Friday, February 15, 2013

Waumini wataka kiongozi kuachiliwa kwa dhamana TZ


Jeshi la Polisi Nchini Tanzania limezima maandamano yaliyopangwa na Baadhi ya Waumini wa Kiislamu Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kumlazimisha Mkurugenzi wa Mashtaka-DPP kuruhusu dhamana ya Kiongozi wa Kidini.
Waandamanaji hao wamepigwa marufuku licha ya kuwa waliomba kibali cha kuandamana ili wamuombe DPP atoe idhini ya dhamana kwa kiongozi huyo ambaye ni Katibu wa Shura ya Maimamu na Jumuiya za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda na Wenzake.
Akizungumza na waandishi wa habari Kaimu Kamanda wa Polisi kanda Maalum ya Dar es Salaam, Ahmed Msangi, amesema pamoja na kuwa jeshi lake halina askari wa kutosha kuwalinda waandamanaji hao lakini pia taarifa zimeonyesha kuwa kuna baadhi ya watu wamepanga kufanya vurugu kupitia maandamano hayo.
Makundi ya askari polisi wakiwa na silaha pamoja na mbwa wamezunguka mitaa yote ya katikati ya jiji la Dar es Salaam kuhakikisha hakuna kundi lolote la watu wenye kuelekea zilipo ofisi za Mkurugenzi huyo.
Katika makutano ya mitaa ya Sokoine Drive na Ohio zilipo ofisi za DPP kumekuwa na ulinzi mkali wa vikosi vya askari polisi wakifanya doria hapo tangu asubuhi na mapema.
Waandamanaji hao walipanga kuanza maandamano yao mara tu baada ya kumaliza sala ya Ijumaa katika misikiti mbalimbali ya jijini kuelekea zilipo ofisi hizo.
Taarifa zinasema waandamanji hao wameongeza msukumo wa kudai dhamana ya Sheikh Ponda na wenzake baada ya Elizabeth Michael Msanii wa filamu anayetuhumiwa kumuuwa msanii mwenzake Steven Kanumba kupewa dhamana hivi karibuni.
Sheikh Ponda na wenzake 45 walitiwa nguvuni mwishoni mwa mwaka jana na kesi yao itaendelea kusikilizwa Februari 25 wakikabiliwa na mashitaka manne likiwemo la kuchochea vurugu na uvamizi wa eneo la kampuni moja isivyo halali

habari na bbc swahili

No comments:

Post a Comment