Tuesday, May 16, 2017

PROF. MUHONGO AKATAA KUSAINI LESENI


 Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (katikati), akizungumza na wawekezaji mbalimbali katika sekta ya madini, waliowasilisha maombi ya kupatiwa leseni kwa ajili ya kuwekeza katika sekta husika.
 Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, akisaini leseni mbalimbali za wawekezaji katika sekta ya madini.
 Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (katikati) akikabidhi leseni ya uchimbaji wa kati wa madini ya ‘Marble’ iliyohamishwa kutoka kwa Salim Mohamed Salum (wa pili kutoka kushoto) kwenda kwa wawekezaji wa kampuni ya S & T Marble and Mining Limited (kulia). Wa kwanza kushoto ni Kamishna wa Madini Tanzania, Mhandisi Benjamin Mchwampaka.
 Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto), akimkabidhi leseni ya uchimbaji wa kati wa madini ya ‘Limestone’, mwakilishi wa Kampuni ya Saruji ya Tanzania Portland Cement, Richard Magoda (katikati). Kulia ni Kamishna wa Madini Tanzania, Mhandisi Benjamin Mchwampaka.
Mwekezaji, Mbarouk Saleh Mbarouk (katikati), akionesha leseni yake ya uchimbaji wa kati wa madini ya ‘Marble’ katika eneo la Mkuyuni Matombo wilayani Morogoro, baada ya kusainiwa na kukabidhiwa na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto). Kulia ni Kamishna wa Madini Tanzania, Mhandisi Benjamin Mchwampaka.

Na Veronica Simba – Dodoma.

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amekataa kusaini ombi la uhamishaji wa leseni ya uchimbaji wa kati wa madini ya Shaba Namba ML 571/2017 kutoka kwa mtanzania David Stanley Kayongoya kwenda Kampuni ya Mechanized Minerals Supreme Mining Company Limited inayomilikiwa na raia kutoka China.

Profesa Muhongo alikataa kusaini leseni hiyo yenye ukubwa wa kilomita za mraba 0.43 katika eneo la Fufu wilayani Chwamwino mkoani Dodoma, baada ya kubaini kuwa mtanzania anayetaka kuhamishia leseni hiyo kwa Raia wa China, hatanufaika kwa kiwango kinachoridhisha.

Akizungumza na wawekezaji mbalimbali wa sekta husika, waliofika Makao Makuu ya Wizara mjini Dodoma, kwa ajili ya kusainiwa leseni zao za uwekezaji, jana (Mei 15), Profesa Muhongo alisisitiza kuwa ni lazima wawekezaji katika sekta husika wazingatie suala la maslahi ya wananchi na Taifa kwa ujumla, wakati wanapotekeleza kazi zao za uwekezaji.

Waziri Muhongo alimwagiza mwekezaji huyo raia wa China kujadiliana kwa mara nyingine na mtanzania mwenye eneo husika (David), ili kuhakikisha ananufaika ipasavyo na uwekezaji huo.

“Ili niweze kusaini leseni hii, rudini mezani, mzungumze na kukubaliana ili David aweze kunufaika. Hatuwezi kukubali kuona watanzania wakidhulumiwa namna hii,” alisisitiza Waziri.

Awali, ilielezwa kuwa mkataba wa mauziano ya leseni husika unaonesha kuwa David amepokea kiasi cha shilingi milioni 30 za kitanzania. Waziri alipotaka kujua endapo kuna manufaa mengine ambayo David atapata, alielezwa kuwa ataajiriwa katika kampuni hiyo kama kibarua, ndipo Waziri akakataa kusaini leseni husika.

Ili kuhakikisha suala hilo linatekelezwa ipasavyo, Profesa Muhongo alimwagiza Kamishna wa Madini nchini, Mhandisi Benjamin Mchwampaka, kujiridhisha kwa kupokea ahadi za maandishi kutoka kwa mwekezaji yeyote anayeomba leseni, namna ambavyo atazingatia maslahi ya nchi, kabla ya kumpatia leseni anayoomba.

Kwa upande wake, Kamishna Mchwampaka, pamoja na kuahidi kuzingatia na kutekeleza agizo la Waziri; aliwataka wawekezaji hao kuzingatia kanuni na miongozo mbalimbali ya uwekezaji kama inavyobainishwa katika Sheria ya Madini ya mwaka 2010.

Wawekezaji wengine waliokidhi vigezo na Leseni zao kusainiwa ni pamoja na ya Salim Mohamed Salum inayohusisha uhamishaji wa leseni tatu za uchimbaji wa kati wa madini ya ‘Marble’ namba ML 566/2016 iliyoko Mumbwi wilaya ya Handeni, ML 567/2016 iliyoko Ulanga Morogoro na ML 568/2016 iliyoko Kwenkambala – Handeni mkoani Tanga kwenda kampuni ya S & T Marble and Mining Limited.

Nyingine ni leseni namba ML 577/2017 ya Mbarouk Saleh Mbarouk, inayohusisha uchimbaji wa kati wa madini ya ‘Marble’ kwa kipindi cha miaka 10 katika eneo la Mkuyuni Matombo wilayani Morogoro.

Vilevile, leseni nyingine iliyosainiwa ni ya Kampuni ya Tanzania Portland Cement, namba ML 575/2017 inayohusisha uchimbaji wa kati wa madini ya ‘Limestone’ kwa kipindi cha miaka 10 katika eneo la Wazo Hill Wilaya ya Kinondoni. Ilielezwa kuwa, maombi ya leseni hiyo yanatokana na leseni ya utafiti wa madini namba PL 9416/2013.

No comments:

Post a Comment