Wednesday, May 9, 2012

RAIS ATEUA WAKUU WA WILAYA NA KUWAACHA WAKONGWE 51

RAIS Jakaya Kikwete amefanya mabadiliko ya wakuu wa wilaya kwa kuteua vijana wengi wenye umri wa kati ya miaka 30 na 45 na wanawake 43, huku akiwaacha wakuu wa zamani 51.

Katika uteuzi huo uliotangazwa jana na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, ofisini kwake Dar es Salaam, Rais aliteua wakuu wa wilaya wapya 70 na kurudisha wa zamani 63.


Kabla ya uteuzi huo, Tanzania Bara ilikuwa na wilaya 114 na baada ya kutangazwa wilaya mpya 19, sasa kuna wilaya 133.


“Wakuu wa wilaya 51 wa zamani wameachwa kwa sababu mbalimbali zikiwamo za umri, maradhi, utendaji na nyinginezo,” alisema Pinda na kuongeza:


“Katika uteuzi huo, Rais amebakiza wakuu wapya wa wilaya 63, na kuteua wakuu wapya 70. Katika hawa, baadhi ya ma-DC ni vijana wenye umri wa kati ya miaka 30 hadi 45, yaani wengi ni vijana.


“Pia katika kusukuma ajenda ya akinamama, tumejaribu kuwapa nafasi wanawake wengi, wapo 43 sawa na asilimia 30 na zaidi,” alifafanua Waziri Mkuu katika mkutano wake na wahariri wa vyombo vya habari.


Aidha, Waziri Mkuu alisema katika uteuzi huo, kwa mara ya kwanza wameteuliwa wakuu wa wilaya ambao ni wabunge. Idadi yao ni watano, wote wa viti maalumu; Lucy Mayenga anayekwenda Uyui, Subira Mgalu (Muheza), Martha Umbulla (Kongwa), Rosemary Kirigini (Meatu) na Agnes Hokororo (Ruangwa).


Wabunge hao ni wa viti maalumu wa Shinyanga anakotoka Mayenga; Mgalu (Pwani), Umbulla (Manyara), Kirigini (Mara) na Hokororo (Mtwara).


Waziri Mkuu alisema mchakato wa uteuzi wa wakuu hao ulichukua muda mrefu kwa sababu ilikuwa kazi nzito iliyohitaji kujiridhisha, kwa sababu ya idadi kubwa ya wilaya baada ya kuanzishwa kwa wilaya mpya, hivyo kuangalia ni nani aende wapi.


Mbali ya wabunge hao wa viti maalumu, pia Rais aliteua wabunge wa zamani na baadhi yao walipata kuwa naibu mawaziri.


Wabunge wa zamani ambao baadhi yao walishindwa katika kura za maoni za CCM na wengine katika Uchaguzi Mkuu ni Suleiman Kumchaya (Tabora), Dk. Charles Mlingwa (Siha), Omar Kwaangw (Kondoa), Venance Mwamoto (Kibondo) na Manju Msambya (Ikungi).


Wengine ni Ramadhan Maneno (Kigoma), Benson Mpesya (Kahama), Esterina Kilasi (Wang’ing’ombe), Felix Kijiko (Karatu), Ponsiano Nyami (Tandahimba) na Crispin Meela (Rungwe) ambaye alishindwa katika kinyang’anyiro cha ubunge Vunjo.


Aidha katika uteuzi huo, waandishi wa habari ni miongoni mwa wakuu wapya wa wilaya, ambao ni Naibu Mhariri Mtendaji wa Uhuru Publications, Jacqueline Liana (Magu), Ahmed Kipozi (Bagamoyo), mtangazaji wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Selemani Mzee (Kwimba).


Wengine ni mtangazaji wa ITV ambaye pia ni Katibu Mwenezi wa CCM wa Mkoa wa Arusha, Novatus Makunga (Hai) na aliyepata kuwa Mhariri Mtendaji wa New Habari (2006) Limited, Muhingo Rweyemamu.


Wakuu wengine wapya wa wilaya ni Mwenyekiti wa UWT wa Mkoa wa Dodoma na Mkurugenzi wa asasi ya Women Work Up, Fatuma Toufiq (Manyoni), Mboni Mgaza (Mkinga), Hanifa Selungu (Sikonge) na Christine Mndeme (Hanang).


Wengine ni Shaibu Ndemanga (Mwanga), Dk. Nasoro Hamidi (Lindi), Farida Mgomi (Masasi), Jeremba Munasa (Arumeru), Majid Mwanga (Lushoto) na Elias Tarimo (Kilosa).


Wamo pia Alfred Msovella (Kiteto), Dk. Leticia Warioba (Iringa), Dk. Michael Kadeghe (Mbozi), Karen Yunus (Sengerema), Hassan Masala (Kilombero), Bituni Msangi (Nzega), Ephraem Mmbaga (Liwale) na Antony Mtaka (Mvomero).


Walioteuliwa wengine ni Herman Kapufi (Same), Magareth Malenga (Kyela), Chande Nalicho (Tunduru), Seleman Liwowa (Kilindi), Josephine Matiro (Makete), Gerald Guninita (Kilolo), Senyi Ngaga (Mbinga), Mary Tesha (Ukerewe), Rodrick Mpogolo (Chato), Christopher Magala (Newala) na Paza Mwamlima (Mpanda).


Wapya wengine ni Richard Mbeho (Biharamulo), Joshua Mirumbe (Bunda), Constantine Kanyasu (Ngara), Yahya Nawanda (Iramba), Ulega Abadallah (Kilwa), Paul Mzindakaya (Busega), Festo Kiswaga (Nanyumbu), Wilman Ndile (Mtwara) na Joseph Mkirikiti (Songea).


Wengine ni Elibariki Kingu (Kisarawe), Sauda Mtondoo (Rufiji), Gulamhusein Kifu (Mbarali), Regina Chonjo (Nachingwea), Wilson Nkhambaku (Kishapu) na Hafsa Mtasiwa (Pangani).


Orodha hiyo pia inao Rosemary Senyamule (Ileje), Luteni Kanali Ngemela Lubinga (Mlele), Iddi Kimanta (Nkasi), Amani Mwenegoha (Bukombe) na Mrisho Gambo (Korogwe) ambaye ni Mjumbe wa Baraza Kuu la UVCCM na mgombea wa ubunge wa Afrika Mashariki mwaka huu.


Kwa upande wa ma-DC wa zamani waliorudi na ambao baadhi yao wamebaki katika vituo vyao vya zamani na wengi kuhamishwa ni James Millya (Longido), Mathew Sedoyeka (Sumbawanga), Fatuma Kimario (Igunga), James Yamungu (Serengeti), Abdallah Kihato (Maswa), Sarah Dumba (Njombe) na Jowika Kasunga (Monduli).


Wengine ni Betty Mkwasa (Bahi), Issa Njiku (Misenyi), John Henjewele (Tarime), Elias Lali (Ngorongoro), Raymond Mushi (Ilala), Francis Miti (Ulanga), Evarista Kalalu (Mufindi) na Mariam Lugaila (Misungwi).


Pia Anna Magowa (Urambo), Anatory Choya (Mbulu), Fatma Ally (Chamwino), Deodatus Kinawiro (Chunya), Ibrahim Marwa (Nyang’hwale), Dk. Norman Sigalla (Mbeya), Moshi Chang’a (Mkalama), Jordan Rugimbana (Kinondoni) na Georgina Bundala (Itilima).


Wengine ni Halima Kihemba (Kibaha), Manzie Mangochie (Geita), Abdula Lutavi (Namtumbo), Zipporah Pangani (Bukoba), Dk. Ibrahim Msengi (Moshi), Cosmas Kayombo (Kakonko), Lembris Kipuyo (Muleba), Elinasi Pallangyo (Rombo), Queen Mlozi (Singida).


Wamo pia Juma Madaha (Ludewa), Angelina Mabula (Butiama), Hadija Nyembo (Uvinza), Ernest Kahindi (Nyasa), Peter Kiroya (Simanjiro), John Mongella (Arusha), Baraka Konisaga (Nyamagana), Husna Mwilima (Mbogwe) na Sophia Mjema (Temeke).


Wengine ni Francis Isaac (Chemba), Abihudi Saideya (Momba), Khalid Mandia (Babati), Anna Nyamubi (Shinyanga), Danhi Makanga (Kasulu), Amina Masenza (Ilemela), Mercy Silla (Mkuranga), Christopher Kangoye (Mpwapwa), Edward Lenga (Kalambo) na Halima Dendego (Tanga).


Pia Lephy Gembe (Dodoma), Saidi Amanzi (Morogoro), Jackson Msome (Musoma), Elias Goroi (Rorya), Benedict Kitenga (Kyerwa), Erasto Sima (Bariadi), Nurdin Babu (Mafia), Khanifa Karamagi (Gairo), Gishuli Charles (Buhigwe), Saveli Maketta (Kaliua) na Darry Rwegasira (Karagwe).


Waziri Mkuu alisema wakuu hao wa wilaya wanapaswa kwenda kuapishwa ndani ya wiki moja na baada ya wiki mbili kutakuwa na mafunzo maalumu kwao wilaya, wakuu wote wa mikoa na makatibu tawala wote ambayo itafanyika Dodoma.


Alisema hiyo si semina, bali ni mafunzo kwa mfumo wa darasa, ili kuwa na umakini katika kazi zao na kutimiza wajibu na majukumu yao ipasavyo, kwa nia ya kuhakikisha kazi zinakwenda kwa ufanisi.


“Haya ni mafunzo na si semina, ni mfumo wa darasani na nimewambia Tamisemi ikibidi kuwe na mitihani…nia ni kuhakikisha wanakuwa makini na kazi zao na wanatimiza wajibu wao ipasavyo,” alisema Waziri Mkuu.


Alisema nia ni kuhakikisha wakuu hao wa wilaya na mikoa wanasimamia vyema shughuli za maendeleo kama inavyopasa, ili halmashauri ziwe na mipango mizuri ya maendeleo.


Akizungumzia suala la aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Gabriel Kimolo kujiuzulu wadhifa, alisema Kimolo hakujiuzulu, bali alishajulishwa kwamba hatakuwamo katika uteuzi huo wa wakuu wapya wa wilaya.


“Mzee (Rais) alitueleza kuwa tuwajulishe watu watakaoachwa, hivyo kazi hiyo ilifanyika Machi mwaka huu…pamoja na ndugu yangu Kimolo, wote waliarifiwa kuhusu hilo, lakini bado akatangaza kwamba amejiuzulu. Hili kidogo linachanganya, inasikitisha. Huyu aliondolewa, akakimbilia amejiuzulu, kwa lipi?” Alihoji Pinda.


Uteuzi huo unakamilisha miezi kadhaa ya baadhi ya wilaya kutokuwa na watendaji hao tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu baada ya baadhi yao kujitosa katika ubunge na kushinda na wengine kupandishwa vyeo na kuwa wakuu wa mikoa baada ya kuanzishwa kwa mikoa minne mipya ya Simiyu, Njombe, Katavi na Geita

No comments:

Post a Comment