Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye
KATIBU
wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye amesema
chama chake hakina mpango wa kuutumia mkutano wake wa leo kwenye Viwanja
vya Jangwani kujibizana na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)
na badala yake, kitajikita zaidi katika kutoa somo kwa wajumbe wapya wa
mashina na viongozi wa matawi Mkoa wa Dar es Salaam. Kauli hiyo
ya Nape inatoa mtazamo tofauti na tetesi kwamba CCM kitatumia mkutano
huo kukijibu chama hicho kikuu cha upinzani ambacho nacho kilifanya
mkutano kwenye viwanja hivyo hivi karibuni. Katika mkutano huo ambao
Chadema kilizindua Mpango wake wa Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) mwishoni
mwa mwezi uliopita, kiliorodhesha shutuma nyingi dhidi ya Serikali ya
CCM zikiwemo za kusababisha maisha magumu kwa Watanzania.
Nape
alisema mkutano huo uliandaliwa na CCM Mkoa wa Dar es Salaam hata kabla
ya huo wa Chadema na lengo lake ni kuwakutanisha viongozi wapya wa chama
hicho tawala na viongozi wa juu wa chama na Serikali, wakiwemo mawaziri
watakaofafanua shughuli zao za kiutendaji. “Mkutano huu unalenga
kuwafundisha wajumbe wa nyumba kumi na viongozi wa mashina
waliochaguliwa hivi karibuni namna ya utendaji wa Serikali, kwa kuwa wao
bado ni wapya kiuongozi na wanahitaji kupewa somo,” alisema Nape.
Alipoulizwa
kama mkutano huo ni moja ya hatua za kufuta nyayo za Chadema hasa baada
ya kuzindua M4C, Nape alisema: “Mkutano huu tuliuandaa mapema kabla
hata ya Chadema hawajafanya mkutano wao. Ila kilichochelewesha ni
Mkutano wa Halmashauri Kuu (Nec) ya CCM,” alisema Nape na kuongeza:
“Mkutano
huu awali, ulikuwa ufanyike ndani ya ukumbi lakini kwa kuwa watu wengi
walipenda kushiriki tumeamua kuufanyia Jangwani ambako wanachama na
viongozi wa CCM watapata fursa ya kusikia sera za viongozi wa chama na
watendaji wa Serikali.”
Aliwataja mawaziri ambao watakuwa katika
mkutano huo kuwa ni pamoja na Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe
ambaye atazungumzia masuala ya usafiri wa reli, bandari na anga na
Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli ambaye atazungumzia masuala ya
miundombinu na barabara.
Wengine ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais
(Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira ambaye atazungumzia hatima ya
Watanzania katika masuala ya ajira na vijana na Naibu Waziri wa
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba ambaye atazungumzia
mipango ya wizara yake.
M4C Mei 25 mwaka huu, Chadema
kilizindua mkakati wake mpya wa ‘Movement For Change-M4C’ ukiwa na lengo
la kukiandaa chama hicho kushinda Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Katika
mkutano huo, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliwataka wanachama
na wananchi kwa ujumla kukichangia fedha chama hicho ili kufanikisha
kampeni aliyoielezea ni ya kukiondoa CCM madarakani mwaka 2015.
Katibu
Mkuu wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa alisema maisha ya Watanzania si
mazuri, vyakula vinaongezeka bei kutokana na Serikali ya CCM kutokuwa
makini hivyo akawataka wabunge wa chama hicho kuibana kupitia Bunge
lijalo la Bajeti.
Aliilaumu Serikali kwa kutotumia vizuri kodi za
Watanzania kwa ajili ya shughuli za maendeleo kwa kuwalipa watumishi
ambao nafasi zao hazina manufaa kwa wananchi. Dk Slaa alilalamikia
kitendo cha kuongeza kodi katika mafuta ya taa ili watu wasichakachue
mafuta ya dizeli akisema ni mwiba kwa Watanzania. |
No comments:
Post a Comment