Friday, October 7, 2016

Kiwanda kikubwa cha mbolea kujengwa Mtwara, Eneo la hekta 400 latengwa


Na Greyson Mwase, Mtwara.

Serikali kwa kushirikiana na kampuni ya Helm kutoka Ujerumani inatarajia kujenga kiwanda kikubwa cha mbolea katika eneo la Msanga Mkuu mkoani Mtwara.

Hayo yalielezwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa katika nyakati tofauti katika ziara ya siku tatu mkoani Mtwara ya kutembelea maeneo ambayo gesi inazalishwa na kujiridhisha iwapo itatosha katika uendeshaji wa kiwanda kikubwa cha mbolea kinachotarajiwa kujengwa.

Profesa Ntalikwa alisema kuwa kutokana na ugunduzi wa gesi nyingi mkoani Mtwara wawekezaji wengi wameanza kuonesha nia ya kuwekeza katika mkoa huo hususan katika uanzishwaji wa viwanda vya mbolea na saruji.

Alisema kiwanda cha mbolea kinachotarajiwa kujengwa, kitahitaji gesi kiasi cha futi za ujazo trilioni 0.8 kwa kipindi cha miaka 20 na kusisitiza kuwa serikali imejipanga katika kuhakikisha kuwa gesi ya kutosha inazalishwa ili kuendana na mahitaji ya kiwanda hicho pamoja na matumizi mengine ya majumbani.

Akielezea uwezo wa kampuni zilizopo Mtwara katika uzalishaji wa gesi ya kutosha, Profesa Ntwalikwa alifafanua kuwa, kampuni ya Ndovu Resources Limited iliyopo katika eneo la Ntorya ipo katika programu ya kuchimba visima ambapo imeshachimba kisima kimoja ambacho kimeweza kutoa kiasi cha futi za ujazo trilioni 0.15

Aliongeza kuwa kampuni hiyo ina mpango wa kuchimba kisima cha pili ambacho kitakuwa na uwezo wa kuzalisha gesi kiasi cha futi za ujazo trilioni 0.9 na kisima cha tatu kitakachokuwa na uwezo wa kuzalisha gesi kiasi cha futi za ujazo trilioni 1.5 na kuongeza kuwa kisima cha pili kinatarajiwa kukamilika mapema Machi, 2017 na cha tatu mwezi Juni, 2017.

Aliongeza kuwa kampuni nyingine ya Maurel & Prom yenye visima vitano imesema kuwa ipo tayari wakati wowote kuchimba visima vya ziada vya kuzalisha gesi ili kuongeza wingi wa gesi itakayohitajika katika viwanda mbalimbali ambapo kwa sasa wanazalisha gesi nyingi hali inayopelekea nyingine kukosa soko.

Akielezea maandalizi ya ujenzi wa kiwanda hicho, Profesa Ntalikwa alisema kuwa Serikali imetenga eneo la Msanga Mkuu lililopo Mtwara lenye ukubwa wa hekta 400 kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda hicho.

Aliongeza kuwa eneo hili limeshalipiwa fidia pamoja na halmashauri ya Mtwara kuboresha miundombinu ya barabara kwa kuweka lami kutoka Mtwara Mjini hadi eneo la kiwanda tayari kwa kukabidhiwa kwa mwekezaji kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa (kulia) akisalimiana na Afisa Rasilimaliwatu kutoka Shirika la Umeme Nchini (TANESCO)- Tanga, Samia Suleman (kushoto) mara baada ya kuwasili kwenye ofisi zake mkoani Mtwara. Profesa Ntalikwa yupo katika ziara ya siku tatu katika mkoa wa Mtwara yenye lengo la kukagua shughuli za sekta za nishati na madini.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili katika kituo cha kuzalisha umeme cha Mtwara.
Kituo cha kuzalisha umeme mkoani Mtwara kama kinavyoonekana pichani.
Meneja wa kituo cha kuzalisha umeme cha Mtwara, Mhandisi Mkulungwa Chinumba (kulia) akitoa maelezo juu ya uendeshaji wa kituo hicho kwa Katibu Mkuu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa (kushoto).
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa (katikati mbele) pamoja na wataalam kutoka Shirika la Umeme Nchini (TANESCO), Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC) akiendelea na ziara katika kituo cha kuzalisha umeme cha Mtwara.
Meneja wa kituo cha kuzalisha umeme cha Mtwara, Mhandisi Mkulungwa Chinumba (kushoto) akielezea mitambo ya kuzalisha umeme inavyofanya kazi katika kituo hicho.
Msimamizi wa mradi wa ujenzi wa kituo cha kupooza umeme cha Mtwara, Mhandisi Amon Gamba (kushoto) akielezea maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa ( wa pili kushoto).
Kamishna Msaidizi wa Madini- Kanda ya Kusini, Mhandisi Benjamin Mchwampaka (kushoto) akiwasilisha taarifa ya maendeleo ya sekta ya madini katika kanda hivyo kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa (kulia) mara Profesa Ntalikwa alipofanya ziara katika kituo hicho.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa (kushoto) akisalimiana na Meneja Uendeshaji wa Mnazi Bay, David Chaudronnier (kulia) mara baada ya kuwasili katika kituo hicho.
Msimamizi wa shughuli za uzalishaji kutoka Mnazi Bay, Kilemo Nyomwa akielezea mikakati ya uzalishaji wa gesi ya kutosha katika kituo hicho ili kuendana na kasi ya ukuaji wa viwanda katika mkoa wa Mtwara.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa (mwenye suti nyeusi) pamoja na wageni wengine, akiendelea na ziara katika kituo cha Mnazi Bay mkoani Mtwara.

No comments:

Post a Comment