Waziri Mkuu mstaafu na mbunge wa Monduli amethibitisha nguvu kubwa ya kisiasa aliyonayo, baada ya kufanikiwa kushinda kwa kishindo nafasi ya ujumbe wa NEC wilaya ya Monduli.
Dr Suleshi Toure baada ya kuona hali mbaya kwa upande wake alitangaza kujitoa, na kusema anamwachia nafasi mgombea mwingine kijana Nanai Taon Konina.
Dalili za Lowassa ambaye wilayani Monduli anajulikana kama Simba, zilionekana mapema hata kabla ya mkutano, baada ya kuwepo taarifa ya kwamba wana ccm walipanga kumsindikiza kwa maandamano hadi kwenye ukumbi wa mkutano wa chuo cha ualimu Monduli.
Akijinadi mbele ya wapiga kura waliyokuwa wakimshangilia muda wote, Lowassa alijivunia mafanikio makubwa ambayo wilaya ya Monduli imeyapata katika sekta ya elimu, afya na barabara, huku uhai wa chama ukiwa mkubwa tofauti na wilaya nyingine za mkoa wa Arusha.Mkoa wa Arusha ndiyo ngome kuu ya chama cha upinzani cha CHADEMA.
''Mtu akiniuliza kwanini nagombea tena nafasi hii ya ujumbe wa NEC, nitamjibu kwa jeuri kwamba nimefanikiwa kuifanya Monduli kuwa moja ya wilaya bora nchini''alisema Lowassa na kushangiliwa. Lakini Dr Toure, alikuwa na wakati mgumu wa kujieleza ambapo alidai kuwa haridhishwi na kiwango cha maendeleo kilichofikiwa katika wilaya hiyo, kauli iliyowafanya wajumbe wa mkutano huo mkuu wa wilaya kumzomea.Na hata alipotangaza kuwa anajitoa, alizomewa.
Mkurugenzi wa uchaguzi huo Athman Sheshe alisema kuwa kwa mujibu wa taratibu, hata kama mgombea ametangaza kujitoa lakini jina litapigiwa kura.
Hali ilikuwa mbaya zaidi kwa mgombea mwengine Nanai Taon Konina, ambapo alionekana kushindwa kujieleza vizuri, hata alipoulizwa swali na mmoja wa wpaiga kura kuwa hakuwa mwanachama halali wa CCM bali ni wa CHADEMA alibabaika na kushindwa kujibu.Msimamizi wa uchaguzi aliingilia kayi kumsadia kwa kumwambia aombe kura na asijibu swali hilo.
Ushindi huo wa Lowassa unazidi kudhihirisha mvuto mkubwa aliyonao mwanasiasa huyo ndani ya CCM.Waziri mkuu mwenziye mstaafu Fredrik Sumaye hapo juzi alikikwaa kisiki baada ya kushindwa na Dr Mary Nnagu katika nafasi ya ujumbe wa NEC wilayani Hanang.
No comments:
Post a Comment