Kuelekeza waumini kula nyasi, kuwapulizia dawa za kuua wadudu machoni waumini kwa ahadi ya kupata utajiri, kupata uponyaji na kuuona ufalme wa Mungu ni miongoni mwa yale ambayo wamekuwa wakihubiri wale wanaojiita manabii ama watumishi wa Mungu barani Afrika.
Katika tukio la hivi karibuni nchini Tanzania Jeshi la polisi nchini humo linamshikilia mtu mmoja anayefahamika kwa jina la Onsemo Machibya maarufu kwa jina alilojipa la Nabii Tito.
Mhubiri huyo anadaiwa kusambaza dini yake kupitia vipeperushi na picha za video, huku maudhui ya imani hiyo yakidaiwa kukinzana na maadili ya Kitanzania.
Jeshi la Polisi katika taarifa yake kwa vyombo vya habari lilisema mwanamume huyo ana matatizo ya akili na bado linaendelea kumshikilia.
Tito alijizolea umaarufu mitandaoni siku za hivi karibuni baada ya kusambaa kwa video zake kadhaa zikimuonyesha yeye na walioelezwa kuwa ni waumini wake wakinywa pombe wakati wa ibada yao lakini pia kucheza nyimbo mbalimbali hasa kwa kunengua viuno.
- Mhubiri awapa waumini dawa ya kuua panya Afrika Kusini
- "Kasisi" aliyemuua albino ashtakiwa Afrika Kusini
- Kasisi aliyewalisha watu nyoka Afrika Kusini, afika Nigeria
Kwenye moja ya video hizo, anaonekana kumbusu mdomoni aliyedaiwa kuwa mkewe pamoja na mwanamke mwingine anayedaiwa kuwa kijakazi wake.
Nabii Tito kwenye video hiyo anasema maandiko yameruhusu mwanaume kufanya zinaa na kijakazi wake.
Uhuru wa kuabudu una mipaka?
Padri Leons Maziku, ambaye ni mtaalamu wa Saikolojia na Mhadhiri katika chuo kikuu cha Mtakatifu Augustino anasema kwa mujibu wa tamko la umoja wa maifa la mwaka 1948 kuna uhuru wa kuabudu lakini uhuru huo umewekewa mipaka kisheria.
Padri Maziku anasema uwepo wa manabii hawa kunawaondolea heshima na hadhi viongozi wa dini lakini pia watu hawa wanaojiiita manabiii wanawatesa watu kisaikolojia hasa pale wanapobaini kuwa waliyemfuata ni nabii wa uongo
Licha ya kupingwa na baadhi ya watu, wapo wale wanaoamini kuwa kila mtu ana uhuru wa kuabudu anachokitaka.
Hivi karibuni nchini Afrika ya Kusini nako serikali ya nchi hiyo ilimpiga marufuku kiongozi wa kidini ambaye alikuwa na tuhuma na zenye kuendana na hizo.
No comments:
Post a Comment