Sunday, December 15, 2013

Kilio cha Rushwa chazidi kuitesha Serikali


Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Goodluck Ole-Medeye (katikati), akiongoza wahitimu wa Mahafali ya 15 ya Chuo cha Uhasibu Arusha (AII) kuelekea kwenye viwanja vya chuo hicho, muda mfupi kabla ya kuwatunuku vyeti kwenye fani mbalimbali mkoani humo mwishoni mwa wiki, wa kwanza ( kushoto) ni Mkuu wa Chuo hicho Prof Johannes Monyo, na Mwenyekiti wa Bodi ya uongozi wa (AII), Mwanaidi Mtanda.
Wahitimu wa Chuo cha Uhasibu Arusha (AII), wakivaa kofia zao muda mfupi baada ya kutunukiwa vyeti vya fani mbalimbali zinazotolewa chuoni hapo, kwenye sherehe za mahafali ya 15 zilizofanyika kwenye viwanja vya chuo hicho mwishoni mwa wiki.

Kukithiri kwa vitendo vya rushwa na ubinafsi ndani ya idara na taasisi za serikali nchini kumeelezwa kuwa ni chanzo na ‘mwiba’ unaorudisha nyuma juhudi na mipango madhubuti inayofanywa kila siku na serikali dhidi ya wimbi la umasikini

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Goodluck Ole-Medeye, ameyasema hayo mkoani hapa, mwishoni mwa wiki, wakati akihutubia kwenye  sherehe za mahafali ya 15 ya Chuo cha Uhasibu Arusha

“Sehemu ya fedha za walipakodi huishia kwenye midomo ya walafi wachache ambao baadhi yao ni  viongozi wasio waadilifu wenye dhamana ya kusimamia miradi ya maendeleo ya taifa letu ,”  alisema Medeye na kuongeza:

“Nawaomba wale watakaobahatika kuteuliwa kuwa wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba wasimame imara na kusema kwa sauti moja kuwa rushwa itamkwe na Katiba kuwa adui wa Taifa na hivyo katiba iweke adhabu kali kwa watakaojihusisha nayo.”

Aliwataka wahitimu na wadau wengine kushirikiana kutoa elimu juu ya ubaya wa rushwa kwa mustakabali mzuri wa amani ya taifa ili kufikia maendeleo ya kijamii, kiuchumi na upevu wa kisiasa wanaoutarajia

Katika hatua nyingine Dk Medeye aliwaasa wanafunzi wote nchini hususan wale wanaotoka vyuoni kutumia fursa ya teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama) katika ushindani wa soko la ajira la Jumuiya ya Afrika Mashariki na kimataifa kwa kusoma na kujua mambo mengi ya kiweledi.

 “Tumieni simu na kompyuta zenu kutafuta taarifa za kiushindani kitaifa na kimataifa na hasa ushindani wa soko la ajira msiitumie mitandao hiyo vibaya..tumieni kwa kupata vitabu, majarida na taarifa za utafiti zenye manufaa kwenu kimasomo,” alisema

 Alisikitishwa na vitendo vya wanafunzi walio wengi kutumia vibaya fursa ya Tehama, kwa kutafuta taarifa zilizo kinyume na maadili ya taifa au kupiga gumzo ‘kuchat’ hususan wanapokuwa wakiperuzi mitandao ya kijamii ikiwemo Twitter, Google na Facebook 

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa (IAA), Mwanaidi Mtanda, alisema chuo hicho kina mpango wa kufungua kampasi nyingine mkoani Mwanza, na pia kwa sasa kipo kwenye maandalizi ya kufungua kampasi mjini Babati-Manyara, lengo ni kutoa fursa kwa watanzania katika muktadha wa ongezeko la ubora wa elimu na idadi ya wanafunzi.

Aliongeza kuwa Chuo hicho cha Uhasibu kwa mwaka huu kimeanzisha Stashahada za Uzamili za Uhasibu, na Ugavi na Manunuzi. Pia kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Conventry cha Uingereza, na kile cha Galgotias nchini India tayari wameanza kutoa kozi mbalimbali zikiwemo Stashahada na Shahada za Uzamili kwa masomo ya kutwa na jioni

Aidha katika hali ya kusisitiza, Mtanda aliomba serikali kuongeza kasi katika kusaidia kutatua changamoto za uhaba wa mabweni na vyumba vya madarasa.

“Kama tunavyosikia kwenye vyombo vya habari usalama wa wanachuo katika vyuo vikuu mbalimbali nchini upo hatarini, majambazi yanawavamia wanavyuo, yanawapora, kuwaibia, kuwajeruhi au wakati mwingine kuwaua,” alisema.

Awali, Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Johannes Monyo, alisema jumla ya wanafunzi 1,510 wamehitimu na kutunukiwa vyeti katika fani mbalimbali zaidi ya 29, zikiwemo za Benki, Ugavi na Manunuzi, Uhasibu, Kodi, Usimamizi wa Fedha, Sayansi ya Komputa na Teknolojia ya Habari.

No comments:

Post a Comment