Maafisa wa usalama wa Somalia wamewaokoa mabaharia wanane ambao walikuwa wametekwa nyara na maharamia.
Maharamia hao waliteka nyara meli ya kihindi ya mizigo mwezi uliopita na kuwashika watu wote kumi waliokuwa wameliabiri huku wakiitisha fidia.
Maafisa wa usalama waliokoa watu wawili pamoja na meli hiyo Jumatatu, huku maharamia wakitoroka na wale wanane waliosalia, ambao sasa wako huru.
Meli hiyo ya Al Kausar ni ya tatu kutekwa nyara chini ya mwezi mmoja.
"Maafisa wa usalama waliwashinda nguvu maharamia na wakalazimika kutoroka lakini watatu kati yao walikamatwa," Abdi Rashid Mohamed Ahmed ambaye ni naibu kamanda wa kikosi cha bahari cha Galmudug alieleza AFP.
Ahmed alisema kuwa waliookolewa wako sawa kiafya . Hakutaja uraia wao.
Siku ya Jumapili, vikosi vya navy kutoka India, Pakistani na China viliwaokoa wafanyikazi wa meli ya Tuvalu ambayo ilikuwa imeabiriwa na maharimia.
Uharamia katika bahari ya maeneo ya Somalia na Yemen uliongezeka mwaka wa 2011, ambapo kulikuwa na visa zaidi ya 200.
Lakini visa hivi vimepungua kwa asilimia kubwa miaka michache iliyopita, kwani kumekuwa na vikosi vya kimataifa ambavyo vimekuwa vikipiga doria majini na kusaidia wavuvi.
Hata hivyo maswala yaliyowafanya wavuvi wengi wa kisomali kuingilia uharamia miaka mingi iliyopita, bado ipo kulingana na mwanahabari wa BBC Frank Gardner.
Kwa sasa kuna ukame mkali sana Somalia huku mamia ya maelfu ya watu wakikumbwa na baa la njaa. Umasikini umekithiri huku nafasi za kazi kwa vijana zikiwa kidogo sana.
No comments:
Post a Comment