Naibu Waziri Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Anastazia Wambura (Kulia)
akizungumza na wadau wa Sekta ya Utamaduni (hawapo pichani) walioshiriki katika
kikao cha Wadau tuzungumze kujadili namna ya kukemea vitendo vya mmomonyoko wa
maadili nchini leo Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Maendeleo
ya Utamaduni Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bibi. Lily Beleko.(Picha zote na Genofeva Matemu - WHUSM)
Kaimu
Mkurugenzi Maendeleo ya Utamaduni Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo, Bibi. Lily Beleko akifafanua jambo wakati wa kikao na wadau wa
sekta ya Utamaduni kujadili namna ya kukemea vitendo vya mmomonyoko wa
maadili nchini leo Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi
wa Mawasiliano, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Bw. Bernard
James akichangia mada wakati wa kikao na wadau wa sekta ya Utamaduni
kujadili namna ya kukemea vitendo vya mmomonyoko wa maadili nchini leo
Jijini Dar es Salaam.
Katibu
Mtendaji Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Bw. Godfrey Mngereza
akijibu hoja za wadau wakati wa kikao na wadau wa sekta ya Utamaduni
kujadili namna ya kukemea vitendo vya mmomonyoko wa maadili nchini leo
Jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Anastazia Wambura (Katikati waliokaa) katika
picha ya pamoja na wadau wa sekta ya utamaduni walioshikiki kikao cha wadau
kujadili namna ya kukemea vitendo vya mmomonyoko wa maadili nchini leo Jijini
Dar es Salaam. Kulia waliokaa ni Kaimu Mkurugenzi Maendeleo ya Sanaa Wizara ya
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bibi. Leah Kihimbi.
NA Shamimu Nyaki - WHUSM.
WIZARA ya Habari
Utamaduni Sanaa na Michezo imewataka wadau wa Sekta ya Utamaduni na jamii kwa
ujumla kusaidiana katika kukemea vitendo vya mmomonyoko wa maadili ambao
umekuwa kikwazo katika kuulinda Utamaduni wa mtanzania.
Hayo yamesemwa leo
Jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe.
Anastazia Wambura alipokuwa anazungumza na Wadau wa Sekta ya Utamaduni katika
muendelezo wa kikao cha “WADAU TUZUNGUMZE” ambapo amesema kuwa suala la
mmomonyoko wa Maadili linaanzia ngazi ya familia hivyo linapaswa kukemea kwa
nguvu zote.
“Suala la mmomonyoko
wa maadili ni mtambuka na huanzia ndani ya familia na huendelea kujigawa
kulingana na umri, rika, na hatimaye jamii kwa ujumla hivyo ni budi watu wote
kulikemea ili tuwe na jamii yenye maadili mazuri”, Alisema Mhe. Anastazia.
Aidha Mhe. Anastazia
ameeleza kuwa Wizara yake itaendelea kuchukua hatua zinazostahili ikiwemo kutoa
elimu kwa kuwatumia maafisa Utamaduni wa kila Mkoa ili kuhakikisha suala la mmomonyoko wa
maadili linashughulikiwa kwa kina kwa kuwa Wizara ndio yenye dhamana ya kuratibu
na kusimamia maadili ya jamii.
Kwa upande wake Kaimu
Mkurugenzi Maendeleo ya Utamaduni kutoka Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na
Michezo Bibi. Lily Beleko amesema kuwa Idara yake inafanya juhudi kubwa za
uhamasishaji wa jamii nzima kwa kushughulikia mipango madhubuti ya kuanzisha
mifumo ya kudhibiti mmomonyoko wa maadili hapa nchini.
“Suala hili la
maadili linahusu jamii nzima hivyo kuna umuhimu mkubwa wa kuhusisha na kushirikisha
jamii yote kuchangia katika mjadala wa kupata njia sahihi za kupambana na
mmomonyoko wa maadili ya jamii yetu.”Alisema Bibi Lily.
Naye Mkurugenzi wa
mawasiliano Baraza la Maaskofu Tanzania Bw. Bernad James ameishauri Serikali
kuendelea kukemea vitendo vyote vinavyosababisha maadili kumomonyoka hasa
udhibiti wa maudhui katika sehemu tofauti ikiwemo Muziki na Filamu ambayo ndio maeneo
yanayohusisha watanzania wengi.
Kikao cha “WADAU TUZUNGUMZE” kilichoanzishwa na Mhe. Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Nape Nnauye kwa lengo la kukutana na wadau na kujadili changamoto zilizopo katika Wizara yake na namna ya kuzitatua leo kimeshirikisha Wadau wa Sekta ya Utamaduni ambapo mada ya leo ilikuwa “Je Maadili rasmi ya Mtanzania yapo au hayapo”.
No comments:
Post a Comment