Tuesday, October 11, 2016

MAGAVANA WA BENKI YA DUNIA KUTOKA AFRIKA WAKUTANA WASHINGTON DC,WAHIMIZA USHIRIKISHWAJI


Benny Mwaipaja, MoFP-Washington DC, Marekani
MAWAZIRI wa Fedha na Magavana wa Benki Kuu kutoka nchi mbalimbali za kiafrika, wanachama wa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa-IMF, wamekutana Jijini Washington DC, Marekan,i na kuzitaka Taasisi hizo kuweka mipango inayoakisi na kutatua changamoto zinazolikabili bara hilo ikiwemo, uhalifu, umasikini, mizozo ya kivita na majanga yanayotokana na mabadiliko ya tabia nchi

Aidha, Viongozi hao wamezitaka taasisi hizo kuweka uwiano wa uwakilishi wa uongozi wa juu ili kuhakikisha kuwa maslahi mapana ya nchi hizo yanalindwa na maendeleo endelevu yanafikiwa kwa haraka.

Akizungumza kwenye moja ya mikutano hiyo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, ambaye kiutaratibu ni mmoja wa Magavana wa Benki ya Dunia na IMF, amesema kuwa mashirika hayo ya fedha ya kimataifa yanamchango mkubwa kwa maendeleo ya nchi za kiafrika ikiwemo Tanzania.

Hata hivyo amesema kuwa mdororo wa uchumi duniani, ambao unaonesha kuwa viwango vya ukuaji wa uchumi vilivyokadiriwa kufikiwa kwa asilimia 3, havitafikiwa ambapo takwimu zinaonesha kuwa ukuaji wake hivi sasa ni asilimia 1.5 tu, unaashiria namna nchi wanachama zinatakiwa kujipanga kuhakikisha kuwa uchumi unapanda.

Dkt. Mpango amesema kuwa uchumi wa Tanzania unakua kwa kasi kwa wastani wa asilimia 7 kwa mwaka lakini changamoto kubwa iliyopo ni kuhakikisha kuwa uchumi huo unaonekana katika maisha ya kawaida ya wananchi wake

“Kila mara utasikia malalamiko ya wananchi kwamba uchumi wetu unakua kwa namba tu hawaoni ni kwa kiasi gani uchumi huo wanauona katika maisha yao ya kawaida kwa hiyo ili uchumi uhesabike kuwa unakua ni lazima uwe jumuishi na ushirikishe watu wengi” alisema Dkt. Mpango

Amesema kuwa hali hiyo itawezekana ikiwa sekta zinazochangia maendeleo kwa kasi zaidi kama kilimo, uvuvi, biashara ya miamala ya simu, miundombinu na viwanda, zitaimarishwa ili kukuza ajira na kuongeza kipato cha wananchi.

“Tunataka kilimo kiwe cha kisasa na cha kibiashara kwa kutumia zana na pembejeo bora za kilimo, uongezaji wa thamani ya mazao na kuwa na masoko ya uhakika ili kukuza ajira nyingi hususani kwa vijana” Aliongeza Dkt. Mpango
Amebainisha kuwa Tanzania itaendeleza uhusiano mzuri uliopo kati yake na Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani-IMF na kuwataka watanzania waelewe kuwa mikopo na ruzuku zinazotafutwa na serikali yao ni kwaajili ya kuwaletea maendeleo kwa kuwekeza kwenye miradi yenye tija.

Wajumbe wa Tanzania waliohudhuria mkutano wa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani-IMF, wakimsikiliza kwa makini Rais wa Benki ya Dunia Dkt. Jim Yong Kim (hayupo pichani) wakati Mawaziri wa Fedha na makatibu wakuu (Magavana) kutoka nchi wanachama wa Taasisi hizo kutoka Bara la Afrika, walipokutana kama kamati, Jijini Washington DC, Marekani.
 Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango (kushoto) na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dotto James, wakifuatilia kwa makini mkutano wa Magavana wa Benki ya Dunia kutoka Barani Afrika uliohudhuriwa na Rais wa Benki ya Dunia Dkt. Jim Yong Kim, Jijini Washington DC, Marekani.
 Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango akiwa na Katibu Mkuu Bw. Dotto James (kulia) wakiandika pointi muhimu wakati Rais wa Benki ya Dunia, Dkt. Jim Yong Kim, alipowahutubia Mawaziri wa Fedha na Makatibu wakuu (Magavana) kutoka nchi za Kiafrika wanaoshiriki Mkutano wa Mwaka wa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani-IMF, Jijini Washington DC-Marekani.


Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango akiwa na Waziri wa Fedha wa Swaziland kushoto kwake walipokuwa kwenye mkutano na  Mkurugenzi Mtendaji Bi. Christine Lagarde Jijini washington DC- Marekani.
 Wataalamu wa Fedha na Uchumi Kutoka Wizara ya Fedha na Mipango na kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) wakisikiliza kwa makini mkutano wa Shirika la Fedha Duniani-IMF, ukisimamiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Bi. Christine Lagarde (Hayupo Pichani) ambaye  aliwambukusha wajumbe wanaoziwakilisha nchi zao kuwa umasikini bado ni changamoto kubwa na  unasababisha vikwanzo vingi katika kukuza maendeleo na ustawi wa nchi wanachama, Jijini Washington DC-Marekani.
 Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango akiwa na Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, wakibadilishana mawazo kabla ya kukutana na uongozi wa Juu wa Shirika la Fedha Duniani-IMF, Kanda ya Afrika, Jijini Washington DC nchini Marekani.
 Waziri wa Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango akisalimiana na Gavana wa Benki Kuu ya Kenya Bw. Patrick Ngugi Njoroge alipokutana nae kwenye mikutano ya Benki ya Dunia Jijini Washington DC- Marekani.
 Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango, akifafanua jambo alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Fedha Duniani-IMF, Kanda ya Afrika, Bi. Chileshe Mpundu Kapwepwe Hayupo pichani), Jijini Washington DC-Marekani. Kushoto kwake ni Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Prof. Benno Ndulu akifuatiwa na Naibu Gavana wa Benki hiyo Dkt. Natu Mwamba.
 Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Fedha Duniani –IMF, Kanda ya Afrika Kundi la Kwanza,  Chileshe Mpundu Kapwepwe (katikati), akisisitiza jambo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Fedha na Mipango, alipokutana na Ujumbe huo Ofisini kwake Jijini Washington DC, Marekani.
 Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Prof. Benno Ndulu (aliyenyoosha mkono) akielezea jambo wakati Ujumbe wa Tanzania Ukiongozwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, kulia kwake, walipokutana na kufanya mazungumzo na  Mkurugenzi Mtendaji wa IMF Africa Group I Bw. Abebe Aemro Selassie (Hayupo pichani) ambapo Gavana  alieleza kuhusu uchumi wa sasa wa Tanzania pamoja na Hali ya uchumi unavyokua kwa kiasi cha kuridhisha, Jijini Washington Marekani.
 Makamu wa Rais wa Shirika la Maendeleo la Japan-JICA, Hiroshi (Hiro) Kato, akimwonesha Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, Kitabu Chenye maelezo mbalimbali ya miradi inayotekelezwa nchini Tanzania kwa ufadhili wa shirika hilo, ambapo Japani imeahidi kuendelea kuwekeza kiasi kikubwa cha fedha kuendeleza miundombinu ya barabara na sekta ya kilimo cha umwagiliaji.
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango, akiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Dotto James (kushoto) wakimsikiliza kwa makini  Makamu wa Rais wa Shirika la Maendeleo la Japan-JICA, Hiroshi (Hiro) Kato, wakati Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Fedha na Mipango ulipokutana na Mkurugenzi huyo ambaye ameahidi kuwa Japan itaendelea kushirikiana na Tanzania katika Nyanja mbalimbali za kiuchumi na kijamii, Jijini Washington DC, Marekani.
(Picha zote na Wizara ya Fedha na Mipango)

No comments:

Post a Comment