Mkurugenzi Mkazi wa
Shirika la Plan International, Jorgen Haldorsen akiongea na waandishi wa habari
leo Jijini Dar es Salaam (hawapo pichani) juu ya maadhimisho ya siku ya
Msichana Duniani itakayoadhimishwa Octoba 11 mwaka huu katika mikoa ambayo shirika
hilo linafanya kazi.(Picha zote na Jacquiline Mrisho - Maelezo)
Msichana atakayekaimu
nafasi ya Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Plan International, Catherine Kapilima
akiongea na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam (hawapo pichani) namna
alivyoipokea na atakavyoitumia nafasi hiyo ikiwa ni moja ya kuadhimisha siku ya
Msichana Duniani Octoba 11 mwaka huu katika Mikoa ambayo shirika hilo linafanya
kazi.
Na Jacquiline Mrisho - Maelezo
SHIRIKA la Plan International limejipanga kuadhimisha Siku ya Msichana
Duniani kwa kuwakabidhi wasichana madaraka katika ofisi zao ili waweze
kuonyesha uwezo wao wa kufanya maamuzi katika masuala mbalimbali.
Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika
hilo, Jorgen Haldorsen alipokuwa akiongea na waandishi wa habari juu ya
maadhimisho ya siku hiyo yatakayofanyika Octoba 11 mwaka huu katika Mikoa
ambayo shirika hilo linafanya kazi.
Haldorsen amesema kuwa Shirika hilo litaungana na
mataifa mengine katika kusimamia usawa na kumpa msichana nafasi ya kujifunza,
kuongoza na kutoa maamuzi yaliyo bora ili kuwapa fursa sawa bila kujali jinsia.
“Kwa kuelekea kilele cha Siku ya Msichana Duniani,
Ofisi zote za Shirika letu pamoja na wadau wetu wakiwemo ubalozi wa Kanada
tumeamua kuadhimisha siku hii kwa kuwakaimisha uongozi baadhi ya wasichana
hivyo, tunatoa rai kwa mamlaka zingine kuwaachia wasichana nafasi ili waone
uwezo wao wakiwa kwenye mamlaka mbalimbali”, alisema Haldorsen.
Mkurugenzi huyo ameyataja matukio mengine ambayo
yatafanyika katika maadhimisho hayo yakiwemo ya kuzindua miradi ya kuzuia ndoa
za utotoni katika Mikoa ya Rukwa na Morogoro pamoja na kufanya majadiliano ya
moja kwa moja kati ya Mke wa Rais wa Amerika, Mitchel Obama na wasichana 25 wa
shirika la plan International kutoka katika nchi 3 za Tanzania, Peru na
Cambodia.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Ulinzi wa
Watoto, Jane Mrema amesema kuwa wasichana wamekuwa wakipambana na vikwazo vingi
vinavyowazuia kupata fursa mbalimbali katika jamii hivyo nguvu ya ziada
inatakiwa katika kuhakikisha mawazo hayo potofu yanakoma.
“Tukijitahidi kuondoa vikwazo vinavyowakabili
wasichana na kuwapa nafasi wanaweza kuleta mabadiliko makubwa, kinachotakiwa ni
kuwaamini na kuwapa fursa sawa na wengine”, alisema Mrema.
Naye msichana atakayekaimu nafasi ya Mkurugenzi
Mkazi wa Shirika hilo, Catherine Kapilima amesema kuwa kitendo cha kuachiwa
madaraka hayo kitamjengea uwezo wa kufanya kazi kwa vitendo pamoja na
kuwashawishi wasichana wenzie kuamini kuwa kila kitu kinawezekana bila kujali
jinsia.
Siku ya Msichana Duniani inaadhimishwa kwa lengo la
kuonesha vizuizi mbalimbali kwa maendeleo ya wasichana na jinsi ya kuvitatua,
huadhimishwa Octoba 11 kila mwaka. Hii ni mara ya tano kuadhimishwa.
No comments:
Post a Comment