Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw. George D. Yambesi akifungua mkutano wa wadau kuhusu Mikataba ya Utendaji Kazi katika Taasisi za Umma katika hoteli ya Serena jijini Dar es salaam. Mkutano huo uliandaliwa mahsusi ili wadau waweze kufahamu mambo muhimu juu ya Mfumo wa Mikataba ya Utendaji Kazi hususan chimbuko, maana na faida zake, mambo ya msingi yatakayofanikisha utekelezaji wa mfumo huo, fomu ya mkataba wa utendaji kazi na vipengele vyake, vigezo vya upimaji wa utendaji kazi wa taasisi, wahusika wa mikataba na utaratibu wake; utaratibu wa kutoa taarifa za mikataba ya utendaji kazi, utaratibu wa kutathmini mikataba ya utendaji kazi; utaratibu wa kushindanisha Taasisi za Umma; na Taasisi zinazopendekezwa kuingia katika Mikataba ya Utendaji Kazi . Sambamba na hilo wadau walipata fursa ya kutoa maoni, ushauri na mapendekezo juu ya mfumo wa Mikataba ya Utendaji Kazi, na namna bora ya kuitekeleza katika Taasisi za Umma. Wadau walioshiriki mkutano huo ni pamoja na watendaji na watendaji wakuu wastaafu katika Taasisi za Umma wakiwemo Makatibu Wakuu wastaafu, watendaji wakuu wa Asasi za Kiraia (AZAKI), wanataaluma kutoka vyuo vya Elimu ya juu, wawakilishi kutoka katika sekta binafsi na Washauri waelekezi Wanaojitegemea.
Sehemu ya baadhi ya wadau walioalikwa katika Mkutano kuhusu Mikataba ya Utendaji Kazi katika Taasisi za Umma wakimsikiliza mgeni rasmi Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw. George D. Yambesi (hayupo pichani).
Wadau walioshiriki mkutano kuhusu Mikataba ya Utendaji Kazi katika Taasisi za Umma wakiwa katika picha ya pamoja na mgeni rasmi Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw. George D. Yambesi (wa sita kutoka kulia mstari wa mbele), kulia kwake ni Naibu Katibu Mkuu Bw. HAB Mkwizu na kushoto kwake ni Mkurugenzi wa Idara ya Uchambuzi na Ushauri Kazi Bw. Mick Kiliba.
Katibu Mkuu mstaafu Bibi Ruth Mollel akitoa mchango wake wakati wa Mkutano kuhusu Mikataba ya Utendaji Kazi katika Taasisi za Umma.
Katibu mstaafu Tume ya Utumishi Bibi Thecla Shangali akitoa maoni yake kuhusu Mikataba ya Utendaji Kazi katika Taasisi za Umma.
Wadau wakiwasilisha maoni na mapendekezo baada ya kufanya kazi ya vikundi kuhusu Mikataba ya Utendaji Kazi katika Taasisi za Umma.
Mdau kutoka AZAKI ya FORDIA akitoa mchango wake kuhusu Mikataba ya Utendaji Kazi katika Taasisi za Umma.
Mkurugenzi wa Idara ya Uchambuzi na Ushauri Kazi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw. Mick Kiliba akiwashukuru wadau kwa mchango, ushauri na maoni waliyowasilisha kuhusu Mikataba ya Utendaji Kazi katika Taasisi za Umma.
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw. HAB Mkwizu akifunga mkutano wa wadau kuhusu Mikataba ya Utendaji Kazi katika Taasisi za Umma uliofanyika katika hoteli ya Serena jijini Dar es salaam.
Serikali imeamua kuanzisha mfumo wa Mikataba ya Utendaji Kazi ambao utahusisha kuchagua vipaumbele, malengo, shabaha,vigezo na viashiria vya utendaji kazi ambavyo vitatumika kupima utendaji kazi wa taasisi kila mwisho wa mwaka.
Akifungua mkutano wa wadau juu ya utekelezaji wa Mikataba ya Utendaji Kazi katika Utumishi wa Umma jana jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bwana George D. Yambesi alisema Mfumo huu utakuwa na faida na manufaa makubwa kwa Menejimenti za Taasisi za Umma, Watumishi, Serikali Sekta Binafsi, Asasi Zisizo za Kiserikali na Wananchi kwa ujumla.
Bwana Yambesi alisema pamoja na kwamba Serikali imechukua hatua za kuboresha utendaji kazi na utoaji huduma, kuongeza uwajibikaji na tija kwa kuweka mifumo mbalimbali , utekelezaji wa mifumo hiyo haijapata mafanikio makubwa sana kutokana na kukosekana kwa mfumo wa kupima utendaji kazi wa taasisi za Umma kila mwaka.
Alisema uzoefu wa utekelezaji wa mfumo huo katika nchi mbalimbali duniani mfano Kenya, Botswana, India na Pakistani umeonyesha kuwa na mafanikio makubwa ya kiutendaji, kuongeza tija na mapato ya Serikali hizo, kupunguza utegemezi wa wafadhili na washirika wa maendeleo, kuongeza ubora wa huduma za kiuchumi na kijamii, kuongeza uwezo wa ushindani wa nchi hizo katika soko la dunia na kuongeza kasi ya mandeleo ya nchi hizo.
Bwana Yambesi aliongeza kuwa Taasisi za Umma Duniani kote ni injini ya Serikali kwa kuwa zinatoa mchango mkubwa na muhimu katika kuongeza tija, kuboresha utoaji huduma, kupunguza umaskini na kuleta maendeleo ya Taifa kwa ujumla.
Kwa kutambua umuhimu na mchango wa Taasisi za Umma katika Taifa letu, tangu nchi yetu imepata uhuru, Serikali imeanzisha taasisi hizo na kuchukua hatua mbalimbali zikiwemo za kisera, kisheria na kimuundo ili kuimarisha utendaji katika taasisi hizo na kuzijengea uwezo ili ziweze kutoa huduma bora kwa Umma.
Alitoa mfano kuwa kuanzia miaka ya 1990 hadi sasa, Serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kuweka mifumo ya utendaji kazi katika taasisi hizo kama msingi wa kuongeza tija, kuimarisha utendaji unaojali matokeo na utoaji huduma bora kwa Umma.
Aliongeza kuwa katika kipindi hicho yamepatikana mafanikio makubwa katika utoaji huduma za kiuchumi na kijamii katika sekta mbalimbali lakini pamoja na mafanikio hayo, changamoto mbalimbali zilijitokeza.
Mfumo huu umeanzishwa ili kuweza kukabiliana na changamoto zilizopo katika Utumishi wa Umma.
Akifunga mkutano huo, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bwana HAB Mkwizu aliwapongeza washiriki kwa kushiriki kikakimilifu katika kutoa maoni yao ili kuweza kuboresha utekelezaji wa Mfumo huu
Bwana Mkwizu aliahidi kuwa michango ya washiriki itafanyiwa kazi katika kuboresha mfumo huu ili uweze kutekelezwa kwa mafanikio na kutimiza malengo ya kuanzishwa kwake yakiyemo kuboresha utendaji, utoaji huduma na kuongeza uwajibikaji ili kukidhi matarajio ya wateja wetu na wananchi kwa ujumla.
“Nawaomba kuwa mabalozi wa kutoa elimu ya Mfumo huu mara mtakaporejea kwenye shughuli zenu za kila siku” Bwana Mkwizu alisema.
Masuala mbalimbali yaliyojadiliwa katika mkutano huo ni pamoja na Chimbuko la Mfumo, Maana na faida, Mambo ya msingi yatakayofanikisha utekelezaji wa mfumo wa Mikataba ya Utendaji Kazi, Fomu ya Mkataba wa Utendaji Kazi na vipengele vyake, Vigezo vya upimaji utendaji kazi wa Taasisi, Watakaohusika na Mikataba ya Utendaji Kazi, Utaratibu wa kuingia Mikataba ya Utendaji Kazi.
Masuala mengine ni Utaratibu wa kutoa taarifa za Mikataba ya Utendaji Kazi, Utaratibu wa Kutathmini ya Mikataba ya Utendaji Kazi, Utaratibu wa kushindanisha taasisi za Umma na Taasisi zinazopendekezwa kuingia katika Mikataba ya Utendaji Kazi.
Mkutano huo ulihudhuriwa na Makatibu Wakuu Wastaafu, Makatibu Watendaji Wastaafu, Wasaidizi wa Katibu wa Baraza la Mawaziri, Makatibu Tawala wa Mikoa Wastaafu, Wakurugenzi Wasaidizi Wastaafu, Watendaji Wakuu Wastaafu wa Wakala za Serikali, Watendaji Wakuu wa Asasi Za Kiraia (AZAKI), Wanataaluma kutoka Vyuo vya Elimu ya Juu, Wawakilishi wa Sekta Binafsi na Washauri waelekezi Wanaojitegemea.
No comments:
Post a Comment