Mwenyekiti wa Jumuiya ya madaktari Tanzanina Dk Steven Ulimboka akiwa amejeruhiwa
NI
unyama. Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk Steven Ulimboka
ametekwa na watu wasiojulikana, kupigwa na kujeruhiwa sehemu mbalimbali
za mwili, kisha kutupwa katika Msitu wa Pande, nje kidogo ya jiji Dar
es Salaam.Daktari huyo ambaye amekuwa akiratibu mgomo wa madaktari
unaoendelea, aliokotwa na msamaria mwema akiwa amefungwa mikono na miguu
akiwa katika hali mbaya.
Baada ya kuokotwa na wasamaria wema na
kufikishwa katika Kituo cha Polisi, Dk Ulimboka aliwahishwa katika
Taasisi ya Mifupa Muhimbili (Moi) kwa matibabu, na ilielezwa kuwa hali
yake haikuwa nzuri.
Taarifa za kujeruhiwa kwa Dk Ulimboka zilisambaa kwa kasi katika vyombo vya habari, mitandao ya kijamii na ujumbe mfupi wa simu.
Kutokana
na tukio hilo, wanaharakati wa haki za binadamu wameituhumu Serikali
kuhusika na tukio hilo, huku Serikali ikikana tuhuma hizo, na papohapo
ikiagiza Jeshi la Polisi kuwasaka waliohusika.
Akisimulia mkasa
huo kupitia Kituo cha Redio cha Clouds FM, Dk Ulimboka alisema tukio
hilo lilitokea usiku wa kuamkia jana katika klabu ya Leaders jijini Dar
es Salaam, alikokuwa na wenzake wawili.
Alisema baada ya kukaa kwenye baa hiyo kwa muda, alianza kujisikia vibaya tofauti na siku zingine.
"Mara,
katikati ya maongezi tukaona mtu anaongea na simu. Ghafla tukiwa
tunasema tuagane, wakaja watu kama watano hivi na bunduki, wakasema wewe
na yule bwana mko free (huru), tunakuchukua wewe (Dk. Ulimboka),"
alieleza na kuongeza,
"Sijakaa sawa, nikaona nimeshaburutwa
nikaanguka kwenye lami, wakaniinua na kuniingiza kwenye gari nyeusi,
lakini ilikuwa haina namba."
Taarifa zaidi zilizolifikia
Mwananchi kutoka Moi alikolazwa kwenye chumba cha uangalizi maalumu,
zilieleza kuwa baada ya uchunguzi, ilibainika kuwa daktari huyo aliteswa
vibaya, ikiwamo kuumizwa sehemu za siri, kuvunjwa meno kadhaa, mbavu na
miguu.
Habari zaidi zilisema kuwa, baada ya kufikishwa katika
Msitu wa Pande na kupata kipigo, alizimia kwa muda na alipozinduka
aliwachomoka watekaji hao na kujaribu kukimbia.
Msitu wa Pande
ulioko wilayani Kinondoni, ndiko wafanyabiashara watatu wa madini kutoka
Mahenge, Morogoro na dereva teksi wa Manzese Dar es Salaam waliuawa na
polisi mwaka 2006.
Chanzo chetu cha habari kilisema, baada ya Dk
Ulimboka kujaribu kuwatoroka watekaji, walipiga risasi mbili hewani,
aliposimama wakamshika na kumpa kipigo na mateso zaidi, hivyo
kusababisha avunjike maeneo mbalimbali ya mwili.
Polisi waunda tume Jeshi la Polisi limeunda jopo kuchunguza tukio la utekaji nyara na shambulio la kudhuru mwili wa Dk Ulimboka.
Kamanda
wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema jana
kuwa tukio hilo ni la aina yake na kwamba halijawahi kutokea hapa
nchini.
Alisema jopo hilo ambalo linaongozwa na Kamishna Msaidizi wa Polisi, Ahmed Msangi linahusisha wapelelezi wa fani mbalimbali.“Ni
issue (jambo) ambayo imetokea bila kutegemea katika namna ambayo ina
utata, hivyo kazi yetu ni kutegua utata huo,” alisema Kova na kuongeza:
“Hatutaki katika nchi yetu matukio kama haya yawe ya kawaida, tunataka liwe la mwanzo na la mwisho.”
Kamanda huyo alisema yeye alipata taarifa za kutekwa Dk Ulimboka usiku wa kuamkia jana saa 7 usiku.
Kwa
mujibu wa Kamanda Kova, Dk Ulimboka aliokotwa na raia mwema katika eneo
la Msitu wa Pande jana saa 2:30 asubuhi karibu na barabara huku akiwa
na majeraha sehemu mbalimbali za mwili, ikiwamo kichwani na mikononi.
Alisema
raia huyo (jina limehifadhiwa) alitoa taarifa katika Kituo cha Polisi
Bunju, na askari walikwenda kwenye gari la raia huyo na kumkuta Dk
Ulimboka wakamchukua na kwenda naye ndani.
Kova alisema:
“Aliyemuokota alisema alimkuta amefungwa mikono na miguu, na inaonekana
kama watu hao walikuwa wanalipiza kisasi.”
Kwa mujibu wa kamanda
huyo, akiwa kituoni hapo, Dk Ulimboka alijieleza kwamba juzi saa 5:30
usiku akiwa katika klabu ya Leaders na wenzake wanapata vinywaji pamoja
na wateja wengine, walikuja watu watano na kuwatishia.
Alisema
watu hao waliwataka walale chini na kwamba walitii, kisha watu hao
walimchukua Ulimboka na kuwaambia wengine waendelee na vinywaji.
“Ulimboka
alisema watu hao walikuwa na gari aina ya Escudo lenye rangi nyeusi na
hili gari halikuwa na namba na walichukua ufunguo wake wa gari, nyaraka
kadhaa na hela alizokuwa nazo,” alisema Kova.
Alisema akiwa katika
gari hilo na watu wengine watano, ghafla walianza kumpiga huku wakiwa
hawasemi chochote na kwamba baadaye walimfunika kichwani na fulana
nyeusi hadi Msitu wa Pande.
Kova alisema baada ya maelezo hayo, Dk
Ulimboka alitoa namba za simu za rafiki yake Dk Deogratius, na baada ya
hapo alipewa fomu ya matibabu (PF3) na kupelekwa katika Hospitali ya
Taifa Muhimbili (MNH) kwa matibabu.
Kamanda huyo alitoa wito kwa
wananchi na mtu yeyote mwenye taarifa kamili kuhusu tukio hilo atoe
taarifa, kwani lisipojulikana vizuri linaweza kuzua minong’ono mingi.
Askari ajeruhiwa MNH Katika
hatua nyingine, Kova alisema watu wasiojulikana wamemjeruhi Mkuu wa
Upelelezi wa Kituo cha Polisi cha Selander Bridge ambaye alikwenda MNH
kufanya upelelezi wa tukio hilo.
Kwa mujibu wa Kova, Mkuu huyo wa
upelelezi alijeruhiwa wakati akiwa anaongea na simu, na kwamba watu hao
pia walimpora vitu alivyokuwa navyo ikiwemo simu. Mkurugenzi Moi
Mkurugenzi
wa Tiba katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (Moi), Cuthbert Mchalo
alisema majeruhi huyo alifikishwa hospitalini hapo saa 4:25 asubuhi,
kwa msaada wa gari la wagonjwa la Kampuni AAR, kutoka Kituo Kidogo cha
Polisi Bunju.
“Tumempokea, anaendelea vizuri na amepata maumivu
katika maeneo ya kifuani, kichwani na tumboni,” alisema na kuongeza kuwa
taarifa zaidi zitatolewa baadaye.
Alifafanua kwamba kwa sasa
wanajitahidi kumpatia matibabu, ingawa alipelekwa hospitalini hapo akiwa
katika hali ambayo siyo nzuri, na uchunguzi zaidi unaendelea.
Wanaharakati walaumu Serikali Miongoni
mwa watu wa kwanza kufika katika Kituo cha Polisi Bunju kumuona Dk
Ulimboka ni Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC),
Dk Hellen Kijo-Bisimba ambaye alisema kilichotokea kinaonyesha jinsi
gani Serikali ilivyo na woga katika kushughulikia matatizo ya wananchi.
Dk
Bisimba alisema wao wanaamini kuwa tukio hilo lina mkono wa Serikali na
kama ni kinyume cha hapo, basi inapaswa kuwaridhisha wananchi kuwa
hawana mkono wao katika sakata hilo.
“Kama wao hawana mkono wao
basi wanapaswa kuwaridhisha wananchi kuwa hawahusiki kwa kuwatia mbaroni
wahusika na kuwafikisha katika vyombo vya sheria,” alisema Bisimba.
Mkurugenzi
huyo alisema matamshi ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda bungeni jana kuwa
wanashughulikia suala la madaktari na watalimaliza liwalo na liwe
inaleta tafsiri kuwa kilichotokea kina mkono wao.
“Alivyosema
liwalo na liwe na kinachotokea sasa kinabainisha kuwa mengi zaidi
yatafuata,” alisema Bisimba na kuongeza kuwa hali hiyo inasikitisha na
haikuwahi kufikiriwa.
Bisimba alisema baada ya wasamaria kumkuta
mnamo saa 12:00 asubuhi, walimpeleka katika kituo kidogo cha Polisi cha
Bunju ambako polisi walifungua mashtaka ya wizi wa maungoni na kupatiwa
RB yenye namba BJ/RB/1870/2012.
“Mimi nilipata taarifa za kutekwa
kwake kutoka kwa mwenzie aliyekuwa naye mnamo saa nane usiku, na baada
ya kupata taarifa hizo niliwaeleza wanaharakati wenzangu juu ya hatua za
kuchukua,” alisema Bisimba.
Bisimba alisema aliwasili katika
Kituo cha Polisi cha Bunju, jana mapema asubuhi na kumkuta Dk Ulimboka
akiwa amejeruhiwa vibaya, lakini hakuwa amepatiwa huduma yoyote.
“Tulikwenda
kumchukua na kukuta hali yake ni mbaya, lakini cha ajabu pamoja na
majeraha yote hakupatiwa msaada wowote wa huduma, jambo ambalo
lilitusikitisha sana,” alisema.
Kwa upande wake Mkurugenzi
Mtendaji wa Taasisi ya Sikika, Irenea Kiria alisema kilichotokea ni kitu
kibaya na kinaonyesha jinsi gani Serikali inavyoshughulika na watu,
badala ya kujali hoja za msingi ambazo zinawasilishwa.
Kiria
alisema hoja za madaktari zilipaswa kusikilizwa kwani licha ya madai ya
masilahi yao lakini pia wanapigania mazingira bora yenye utu kwa ajili
ya wagonjwa.
Madai mengine ni upatikanaji wa dawa na vifaa tiba
kwa ajili ya kuwahudumia wananchi pamoja na upatikanaji wa dawa, mambo
ambayo alisema hayahitaji mjadala.
“Suala la masilahi ya
madaktari linazungumzika lakini siyo suala la dawa, mazingira bora ya
kuwahudumia wagonjwa na upatikanaji wa vifaa tiba na vipimo vingine,”
alisema Kiria.
Nchimbi: Tutawasaka Kwa upande
wake Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi alisema Serikali
imeliagiza Jeshi la Polisi kuwasaka na kuwachukulia hatua watakaobainika
kuhusika na utekaji huo.
Dk Nchimbi alisema mjini Dodoma kuwa
Serikali haihusiki kwa namna yoyote ile na utekaji nyara huo, na kwamba
kitendo hicho kinapaswa kulaaniwa kwani hakikubaliki katika jamii hasa
kwa zama hizi.
“Kwanza, madaktari ni watu muhimu ambao wao ndio
wanaotuwezesha sisi kuishi, kwa hiyo wapo kwa ajili ya maisha yetu, hata
kama asingekuwa daktari, kwa mtu yeyote yule, jambo hili halikubaliki
katika nchi yetu,” alisema Dk Nchimbi na kuongeza:
“Tumewaagiza
polisi wafanye uchunguzi ili kuwabaini wahusika na wakipatikana
wafikishwe katika vyombo vya sheria, maana hatuwezi kwa namna yoyote
kuvumilia vitendo vya aina hii.”
Alisema Serikali imestushwa
sana na tukio hilo na haitavumilia kwa namna yoyote vitendo hivyo pamoja
na vile vya unyanyasaji kwani ni kinyume cha sheria.
Kuhusu
kupigwa kwa Mkuu wa Upelelezi (OC- CID), ASP Mukiri, Dk Nchimbi alisema
lilikuwa ni tukio la bahati mbaya kwamba madaktari waliokuwapo Muhimbili
walishindwa kuwa na uvumilivu kwani askari aliyepigwa alikuwa ameagizwa
na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela kwenda
kufuatilia matibabu ya Dk Ulimboka.
“Hapa ndipo ninapotofautiana
na watu wengi, mnampigaje polisi, maana yule anapaswa kuwa rafiki wa
raia, sasa unampigaje mtu ambaye ni mlinzi na umemwajiri, analipwa kwa
kodi yako?” alihoji Dk Nchimbi.
Yaliyojiri bungeni Tukio
hilo lililosambaa kwa kasi katika mitandao ya kijamii na vyombo vya
habari, liliibuka bungeni, ambako Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee
alilaani vikali kitendo cha watu wanaodaiwa ni maofisa wa vyombo vya
usalama kumpiga Dk Ulimboka.Alisema kitendo hicho ni unyama unaostahili
kukemewa na kila mpenda amani hapa nchini.
“Tumestushwa na tukio
hilo na tunalaani vikali kitendo hicho na kumwombea Dk Ulimboka ili
apone haraka,” alisema Mdee.Katika hatua nyingine, Mwananchi
lilitembelea hospitali za Mwananyamala, Temeke na Amana, kujionea hali
ilivyokuwa baada ya kusambaa kwa taarifa za kupigwa kwa Dk Ulimboka.
Katika
hospitali ya Mwananyamala, wengi walioonekana walikuwa ni wauguzi huku
madaktari wakidaiwa kwenda katika hospitali ya Muhimbili kumuona mwenzao
aliyejeruhiwa.
Dk Ulimboka aliwahi kufanya kazi katika hospitali hiyo ya Mwananyamala katika miaka ya nyuma.
Hata
hivyo, juhudi za waandishi kuzungumza na uongozi wa hospitali hiyo,
hazikufanikiwa baada ya wafanyakazi wa Ofisi ya Mganga Mkuu kusema kuwa
mganga huyo amekataa kuzungumza, akiwataka waandishi wafike ofisini
kwake leo.
“Ameniambia niwapeleke kwa katibu wake, lakini na yeye
nimemkosa, sasa nimerudi kwake ameniambia niwaambie mrudi kesho,”
alisema katibu muhtasi wake.
Katika hospitali za Temeke na Amana,
hali pia ilikuwa hivyo, baadhi ya wahudumu waliokutwa katika hospitali
hizo wakikataa kuzungumza kwa madai kuwa wanaotakiwa kuzungumza hawapo.
Madaktari jeshini waitwa kazini Taarifa
zilizotufikia wakati tukienda mitamboni, ambazo hazijathibitishwa,
zilieleza kwamba madaktari wote wanaofanya kazi kwenye hospitali za
jeshi ikiwamo Lugalo ambao hawakuwa zamu jana jioni, waliitwa kazini,
tukio ambalo linahusishwa na tamko la Serikali linalotarajiwa kutolewa
leo. |
No comments:
Post a Comment