SIKU
moja baada ya Jukwaa la Wahariri (TEF) kutokuwa na imani na Wizara ya
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, imekuja juu na kukanusha madai ya
Jukwa la hilo kwamba msuguano baina ya viongozi wakuu wa wizara
unakwamisha kupatikana kwa sheria ya vyombo vya habari nchini.
Kauli
ya wizara imekuja siku moja baada ya TEF kusema hawana imani na Waziri
wa Wizara hiyo, Dk Fenella Mkangala na Katibu Mkuu wake Sethi Kamuhanda,
kama wanaweza kufanikisha kupatikana kwa sheria hiyo kutokana na
msuguano baina yao.
Akizungumza na waandishi wa habari jana
Jijini Dar es Salaam, Kamuhanda alisema hana ugomvi wala msuguano wowote
na waziri wake na kuongeza kuwa wanaelewana na wanafanya kazi vizuri na
kudai kuwa ameshangazwa na taarifa zilizotolewa na vyombo vya habari.
Alisema haiwezekani watu wenye uadilifu wakagombana wakati ni watu makini katika kazi zao na wanaelewana hata kwenye kazi zao.
“Mkumbuke
kuwa sisi hatuna mgogoro wowote kwa sababu waziri kipindi alipokuwa
naibu waziri tulifanya kazi kwa pamoja hivyo nashangaa mimi na waziri
wangu kuona vyombo vya habari vinaripoti kuwa tuna mgogoro kati ya mimi
na waziri,” alisema na kuongeza:
“Mimi sio mtu wa migogoro kwa
watu wanaonifahamu kwa sababu sina sababu ya kugombana na waziri wangu
hili nataka kila mmoja wetu ajue,” aliongeza. Katibu huyo Mkuu
alikiri kupokea mwaliko wa kufungua na kufunga Mkutano wa Mwaka wa
Wahariri wa Vyombo vya Habari pamoja na Baraza la Habari na kusema kuwa
alipata udhuru na kutoa taarifa kwa Katibu Mkuu wa Baraza la Habari
nchini (MCT) Kajubi Mukajanga. “Nilitakiwa nije kwa niaba ya waziri
lakini tukaletewa taarifa za vikao vya kamati ya bunge vinaanza na mimi
ndiye muandaaji mkuu wa vikao hivi, hivyo nilishindwa kuja na nilitoa
taarifa kwa katibu wa MCT lakini nashangaa kuona taarifa hizi zimekuja
tofauti ….muulizeni huyo katibu kama sikuongea naye,” alisema.
Aliongeza: “Mimi nilizungumza nao juu ya hali ya dharura iliyojitokeza kwa hiyo sikuwa na sababu ya kuwakimbia," alisema.
Kufuatia
hatua hiyo katibu huyo mkuu alisema wizara haitachukua hatua yoyote
kuhusiana na taarifa iliyotolewa na Jukwaa la Wahariri pamoja na baraza
la Habari nchini (MCT). Katika hatua nyingine, Serikali imepongeza
jukwaa la Wahariri nchini kwa kuwezesha kazi ya uandishi wa habari
kufanyika kwa kuzingatia maadili, wajibu na waledi wa kitaaluma. Pia
Katibu huyo Kamuhanda alisema Jukwaa hilo kwa kuimarisha weledi wa
kitaaluma, uwajibikaji, utendaji wa kazi, uhuru wa vyombo vya habari
pamoja na kujenga mfumo wa usimamizi wa maadili ndani ya vyombo vya
habari.
Tamko la TEF linatokana na viongozi hao kualikwa kwenye
mkutano huo ambao pamoja na mambo mengine ulijadili Mchakato wa Sheria
ya Haki ya Kupata Habari na Huduma za Vyombo vya Habari nchini, ambao
umekuwa ukisuasua kwa takriban miaka 10 sasa.
Taarifa ya TEF na
kusainiwa na Katibu wake Neville Meena, ilisema azimio hilo lilitolewa
na wahariri watendaji wa vyombo vya umma, vinavyomilikiwa na mashirika
ya dini pamoja na watu binafsi katika mkutano uliofanyika Morogoro kati
ya Juni 3 mpaka 5. Inasema kuwa, vitu vingine muhimu vilivyokuwa
vinajadiliwa ambavyo vilihitaji viongozi kutoka wizarani kuwepo ni
pamoja na, kuwezesha kazi ya uandishi wa habari kufanyika kwa kuzingatia
maadili, wajibu na weledi wa kitaaluma.
Pia kuimarisha weledi
wa kitaaluma, uwajibikaji utendaji wa kazi, na uhuru wa vyombo vya
habari na zaidi kujenga mfumo wa usimamizi wa maadili ndani ya vyombo
vya habari. Taarifa hiyo ilisema kuwa, wanachoomba ni dhana ya
kutekeleza jambo hilo ambayo ni Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari na
Sheria ya Haki ya Kupata Habari, ambazo mchakato wake umedumu kwa zaidi
ya miaka 10 sasa bila kupatikana. |
No comments:
Post a Comment