Saturday, September 7, 2013

Ushiriki wa Jeshi la Tanzania katika kulinda Amani Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC)


Msemaji wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Meja Erick Komba, akizungumza na waandishi wa habari, Makao Makuu ya jeshi hilo, Upanga jijini Dar es Salaam kuhusu kupotoshwa habari za kazi za jeshi hilo nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), chini ya Jeshi la Kulinda amani la Umoja wa Mataifa (MONUSCO). Kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari, Maelezo, Assah Mwambene. (Picha zote na Anna Nkinda-Maelezo na Kassim Mbarouk-www.bayana.blogspot.com)
Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) Assah Mwambene akiongea na waandishi wa habari jinsi baadhi ya vyombo vya habari vinavyoandika taarifa zisizo  sahihi  kuhusu  ushiriki wa  majeshi ya Tanzania katika operesheni ya ulinzi na amani katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ikiwa ni sehemu ya SADC standby brigade inayotoa mchango wake katika Jeshi la Umoja wa Mataifa (MONUSCO)  . Kushoto ni Msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Meja Erick Komba.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) Assah Mwambene (kulia) akimuonyesha kitu Msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Meja Erick Komba wakati wa mkutano na waandishi wa habari  uliofanyika   leo katika ukumbi wa mikutano uliopo makao makuu ya JWTZ jijini Dar es Salaam.  Mkutano huo uliongelea juu ya ushiriki wa Tanzania katika operesheni ya ulinzi na amani katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).  
Mwandishi wa Habari na Mpiga picha Mwandamizi wa kituo cha Televisheni  cha channel 10 Kibwana Dachi akiuliza maswali  wakati wa mkutano uliofanyika   leo katika ukumbi wa mikutano wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi  wa Tanzania (JWTZ) jijini Dar es Salaam.  Mkutano huo uliongelea juu ya ushiriki wa Tanzania katika operesheni ya ulinzi na amani katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).  Wanaomsikiliza kwa makini ni Msemaji wa JWTZ Meja Erick Komba (kushoto) na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) Assah Mwambene(kulia).
Msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Meja Erick Komba akiongea na waandishi wa habari  leo katika ukumbi wa mikutano uliopo makao makuu ya Jeshi hilo  jijini Dar es Salaam kuhusu ushiriki wa Tanzania katika operesheni ya ulinzi na amani katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC). Tanzania ni moja kati ya nchi tatu zilizopeleka kikosi chake nchini DRC ikiwa ni sehemu ya SADC standby brigade inayotoa mchango wake katika Jeshi la Umoja wa Mataifa (MONUSCO) na kinafanya kazi chini ya Force Commander  huku majukumu yake yakiwa ni kujizuia waasi kujitanua, kuvunja nguvu ya waasi na kuwapokonya silaha makundi yote ya waasi.
Waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari wakimsikiliza Msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Meja Erick Komba (hayupo pichani) wakati akiongea nao leo jijini Dar es Salaam kuhusu ushiriki wa Tanzania katika operesheni ya ulinzi na amani katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).  
Picha na Anna Nkinda - Maelezo.



Na Lorietha Laurence-Maelezo
JESHI la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania limetoa taarifa ya maendeleo ya  wanajeshi wanaoshiriki  kulinda amani kwa nchi mwanachama wa maziwa makuu Jamuhuri ya Demokrasia ya Kongo eneo la Goma.

Taarifa hiyo imetolewa na msemaji wa Jeshi hilo Meja Erick Komba alipokuwa akiongea na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam.

Meja Komba alisema kuwa  baadhi ya vyombo vya habari na mitandao ya Kijamii hususan “blogs” kuandika taarifa zisizo rasmi ambazo zinapotosha umma kuhusu ushiriki wa Jeshi la Tanzania katika nchi ya Kongo.

 Alieleza kuwa  jeshi la Tanzania  linashiriki kulinda amani Nchini Kongo kutokana na Rais wa nchi hiyo Mhe.Joseph Kabila kuwasilisha ombi katika kikao  cha nchi za maziwa  makuu  kilichofanyika Julai 12 mwaka jana mjini Addis Ababa, Ethiopia baada ya waasi wa M23 kujitenga na Serikali na kuanzisha mapambano.

“Ushiriki wa Jeshi la Tanzania katika kulinda amani nchini Kongo umetokana na ombi liliwasilishwa na Rais Mhe. Joseph Kabila kwa nchi wanachama wa maziwa makuu ambazo ni Rwanda,Uganda,Tanzania na  DRC  kusaidia kulinda amani na kuwapokonya waasi wa M23 silaha”alisema Meja  Komba .

Meja Komba aliongeza  kuwa, jeshi la Tanzania ni sehemu ya SADC Standby brigade  iliyotoa mchango wake katika jeshi la Umoja wa Mataifa (MUNUSCO) kinachofanya kazi chini ya “Force Commonder” ambapo  majukumu yake makubwa ni kuzuia waasi kujitanua, kuvunja  nguvu za  waasi na kuwapokonya silaha makundi yote ya waasi.

Naye Msemaji wa Serikali ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo Bw. Assah aliwaomba waandishi na wadau mbalimbali wa habari kuandika habari zenye uhakika na ambazo hazitapotosha umma.

“Nawaomba waandishi na wadau wa habari tuwe tunatoa taarifa zilizo sahihi ili tusipotoshe umma ukizingatia jeshi letu lipo huko kwa ajili ya kulinda amani na siyo kupigana na M23,” alisema Mwambene.

Jeshi la Ulinzi la Wananchi  Kikosi cha Tanzania  kiko chini ya MUNUSCO ambao ndio wanaoendesha  operasheni ya kulinda amani na Tanzania  haipigani na M23 wala haina tatizo na Rwanda kuhusiana na operesheni hiyo.

Pia Rwanda imesaidia Tanzania kwa kuruhusu kikosi kupitisha watu, vifaa na zana  kuelekea Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

No comments:

Post a Comment