Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam limeanzisha
msako mkali wa kuwatafuta majambazi watano ambao jana tarehe 27/7/2014
saa 8.00 mchana walifika katika benki ya Stanbic Tawi la Kariakoo lililoko
mtaa wa Swahili.
Watatu kati yao waliingia ndani ya benki hiyo
wakiwa na mifuko mikubwa wakijifanya ni wateja waliopeleka fedha nyingi
katika benki hiyo. Watu hao watatu walipoingia ndani walianza
kulazimisha kuvuka wigo wa wateja wa kawaida na kutaka kuingia kwa nguvu
kwenda kupora fedha.
Stanbic Bank ina mitambo ya aina mbali mbali ikiwa
ni pamoja na ving’ora vya tahadhari. Ving’ora
hivyo vilianza kulia kwa sauti kubwa nje na ndani ya benk hiyo hali
iliyowatia kiwewe wahalifu hao. Waliamua kurudi nje kwa kasi ambapo
kulikuwa na gari aina ya Noah na pikipiki moja ambazo hazikusomeka namba
kwa haraka na wakatoweka baada ya kufyatua risasi hewani na kuwatisha
watu waliokuwa nje na ndani ya Benk.
Baada ya kuondoka majambazi
hao iligundulika kwamba mmojawao alichota kwa mkono kiasi cha fedha
ambazo mteja alizileta kwa madhumuni ya kuziweka katika Tawi hilo.
Baada ya kutoroka majambazi hao waliteIekeza mifuko mikubwa ambayo walitegemea
kubebea fedha watakazopora katika benk hiyo ambayo imehifadhiwa kama
kielelezo na ndani ya mifuko hiyo waliweka kokoto na uchafu mwingine
kwa madhumuni ya kuwadanganya walinzi na watumishi wa benk kwamba walikuwa
wamebeba fedha za kuweka benki.
Kutokana na tukio hili tunahimiza benki zote kuchukua
tahadhari za kiusalama ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba wanaingia
mkataba wa kulindwa na Jeshi la Polisi, kuweka vifaa mbali mbali vya
ulinzi vikiwemo ving’ora (alarms), CCTV Camera na mashine za kugundua
(metal detectors) mtu anapoingia na silaha au kitu kingine cha hatari
kama visu, mitarimbo n.k.
No comments:
Post a Comment