Dereva na kondakta
Wake Walivyombaka kwa Zamu Ndani ya Basi Lao. Dereva na kondakta wa daladala
zinazofanya safari ndani ya Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro,
Soweto–Mbuyuni wanatuhumiwa kumbaka abiria wao kwa zamu na kumuumiza sehemu za
siri. Tukio hilo lililotokea Juni 12 saa moja jioni maeneo ya Veta katika
uchochoro uliopo karibu na shule ya Northen Highland iliyo umbali wa mita 400
kutoka barabara ya lami. Akielezea tukio hilo, binti huyo mwenye umri wa miaka
20 alisema alitumwa na bosi wake kwenda kununua mahitaji ya nyumbani Soko la
Mbuyuni na kumuelekeza kuwa akimaliza apande basi la Soweto sokoni hapo na
ashukie mwisho ambako angechukua bodaboda ya kumfikisha nyumbani.
“Nilipomuuliza konda akaniambia ndiyo na nikampigia bodaboda ambaye nilipewa namba
na bosi wangu ili ampe maelekezo huyo kondakta sehemu ambayo watanishusha ili
yeye anichukue hapo na wakazungumza na baadaye akanirejeshea simu yangu,”
alisema msichana huyo. Alisema baada ya hapo safari ya kutoka Mbuyuni kwenda
Soweto ilianza. “Kwa kuwa nilikuwa mgeni, sikuelewa hata kituo kipi cha
kushukia. Niliendelea kukaa hadi nilipoona watu wote wameisha kwenye (Toyota)
Hiace, ndipo nikamuuliza konda kwa nini hanishushi akasema bado sijafika,”
alisema. Anasema alishangaa kuona dereva anaenda kuegesha gari uchochoroni na
aliposimama, kondakta akashuka, akidai anaenda kujisaidia. “Aliporudi kwanye
gari alifunga mlango na wakazima taa na kuanza kuniambia kuwa wamenipenda kama
ninataka kuwa hai nikubaliane na wanachokitaka na nikikataa wataniua,” alisema
binti huyo. Alisema baadaye dereva alitoka kwenye usukani na kumfuata alipokaa
na kuanza kumpapasa. Alisema alipoona hivyo alijaribu kutoka nje kupitia
dirishani, lakini walimvuta ndani huku wakimfunga mdomo asipige kelele na
kumtishia kumuua. “Nilikubali yaishe na nikatulia. Akaanza dereva huku kondakta
akinishika mikono na baada ya kumaliza alichofanya, konda naye akaja akafanya
hivyohivyo. Nilisikia maumivu, lakini nilishindwa kupiga kelele kwa kuwa
walinitisha kuwa wangeniua,” alisema dada huyo. “Walipomaliza kufanya ukatili
huo, konda alimwambia dereva kuwa waniue kwa kuwa nimeshawatambua, lakini
dereva akasema hakuna haja.” Alisema katika mabishano hayo alijikaza na
kuwaambia kuwa yeye ni mgeni na hajui popote kwa hiyo hatamwambia mtu kwa kuwa
hilo ni tukio la aibu. “Walikubaliana na mimi na wakaniambia kuwa ni kweli
kubakwa ni kitendo cha aibu kwa hiyo nikimwambia mtu nitatengwa na jamii.
Nikawaomba wanisaidie sehemu ya kupata msaada niweze kufika nyumbani,” alisema.
Alisema baadaye aliwaomba aende kuchukua kiatu chake kilichokuwa kimedondoka
dirishani wakati akitaka kuruka, na walipomruhusu akatumia nafasi hiyo kusoma
namba za gari. Mlezi wake, Abdi Massawe alisema baada ya kufika nyumbani akiwa
na bodaboda, binti huyo alimweleza tukio hilo na akatoa taarifa polisi ambako
alipewa fomu ya matibabu aliyoitumia Hospitali ya Mawenzi, ambako vipimo
vilithibitisha kuwa alibakwa. “Huyu binti ni mgeni kutoka mkoani Singida. Hapa
Moshi ana mwezi mmoja tu,” alisema Masssawe. Massawe alisema baada ya hapo alianza
kusaka daladala hilo kwa kutumia namba alizopewa na binti huyo na kufanikiwa
kuikuta maeneo ya Soweto. Baadaye aliwapigia simu polisi ambao walifika na
kushusha abiria waliokuwamo na kuipeleka kituoni. Alisema wakati dereva
akiendelea na mahojiano kondakta alitoroka. Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Kilimanjaro, Koka Moita alisema derava wa gari hilo aliyemtaja kuwa ni Salimu
Abdalla (30) anashikiliwa na polisi ambao wanaendelea kumtafuta kondakta ambaye
alitoroka akiwa katika kituo cha polisi. Kwa sasa binti huyo anatibiwa
Hospitali ya Mawenzi.
No comments:
Post a Comment