Rais Jakaya Kikwete
NI YA KUJITATHIMINI KATIKA MKUTANO WA AU,KISA MADENI
RAIS
Jakaya Kikwete amezuiwa kuwasilisha taarifa ya Tanzania kuhusu
utekelezaji wa mpango wa Mpango wa kujitathmini wa Umoja wa Afrika
(APRM), kwa sababu ya madeni makubwa yanayotokana na kutowasilishwa kwa
michango kwa ajili ya uendeshaji wa sekretarieti ya mpango huo.Tanzania
inadaiwa kiasi cha Dola za Marekani 800,000 sawa na Sh1.258 bilioni kwa
kuzingatia viwango vya kubadilisha fedha (exchange rate) vya Benki Kuu
ya Tanzania (BoT) ambavyo ni wastani wa Sh1, 572.87 dhidi ya Dola ya
Marekani.
Deni hilo ambalo ni malimbikizo ya ada ya Dola 100,000
kila mwaka kwa miaka minane mfululilizo tangu mwaka 2005 ni kashfa kwa
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa inayoongozwa na
Waziri Benard Membe, ambayo mpango wa APRM unatekelezwa chini yake.
Julai
22 mwaka jana, wakati akiwasilisha makadirio ya wizara yake, Membe
alisema taarifa kamili ya mchakato huo hapa nchini ilitarajiwa kuwa
imekamilika na kuwasilishwa katika Mkutano Mkuu wa nchi wanachama wa
APRM Julai, 2012. Ni kwa mantiki hiyo, Rais Kikwete alitarajiwa
kuwasilisha ripoti ya Tanzania kwenye mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Umoja
wa Afrika (AU) utakaofanyika Lilongwe, Malawi Julai 10 mwaka huu, lakini
habari zinasema deni hilo limekwaza mpango huo.
Katibu Mtendaji
wa APRM Tanzania, Rehema Twalib alisema jana: “Ni kweli kwamba tunadaiwa
Dola 800,000 ambazo ni kama Sh1.2 bilioni na kidogo hivi na hizo ni
malimbikizo ya mwaka huu wa 2012 na miaka mingine ya nyuma kwa sababu
kila mwaka tunatakiwa kulipa Dola 100,000.”
Habari zilizopatikana
baadaye na kuthibitishwa na Twalib zinasema tayari APRM Tanzania
imepokea waraka kutoka Sekretarieti ya APRM na AU makao makuu kwamba
ripoti ya Tanzania haitaweza kuwasilishwa katika mkutano huo wa
Lilongwe.
“APRM nadhani wamepokea barua kutoka makao makuu kwamba
Rais wetu hataweza kuwasilisha ripoti ya Tanzania, lakini hawa jamaa ni
wajanja sana hawakueleza sababu ila wameambatanisha na orodha ya madeni
tunayodaiwa kama nchi,”alisema mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Bunge ya
Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama na kuongeza:
“Hii ni aibu kwa
Tanzania, wenzetu wanatushangaa kwamba sisi tumekuwa nyuma katika mambo
haya yanayohusu Utawala Bora wakati sisi ndiyo tulitarajiwa kuwa msitari
wa mbele kuliko wengine.” Twalib katika maelezo yake alikiri kwamba
Rais Kikwete hatawasilisha ripoti ya Tanzania kwenye mkutano huo wa
Lilongwe lakini akasema hilo halihusiani moja kwa moja na deni nchi
inalodaiwa.
“Kweli walileta taarifa hiyo kwamba taarifa yetu
haitawasilishwa kwenye mkutano ujao, lakini ni kwa sababu ya mchakato
wenyewe kuwa mrefu, lazima ipitie kwenye ngazi mbalimbali na kwa
kungalia muda uliobaki pengine waliona kuwa hautatosha kukamilisha hatua
zote,” alisema Katibu Mtendaji huyo.
Sehemu ya taarifa ya APRM
Tanzania iliyowasilishwa kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya
Chama cha Mapinduzi (NEC- CCM), Mei 15 mwaka huu, mjini Dodoma inaeleza
kuwapo kwa kusudio miongoni mwa nchi zinazoshiriki mchakato wa APRM
kuziengua zile zisizolipa madeni yake.
“Tanzania imeshindwa kulipa
ada zake za kila mwaka kwa Sekretarieti ya AU/APRM kwa miaka saba
iliyopita. Baadhi ya nchi zimeanza wanachama wa mchakato huu zimeanza
kujenga hoja kwamba nchi kama Tanzania ziondolewe kwenye mchakato
huu,”inaeleza sehemu ya taarifa hiyo. Hata hivyo, Twalib alisema
licha ya kwamba Tanzania inapaswa kulipa madeni yake, lakini hakuna
kipengele chochote kinachoipa Sekretarieti ya APRM mamlaka ya kuizuia
nchi kutathminiwa katika mkutano wa wakuu wa nchi. Alikiri kuwa deni
hilo linachafua taswira ya Tanzania mbele ya nchi nyingine na kwamba
lazima yalipwe kwani ilijiunga kwa hiari na kusaini makubaliano ya kutoa
michango husika.
Deni la Tanzania Rais Kikwete alipata
taarifa za Tanzania kudaiwa na APRM katika kikao cha (NEC- CCM) Mei 15,
mwaka huu mjini Dodoma na inaelezwa kwamba zilimsutua.
Habari
kutoka ndani ya kikao hicho zinasema kuwa Rais alishangazwa na taarifa
hizo hivyo kuagiza mchakato wa malipo ya deni hilo uanze mara moja:
“Kweli Rais alionyesha kushangazwa na deni hilo na aliagiza kwamba fedha
hizo zilipwe kesho yake,” alisema mmoja wa wajumbe wa NEC.
Hata
hivyo, haifahamiki iwapo agizo hilo la Rais lilitekelezwa au la kwani
wiki mbili tangu atoe maelekezo hayo ndipo APRM Tanzania walipopata
taarifa kutoka AU kwamba ripoti ya Tanzania haitaweza kuwasilishwa.
Taarifa
iliyowasilishwa NEC ambayo Mwananchi limeiona, inaonyesha kuwa katika
mwaka wa fedha wa 2012/13 APRM Tanzania wameomba kuidhinishiwa kiasi cha
Sh5.194 bilioni kwa ajili ya kugharamia kazi zake lakini maombi
yaliyowasilishwa Hazina na wizara kwa ajili ya mango huo ni Sh1.149
bilioni tu.
“Kwa upande mwingine kama fedha tulizoomba Sh5,194,
204,304 zingeidhinishwa, tungeweza kutekeleza majukumu yetu kama
yalivyopangwa kwa kuzingatia mahitaji ya kitaifa ikiwa ni pamoja na
kulipa limbikizo la deni la Sh1.280 bilioni ambalo halijalipwa kwa miaka
saba,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Taarifa hiyo inaonyesha
kwamba kiwango kinachopendekezwa kuidhinishwa na Bunge kinaweza
kutosheleza kugharamia kazi za mchakato wa APRM nchini kwa miezi mitatu
na kidogo ikilinganishwa na kile kilichoidhinishwa katika mwaka wa fedha
unaoishia Juni 30, mwaka huu ambacho ni Sh 2.04 bilioni. Tanzania
pia inatajwa kwenye taarifa ya Sekretarieti ya APRM ya mwaka 2010 kwamba
ni miongoni mwa nchi ambazo zimewahi kuwasilisha michango yake mara
moja tu tangu iliposaini na kuridhia kushiriki kwenye mchakato wa
kutathminiwa utendaji wake.
Nchi nyingine ambayo imewahi kulipa
michango yake mara moja ni Sierra Leone wakati Jamhuri ya Kidemokrasi ya
Kongo (DRC), Djibouti, Sudani na visiwa vya Sao Tome na Principe
hazijawahi kutoa mchango wowote.
Tanzania ni nchi pekee katika
kanda ya Afrika Mashariki na Kati inayodaiwa fedha nyingi ililinganishwa
na majirani zake ambazo zinadaiwa kiasi cha fedha kwa Dola za Marekani
kwenye mabano, Rwanda (300,000), Zambia (200,000), Kenya (100,000) na
Uganda (400,000). Waziri Kivuli wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Ezekia Wenje katika maoni ya Kambi ya Upinzani Bungeni, Julai
22 mwaka jana alihoji sababu za Serikali kushindwa kulipa deni hilo
ambalo alisema linalitia aibu taifa.
“Deni la nchi yetu katika
Sekretarieti ya APRM ngazi ya Bara la Afrika na malimbikizo yanafikia Sh
1.07 bilioni. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuthibitisha
taarifa hizi na kujieleza ni kwa nini kwa kipindi chote hicho haikulipa
ada ya uanachama APRM na lini italipa fedha hizo, kwani hii ni aibu
kubwa kwa Taifa,” alisema Wenje.
APRM Tanzania Mchakato wa
kujitathini wa nchi za Afrika ulibuniwa na viongozi wa Afrika mwaka
2002, taasisi hiyo ilianza rasmi mwaka 2003 baada ya idadi ya wanachama
iliyotakiwa kusaini mkataba huo kutimia.
Kwa upande wa Tanzania,
Kamati ilibaini Taarifa Rasmi za Bunge (Hansard) zinaonyesha kuwa mpango
huo uliridhiwa na Bunge la Nane, Februari 1, 2005, katika kikao cha
Kumi cha Mkutano wake wa 14 na kupitisha Azimio la kuridhia Mkataba wa
Tanzania kujiunga na Utaratibu wa African Peer Review Mechanism.
Kamati
ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama katika taarifa yake mwaka
jana ilisema: “Kuna umuhimu mkubwa kwa Serikali kutenga fedha kwa ajili
ya mchakato huo sanjari na kulipia michango na ada ya uanachama kwa
wakati.”
Hivyo hatua ya Tanzania kuzuiwa kuwasilisha taarifa yake
kunaifanya iendelee kuchelewa zaidi kwani tayari muda uliotarajiwa
kukamilisha mchakato huo ulikwishapita.
Wenje katika hotuba ya
upinzani alibainisha kwamba: “Ni dhahiri kuwa nchi yetu imechelewa sana.
Ni dhahiri kuwa Serikali haikutimiza wajibu wake kuhakikisha mchakato
huu wa kujitathmini unatekelezwa kwa wakati kwani takriban miaka sita
imepita tangu Bunge hili lipitishe uamuzi wa kuingia kwenye mchakato wa
APRM, lakini hadi leo hatujaweza kupata ripoti ya mwisho ya APRM kuhusu
nchi yetu.”
“Kwa kawaida kazi ya kujitathmini inapaswa kufanyika
mara moja ndani ya kila miaka mitano, lakini kwa Tanzania huu ni mwaka
wa saba bila kupatikana kwa ripoti ya mwisho. Nchi nyingine kama
Ghana,Uganda na Rwanda tayari zimejitathimini na kupata ripoti zao za
mwisho.” |
No comments:
Post a Comment