maudhi kwa wateja na hivyo kuharibu kabisa taswira ya Jeshi la Polisi kwa wananchi.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment