Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo Duniani, FAO limeonya kuwa nchi za Algeria, Libya, Mauritania na Morocco yamkini zikakumbwa na baa la nzige wiki chache zijazo na hivyo zimetakiwa kujiandaa kukabiliana na wadudu hao waharibifu.
Katika tahadhari hiyo FAO imesema nzige hao watatokea eneo la Sahel la Afrika Magharibi.
Mtaalamu mwandamizi wa utabiri wa mwelekeo wa nzige katika FAO Keith Cressman amesema wadudu hao wanatokea Chad, Mali na Niger na wakifika katika nchi hizo wanaweza kuharibu malisho ya wanyama na mazao wakati huu ambapo wanatishia mavuno huko wanakotokea.
Cressman amesema FAO imeweza kufuatilia na kudhibiti mwelekeo wa nzige kutoka Niger na Chad kwa kupulizia dawa lakini inashindwa kufanya hivyo nchini Mali.
Halikadhalika, FAO imeomba msaada zaidi wa kifedha kufikia lengo lake la dola Milioni 10 kwa ajili ya operesheni za kudhibiti nzige ambapo hadi sasa imepata dola Milioni Moja nukta Nne tu.
No comments:
Post a Comment