Sunday, May 20, 2012

MTOTO WA MIAKA SITA ABAKWA

MKAZI wa Kijiji cha Emarti Kata ya Songambele Wilaya ya Kiteto Mkoani Manyara anashikiliwa na askari polisi wa mkoa huo baada ya kudaiwa kumbaka mtoto mdogo mwenye umri wa miaka sita.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo,mtu huyo Maine Chomora (33) mkazi wa kijiji cha Emarti wilayani Kiteto mkoani humo alimvizia mtoto huyo barabarani na kumfanyia kitendo hicho cha kikatili.

Walisema tukio hilo limetokea  kijijini hapo baada ya mtoto huyo jina lake tunalihifadhi kutumwa dukani na wazazi usiku huo ambapo ilidaiwa kuwa baada ya kukutana na mwanaume huyo alimkamata na kuanza  kumbaka.

Mwangalizi wa haki za binadamu wa kijiji hicho Jackson Mwire alisema alisikia mtoto huyo akilia huku akiomba msaada kwa watu ndipo wakatoka nje na walipofika hapo wakamkuta mtuhumiwa akitenda kitendo hicho.

"Huwezi kuamini kabisa kwani vitendo hivi vimezoeleka hapa Emarti kila tukiwakamata watu hawa baada ya muda mfupi huachiwa na polisi wakidaiwa kuwa hawana hatia,hali hii inatisha sana hapa kijijini," alisema Mwire.

Alisema pamoja na kutolewa elimu kwa umma juu ya madhara ya ubakaji bado jamii imekuwa ikikumbana na mkasa huu ambao wakati mwingine hofu imezidi kutanda kuwa huwenda wanaofanya vitendo hivi ni kutaka kufanya maambukizi ya Ukimwi.

Mwire alisema pamoja na mtuhumiwa kukutwa akitenda kosa hilo wazi wazi baada ya muda utamwona akidunda mitaani huku akitapa kuwa mbona yupo huru na hajafungwa na kudai vitendo hivi vinawakatisha tamaa wananchi.

Katika hatua nyingine Mwire ameiomba Serikali pamoja na mahakama kusimamia sheria vizuri hasa pale wanapokamatwa watu juu ya matukio hayo na uchunguzi ufanyike haraka na kufikishwa mahakamani ili sheria ichukuwe mkondo wake.

Kwa upande wake Maulidi Kijongo mwananchi wa wilayani Kiteto aliliambia blog hili kuwa moja ya sababu ya kutotokomezwa vitondo hivyo ni pamoja na kukithiri kwa rushwa kwa wasimamizi wa sheria hizo.

Alisema kila jambo ama tatizo linaloibuka ndani ya jamii linakuwa kwa baadhi ya viongozi kuwa ni chanzo cha mapato yao hivyo hata kama kutakuwa na jitihada gani bado hali itazidi kuendelea hadi maadili ya kitanzania yarejeshwe.

"Ukienda Polisi na tatizo lako kuingia ni bure kutoka ni pesa hivyo ili hali hii iishe na kufanya vitendo hivi visiendelee lazima turudishe maadili ya Kitanzania ambayo awali yalikuwa msaada mkubwa kwetu," alisema Kijongo.

No comments:

Post a Comment