Muungano wa Afrika umeiruhusu tena Mali kuwa mwanachama baada ya kusimamisha kwa muda uanachama wake mwezi Machi kufuatia mapinduzi ya kijeshi.
Muungano huo pia umeidhinisha mpango wa Mali kuitisha uchaguzi mkuu na kuirejesha nchi katika hali ya utulivu , kwa mujibu wa msemaji wa AU.
Eneo hilo lilitwaliwa na waasi baada ya vurugu zilizotokea katika mji mkuu, Bamako mwezi Machi.Maafisa wa Muungano huo pia wamekuwa wakijadili mipango ya kutuma vikosi vya jeshi kusaidia wanajeshi wa Mali kudhibiti maeneo yaliyotwaliwa na wapiganaji wa kiisilamu Kaskazini mwa nchi.
''Baraza la usalama na ulinzi la Umoja wa Afrika, uliamua kuirejesha Mali kwenye uwanachama wake na kwa hivyo nchi hiyo inakaribishwa kushiriki kikamilifu.'' alisema Ramtane Lamamra, msemaji wa baraza hilo .
AU pia inakamilisha mipango yake ya kutuma vikosi vya wanajeshi wa Afrika nchini Mali kulingana na mwenyekiti wa tume ya AU Nkosazana Dlamini-Zuma.
''Hata hivyo, serikali itatoa fursa kwa wapiganaji ambao wanataka kufanya mazungumzo nayo.'' aliongeza Bi Zuma.
Mapinduzi ya mwezi Machi, yalifanywa na wanajeshi waliopindua serikali ya Rais Amadou Toumani Toure, wakidai kuwa serikali yake ilikosa kukabiliana vilivyo na waasi wa Tauareg.
Baada ya mapinduzi , wapiganaji wa kiisilamu walidhibiti miji ya Kaskazini mwa Mali wakishirikiana na waasi wa Tuareg, lakini ushirkiano wao ulivunjika.
Mapema mwezi huu, baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, lilipitisha azimio la kuruhusu jeshi kuingilia hali nchini Mali na kuyataka mashirika ya Afrika kubuni mkakati wa jeshi la pamoja katika muda wa siku arobaini na tano.
No comments:
Post a Comment