Mpatanishi wa kimataifa kwenye mzozo wa Syria Kofi Annan amesema kuwa kundi maalumu linaloshughulikia amani ya nchi hiyo litakutana Jumamosi mjini Geneva.
Jukumu la kundi hilo ni kubainisha njia na hatua zinazohitajika kuuwezesha mpango wa amani wenye vipengele sita wa Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kufanikiwa kwa ukamilifu.
Mpango huo unahusisha pia juhudi za kuzifanya pande zote zinazohasimiana nchini Syria kusitisha mapigano ya aina zote.
Katika tamko lake, Annan amesema kwamba amewaalika pia mawaziri wa mambo ya kigeni kutoka mataifa matano yenye nguvu duniani ambayo ni Marekani, Urusi, China, Uingereza na Ufaransa pamoja na Umoja wa Ulaya na nchi nyingine.
Hata hivyo Annan hakuitaja Iran kwenye orodha ya nchi hizo zitakazohudhuria mkutano huo wa Jumamosi.
No comments:
Post a Comment