Mkuu wa Mkoa wa
Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum Kijuu akiongea na waandishi wa habari leo
mjini Bukoba alipokuwa akitoa taarifa ya hatua zilizochukuliwa na Serikali
katika kurejesha hali baada ya maafa ya tetemeko la ardhi lililoukumba mkoa
huo.
Na
Eleuteri Mangi, MAELEZO, Bukoba
SERIKALI inaendelea na
juhudi za kurejesha miundombinu iliyoharibiwa na tetemeko ili kuhakikisha
wananchi wanapata huduma za msingi za kijamii ikiwemo shule za msingi,
sekondari, barabara na vituo vya afya.
Akitoa taarifa ya urejeshwaji wa hali baada ya
tetemeko la ardhi la Septemba 10 mwaka huu kwa waandishi wa habari leo mjini
Bukoba, Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum Kijuu amesema
kuwa Kamati ya Maafa tayari imetoa vifaa vya ujenzi ili kuhakikisha hali ya
miundombinu inarejea na kuwahudumia wananchi.
Aidha, Watanzania walioguswa na janga tetemeko
wametakiwa kuendelea kuwachangia Wanakagera ili kuwarejeshea maisha yao ya
kawaida.
Katika kurejesha hali, tayari vifaa mbalimbali
vimetolewa ikiwemo mabati 4,496 ya geji 30, mbao 98, misumari ya bati kilo 110
na misumari mchanganyiko kilo 558 ili kurekebisha na kujenga miundombinu
kulingana na uharibifu uliotokea.
“Tumetoa kipaumbele katika kurejesha miundombinu ya
huduma za kijamii kwenye halmashauri za wilaya zilizoathirika ili kamati za
maafa za wilaya ziweze kukarabati miundombinu ya kutolea huduma za kijamii kama
shule za sekondari na msingi, vituo vya kutolea huduma za afya vilivyoharibiwa
na tetemeko ili huduma hizo muhimu ziweze kurejea mara moja na kutoa huduma kwa
wananchi” amesema Meja Jenerali Mstaafu Kijuu.
Katika kuhakikisha wananchi wananchi wanapata mahitaji
muhimu, Meja Jenerali Mstaafu Kijuu amesema kuwa Kamati ya Maafa imeendelea
kugawa mahitaji kwa wananchi walioathirika na tetemeko kadri inavyoyapokea
kutoka kwa wadau mbalimbali.
Mahitaji yaliyogawiwa kwa wananchi ni pamoja na
unga wa sembe kilo 4,350, sukari mifuko 1,014, mchele kilo 103,400, maharagwe
kilo 5,753, mahindi kilo 50,000 majani ya chai tani 3, maji katoni 850, mafuta
ya kula lita 249, sabuni katoni 26, mashuka 90, mablanketi ya watu wazima na
watoto 2,680, vyandarua 1,274, sare za wananfunzi 570, magodoro 694, mahema 127
na matrubali 5,760.
Kuhusu watu waliopata majeraha, Meja Jenerali
Mstaafu Kijuu amesema wamebakia majeruhi sita, ambapo katika Hospitali ya Rufaa
ya Mkoa wa Kagera wamebakia majeruhi wawili, Hospitali ya Mugana majeruhi
mmoja, na Hospitali ya Rufaa ya Bugando majeruhi watatu na majeruhi wote
wanaendelea kupata huduma za matibabu na hali zao zinaendelea vizuri.
Mkuu huyo wa mkoa amesema kuwa awali baada ya
tetemeko la ardhi kulikuwa na majeruhi 440 ambapo tayari majeruhi 434
wametibiwa na kuruhusiwa katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa na vituo mbalimbali
vya afya kwenye mkoa huo.
Kwa upande wa misaada iliyopokelewa na kamati ya
maafa, Meja Jenerali Mstaafu Kijuu amesema kuwa kamati ya maafa imepokea
misaada ya mahitaji mbalimbali yenye thamani ya zaidi ya shilingi 1,094,478,950
ambayo imeendelea kugawiwa kwa wananchi kadiri ilivyokuwa inaletwa na wananchi
na wadau wengine.
Aidha, Mkuu huyo wa mkoa amewashukuru wananchi
pamoja na wadau mbalimbali ambao wameendelea kutuchangia kwa fedha taslimu na
hundi katika akaunti maafa inayojulikana kwa jina la “Kamati Maafa Kagera
0152225617300 CRDB BUKOBA.” ambapo hadi Oktoba 03 mwaka huu zimepokelewa jumla
ya shilingi bilioni 3,481,069,473.43 na kuwaasa wananchi wasikatishwe tamaa
kuchangia kutokana na tukio la hivi karibuni la kufunguliwa akaunti nyingine
ambayo siyo halali na kuwahakikishia kuwa suala hilo limedhibitiwa na
hakutakuwepo na udokozi wala matumizi mabaya ya fedha zinazochangwa wala vifaa
vinavyochangiwa.
Wakati huo huo, Mkuu wa mkoa amesema kuwa mitandao
ya simu ya M-pesa 0768196669, Tigo Pesa 0718069616, na Airtel Money 0682950009
hadi kufikia Oktoba 03 2016 zimepokelewa jumla ya shilingi milioni 4,750,927.
Zaidi ya hayo Meja Jenerali Mstaafu Kijuu aesema kuwa
Kamati ya Maafa inaendelea kuwahudumia wananchi walioathirika na tetemeko
mkoani Kagera wanaotoa malalamiko, ushauri, maoni na taarifa mbalimbali kutoka
kwa wananchi waloathirika katika tetemeko.
Malalamiko yanaweza kuletwa kwa kamati kupitia za
namba za simu zilizotolewa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa 0621155777na Ofisi ya
Waziri Mkuu 0621155888 na kujibiwa au kuelekezwa wanachotakiwa kufanya ili
kupata huduma ya misaada.
Kupitia namba hizo za simu kamati imepokea jumla ya
simu 82 kutoka maeneo mbalimbali na wananchi kuhudumiwa na kupata misaada
waliotarajia na kuwataka wananchi kuendelea kutumia simu hizo ili kutatuliwa
kero zao hasa kuhusu misaada.
Mkuu wa mkoa alitumia nafasi hiyo kuwaomba wananchi
wote ambao waliathirika na tetemeko la ardhi na nyumba zao kuharibiwa
wahakikishe wanaanza kurejesha miundombinu ya nyumba zao kama baadhi yao
walivyokwisha kufanya wasisubiri kujengewa na kuongeza kuwa Serikali inajenga
miundombinu iliyoharibiwa ya kutolea huduma za jamii.
No comments:
Post a Comment