Balozi
Mdogo wa Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China Bwana Xie Yunliang
akisalimiana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
Hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Balozi
Mdogo wa Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China Bwana Xie Yunlia
aliyefika Ofisini kwake kusalimiana naye. Picha na Hassan Issa wa – OMPR
– ZNZ.
Serikali
ya Jamuhuri ya Watu wa China imesisitiza kuendelea kuunga mkono
harakati za Kiuchumi na Maendeleo za Wananchi wa Zanzibar kwa kusaidia
miundo mbinu sambamba na ufadhili katika miradi tofauti kwa lengo la
kustawisha Jamii.
Kauli
hiyo imetolewa na Balozi Mdogo wa Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China
aliyepo hapa Zanzibar Bwana Xie Yunliang alipokuwa akizungumza na Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Ofisini kwake
Vuga Mjini Zanzibar.
Balozi
Xie Yunliang alisema Miradi ya Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya Zanzibar
kama vile ujenzi wa Hospitali ya Abdula Mzee Mkoani Pemba na Uwanja wa
Ngege wa Zanzibar ni uthibitisho kamili wa Ushiriki wa China katika
kusaidia maendeleo ya Zanzibar.
Balozi
huyo mdogo wa China hapa Zanzibar alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar kwamba tayari ameshafanya ziara maalum ya kukagua baadhi ya
miradi inayosimamiwa na Nchi hiyo pamoja na kukutana na Taasisi na
wahandishi wa miundo mbinu na makampuni ya Nchi hiyo yanayofanya kazi
hapa Zanzibar na kuridhika na hatua inayoendelea kuchukuliwa na Taasisi
hizo.
Balozi
Xie aliiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuharakisha upatikanaji
wa eneo lililokubaliwa kutumiwa katika upanuzi wa Hospitali ya Abdulla
Mzee Mkoani Pemba ambalo bado linaonekana kuendelea kuwepo baadhi ya
majengo ya ibada na Makazi ya Watu.
Alisema
upatikanaji wa eneo hilo utasaidia kurahisisha ukamilishaji wa ujenzi
wa Hospitali hiyo kwenda kwa wakati uliopangwa ili kuepuka hasara
zinazoweza kuleta usumbufu hapo baadaye.
Akizungumzia
suala la uwanja wa Michezo wa Mao Tse Tung uliopo Mtaa wa Kikwajuni
Mjini Zanzibar Balozi Mdogo wa China hapa Zanzibar Bwana Xie Yunliang
alisema ushauri wa suala hilo tayari limeshawasilishwa kwa Serikali ya
China kwa hatua za utekelezaji.
Alifahamisha
kwamba Serikali ya Jamuhuri ya China inathamini sana uwamuzi wa
Zanzibar wa uwanja huo kuitwa jina la Mwenyekiti wa Chama cha
Kikoministi cha Nchi hiyo Mao Tse Tung na kuahidi kwamba mipango
itaandaliwa katika kuona kiwanja hicho kinapatiwa hadhi kama kilivyo
jina lake.
Aliipongeza
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ukarimu wake wa kuuhudumia Ujumbe
wa China ulioshiriki maadhimisho ya sherehe za kutimia miaka 50 ya
Mapinduzi ya Zanzibar ukiongozwa na Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya
Makazi ya Nchi hiyo.
Alisema
ujumbe huo umefarajika na mapokezi makubwa uliyoyapata ambayo
yamethibitisha uhusiano wa Kihistoria na wa muda mrefu uliopo kati ya
Zanzibar na Jamuhuri ya Watu wa China.
Naye
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliishukuru
Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China kwa misaada yake mbali mbali
inayotowa kwa Zanzibar ambayo imepunguza kasi ya ukali wa maisha.
Balozi
Seif litolea mfano wa Ujenzi wa Hospitali ya Abdulla Mzee iliyopo
Mkoani Pemba ambao kwa kiasi kikubwa utakapokamilika kwake utapunguza
usumbufu kwa Wananchi wa Kisiwa cha Pemba wa kufuata huduma za Afya
Kisiwani Unguja.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimuahidi Balozi Mdogo huyo wa Serikali ya
Jamuhuri ya Watu wa China kwamba uhusiano kati ya pande hizo mbili
utaendelea kuimarisha kwa faida ya wananchi wake.
China
imekuwa mshirika mkubwa wa Zanzibar katika kusaidia maendeleo mbali
mbali mara tu baada ya Zanzibar kufanya Mapinduzi ya mwaka 1964 y a
kuondosha utawala wa kikoloni.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
5/2/2014.
No comments:
Post a Comment