Sunday, June 10, 2012

Serikali yalipa Sh5 bilioni wafanyakazi hewa 10,000

 
SERIKALI  imepoteza zaidi ya Sh5.4 bilioni kutokana na kulipa mishahara kwa wafanyakazi hewa 9,949 katika kipindi cha miezi mitano iliyopita.Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa alisema vitendo hivyo vimekwamisha utekelezaji wa miradi mingine ya maendeleo ambayo ingegharamiwa kwa fedha hizo.

Kauli ya Dk Mgimwa imekuja ikiwa ni zaidi ya mwaka mmoja tangu Rais Jakaya Kikwete alipotoa agizo la kudhibiti wafanyakazi hewa katika wizara na idara za Serikali.


Machi mwaka jana, Rais Kikwete aliamuru kufanyika kwa ukaguzi katika idara zote za serikali kutokana na kuwapo kwa taarifa kwamba kiasi cha Sh9 bilioni kilikuwa kimelipwa kama mishahara kwa wafanyakazi hewa katika wizara tatu tu za Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Katiba na Sheria na Afya na Ustawi wa Jamii.

Rais alisema wahusika wa vitendo hivyo walipaswa kubainishwa ikiwa ni hatua ya kukomesha mara moja wizi wa fedha za umma kupitia mishahara hewa na kwamba Serikali haipaswi kuwaruhusu watu ambao wameiibia Serikali fedha kuendelea kufanya kazi za umma.

Lakini jana akifungua Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Fedha lililofanyika Dar es Salaam, Dk Ngimwa alikiri kuwapo kwa tatizo hilo, mwaka mmoja tangu kutolewa kwa agizo hilo la Rais Kikwete.

Kutokana na hali hiyo, alisema Serikali imechukua hatua za kukabiliana na ufisadi huo kwa kuweka utaratibu wa orodha ya wafanyakazi kupitiwa kila mwezi.Aliwataka wafanyakazi wenye tabia hiyo kuiacha mara moja akisema Serikali iko makini na itawachukulia hatua kali wahusika wote.

Alisema wiki ijayo itasomwa Bajeti ya Serikali 2012/13 ambayo imezingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 na imelenga ukuaji wa uchumi wa kiwango cha kati, hivyo suala la udhibiti wa mapato ya Serikali halitakuwa na mjadala.

“Tunataka kuleta hali bora ya maisha ya wananchi. Lengo la Serikali ni kila mmoja kupata wastani wa pato la Dola za Marekani 3,000 (Sh3.8 milioni) kila mwezi ifikapo mwaka 2025,” alisema.
Alisema bila udhibiti wa tatizo la mishahara ya wafanyakazi hewa, ni vigumu kufikia lengo hilo hivyo kuwataka wafanyakazi wa wizara hiyo kujipanga vizuri ili lengo hilo lifikiwe.

Alisema wafanyakazi wa Hazina ndiyo wanaobeba jukumu hilo wakati Serikali inajitahidi kupambana na mtikisiko wa kiuchumi hususan kipindi hiki cha kuelekea bajeti.Alisema Serikali imeomba nguvu ya kujiongezea uwezo kutoka mashirika ya kimataifa, nchi za Mashariki ya Kati na Asia.

Awali, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi, Ramadhan Khijjah alisema kuna tatizo la wafanyakazi wa wizara hiyo kuogopa kuzungumza katika vikao vya baraza hilo.

“Watu waoga huogopa kuzungumza. Wanawahofia wakuu wao wa idara jambo ambalo halijengi,” alisema.
Alisema hali hiyo inachangiwa na walio wengi kuogopa kuchukiwa na mabosi wao jambo ambalo alilipinga na kuwatoa hofu akiwataka wawe wazi.

Alisema mabaraza hayo ndiyo sehemu ya kukosoa, kuelekeza na kubainisha kasoro zilizopo ili hatua zichukuliwe na kujenga mshikamano kwa manufaa ya Taifa na jamii kwa ujumla.


No comments:

Post a Comment