Friday, August 2, 2013

WIZARA YA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA NA WATOTO: MTANDAO WA MAWASILIANO WASAIDIA KUPUNGUZA UKATILI


Msemaji wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, jinsia na Watoto, Erasto Ching‘oro (kushoto), akizungumza na waandishi wa habari leo, jijini Dar es Salaam, kuhusu mafanikio waliyoyapata tangu kuzinduliwa kwa Mtandao wa Mawasiliano ya Kuwasaidia Watoto wanaofanyiwa Ukatili Na. 116 (Child Help Line), Idara ya Habari, Maelezo. Kulia ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari, Zamaradi Kawawa. (Picha zote na Eliphace Marwa)


Msemaji wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, jinsia na Watoto, Erasto Ching‘oro (kushoto), akizungumza na waandishi wa habari leo, jijini Dar es Salaam, kuhusu mafanikio waliyoyapata tangu kuzinduliwa kwa Mtandao wa Mawasiliano ya Kuwasaidia Watoto wanaofanyiwa Ukatili Na. 116 (Child Help Line), Idara ya Habari, Maelezo. Kulia ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari, Zamaradi Kawawa.

Ndugu Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari, MAELEZO,
Ndugu Wanahabari,
Mabibi na Mabwana,

Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi ya kukutana nanyi; napenda pia kuwashukuru ninyi Wanahabari kwa kuweza kuhudhuria kikao hiki.

Mnamo tarehe 14 Juni, 2013, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto kwa kushirikiana na wadau wa masuala ya watoto ilizindua Mtandao wa Mawasiliano ya Kuwasaidia Watoto wanaofanyiwa Ukatili Na. 116 (Child Help Line). Mtandao huu ulizinduliwa kutokana na kuwepo kwa matukio mengi yaliyokithiri ambayo yamekuwa yakiwakabili watoto hapa nchini. Madhumuni ya uzinduzi wa mtandao wa mawasiliano na 116 ni kuwezesha watoto na jamii kwa kuripoti matukio ya ukatili wanaofanyiwa watoto ili kuwaunganisha na mamlaka husika kuhakikisha kuwa mtoto anapata huduma na ulinzi stahiki.

Ukatili huo ni pamoja na kubakwa, kuchomwa moto, kutelekezwa, unyanyasaji mbalimbali na wakatai mwingine kuuawa. Ukatili huo kwa kiasi kikubwa umekuwa ukiathiri maendeleo ya watoto, makuzi ya watoto pamoja na kuwasababishia madhara ya kisaikolojia.

Ndungu Wanahabari,
Matokeo ya Utafiti uliofanywa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto (2009)  kwa kushirikiana  na wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Afya ya Sayansi na Tiba cha Muhimbili, UNICEF pamoja na Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC) ambao ulihusu kuelewa tatizo na sura ya ukatili wa kijinsia, kimwili na kiakili wanaofanyiwa  watoto nao ulichangia kuona umuhimu wa kuwa na mtandao wa mawasiliano ili kusaidia utoaji wa taarifa ya matukio ya ukatili na kuwaunganisha watoto na wasimamizi wa ulinzi wa mtoto.

Kutokana na ukweli kwamba, matokeo ya utafiti huu yalionyesha kuwa kuna kiwango kikubwa cha ukatili dhidi ya watoto na matukio mengine ya ukatili dhidi ya watoto yamekuwa yakifanyika ama shuleni, nyumbani na ndani ya jamii. Hali hii ilipelekea wadau wa masuala ya watoto  kuandaa Mpango Mkakati wa mwaka mmoja wa Kushughulikia Tatizo la Ukatili Dhidi ya Watoto (2012 – 2013); na hatimaye kuandaa Mpango wa Miaka Mitatu wa kushughulikia tatizo hilo (2013 – 2016) ambao ulizinduliwa mkoani Dodoama mwezi Aprili, 2013.

Ndugu Wanahabari,
Pamoja na jitihada za Serikali kuhakikisha kwamba kunakuwepo na Sera ya Maendeleo ya Mtoto (2008), Sheria ya Mtoto Namba 21 ya mwaka 2009, uanzishaji wa Madawati ya Jinsia na Watoto katika vituo mbalimbali vya polisi nchini; bado Wizara na wadau tuliona kuna umuhimu wa kuwa na chombo kingine ambacho kitasaidia upatikanaji wa taarifa za matukio ya ukatili kwa watoto ili kuwaunganisha watoto na taasisi zinazotoa huduma ya stahiki kwa watoto walioathirika.

Mapema tarehe 3 Januari, 2013 Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto ilifikia makubaliano na Asasi isiyokuwa ya Kiserikali ya C-sema kuhusu uendeshaji wa mtandao wa mawasiliano ya matukio ya ukatili dhidi ya watoto Na 116 ili kuripoti matukio ya ukataili wanaofanyiwa na kuwasilisha taarifa hizo kwa watoa huduma. Kwa kuanzia, Mtandao huu unafanya kazi katika Wilaya na Manispaa za Temeke, Magu, Bukoba Vijijini, Musoma Mjini, Kasulu, Hai, Manispaa za Ilala na Kinondoni kama eneo la majaribio.

Mafanikio;
Ndugu wanahabari,
Toka mtandao huu ulipozinduliwa ni kipindi cha mwezi mmoja na takriban wiki tatu. Hata hivyo mtando umeonesha mafanikio kwa kuwepo mwitikio mkubwa kwa wananchi katika kutoa taarifa za ukatili kwa watoto na kuonesha umuhimu wa upatikanaji wa msaada wa kisheria na hivyo kuharakisha jukumu la utoaji wa huduma kwa mtoto aliyefanyiwa ukatili katika maeneo mbalimbali.

Tangu kuanzishwa Mtandao wa Mwasiliano ya Msaada wa Kuzuia Ukatili wa Watoto mapema tarehe 12 Mei 2013 kumekuwepo na mafanikio makubwa. Kwa kipindi kinachoishia tarehe 18 Julai 2013 kiasi cha simu 1,146 zilipokelewa kutoka mikoa mbalimbali. Kati ya simu hizo, simu 235 zilihitaji kufahamu jinsi mtandao unavyofanya kazi na namna ya kuripoti matukio ya ukatili.Simu 29 zilihitaji huduma ya ushauri na msaada zaidi ambapo taarifa za matukio ya ukatili zilipelekwa kwa Kamati za Ulinzi na Usalama wa Mtoto katika ngazi ya Wilaya kwa ajili ya ufuatiliji. Kamati hizi zinahusisha Maafisa Ustawi wa Jamii wa halmashauri, Maafisa Maendeleo ya jamii, Polisi- Dawati la Jinsia na watoto.

Ndugu Wanahabari,
Takwimu hizi zinaonesha mafanikio makubwa ya matumizi ya namba 116, kutokana na ukweli kwamba wakati wa uzinduzi tarehe 14 Juni 2013 ilielezwa kuwa kulikuwa na jumla ya miito ya simu 267. Kati ya simu hizo, simu 64 zilipokelewa wiki ya kwanza, wiki ya pili miito 96 na hadi siku ya uzinduzisimu 107.

Hadi sasa kuna ongezeko la simu 939 kwa kipindi cha mwezi mmoja. Idadi hii ya miito ya simu inaashiria kuwa kunamwitikio mkubwa kutoka kwa wananchi katika kuripoti ukatili dhidi ya watoto katika maeneo tunakoishi. Vilevile, taarifa hizi ni kielelezo cha kuwepo kwa matukio ya ukatili wanaofanyiwa watoto katika familia na jamii kwa ujumla..  

Hili linathibitishwa na baadhi ya kesi ambazo zinaripotiwa na wananchi likiwemo tukio ambalo lilifanyika Mkoani Arusha ambapo raia mwema kwa niaba ya mama mzazi wa mtoto alipiga simu akiripoti tukio la ukatili aliofanyiwa mtoto wa kike (umri 12) ambaye alitekwa na bwana mmoja, alimbaka mtoto huyo na kisha mbakaji akamshikilia binti huyo mwanafunzi wa darasa la sita na kuendelea kuishi naye kama mke.

Ndugu wanahabari,
Kuwepo kwa mawasiliano ya msaada wa simu Namba 116 kuliweza kusaidia kumwokoa mtoto huyo kwa ushirikiano kutoka Jeshi la Polisi Arusha ambao waliweza kumrejesha mtoto huyo nyumbani na kuendelea na masomo yake. Hivyo, Wizara inazidi kuwaomba ninyi wanahabari kuendelea kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kutumia huduma hii ili kwa pamoja tuweze kuzuia na kudhibiti ukatili dhidi ya watoto. Juhudi hizi zikiunganishwa na jitihada za vyombo vya habari na wadau wengine tutaendeleza azma ya kuwa na jamii inayowajali na kuwalinda watoto.

Aidha ni matumaini ya Wizara kuwa wadau mbalimbali wataendelea kujitokeza kushirikiana na Wizara na asasi ya C-Sema katika kuhakikisha kuwa huduma hii ya mawasilino inapatikana katika maeneo yote hapa nchini katika muda muafaka ili kuhakikisha kuwa watoto wetu wanapata ulinzi wa kutosha, na kwamba kila mwananchi anawajibu wa kuwalinda watoto na kuzuia vitendo vya ukatili.  

Ndugu Wanahabari,
Wizara inaendelea kuhimiza jamii kubadilika na kuhakikisha kuwa familia ambayo ndio kitovu cha jamii panakuwa ni mahala salama penye upendo amani na mshikamano miongoni mwa wanafamilia; na kuwapatia watoto haki zao za msingi ikiwemo haki ya kuishi, kulindwa, na kuendelezwa.

Jamii inapaswa kukumbuka kwamba Haki ya mtoto ya kuishi ni haki yao ya Kikatiba, hivyo kumnyima mtoto haki hiyo ni kukinzana na Mkataba wa Kimataifa wa Haki na Ustawi wa Mtoto, Sera ya Maendeleo ya Mtoto na Sheria ya Mtoto Na. 21 (2009). Hivyo, jamii inawajibu wa kulinda na kutetea utu na uhai wa mtoto, ili kuhakikisha kuwa watoto wanaishi kwa amani, furaha, uhuru na utulivu.

Mwisho napenda kuwashukuru wanahabari kwa kuendelea kufichua na kuripoti taarifa nyingi za ukatili wanaofanyiwa watoto kutoka katika maeneo mbalimbali. Napenda kuwathibitishia kuwa taarifa zenu zimekuwa kikifanyiwa kazi na mamlaka husika katika ngazi mbalimbali ili kuwasaidia watoto wetu wanaokumbwa na ukatili. Kwa pamoja tunaweza kumlinda mtoto wa Tanzania na kumwekea mazingira rafiki.
Asanteni kwa Kunisikiliza
ErastoT. Ching‘oro
Msemaji
Wizara ya Maendeleo ya Jamii, jinsia na Watoto

No comments:

Post a Comment