Waandamanaji wenye hasira
wamekusanyika katika mji mkuu wa Togo, Lome kwa siku ya tatu ya
maandamano wakidai mageuzi ya mfumo wa uchaguzi wanaosema umekuwa
ukipendelea chama tawala.
Katika siku mbili zilizopita kumekosekana
utulivu ambapo nchi hiyo imeshuhudia vurugu kati ya vikosi vya usalama
na maelfu ya waandamanaji ambapo mawe yalirushwa, mabomu ya machozi
kupigwa na kufanya watu wapatao 30 kujeruhiwa.Maandamano hayo yanafuatia mageuzi ya hivi karibuni katika mfumo wa uchaguzi uliofanywa kabla ya uchaguzi baadae mwaka huu.
Waandamanaji wanataka mfumo wa kuruhusu ukomo wa urais.
Togo imekuwa ikiongozwa na viongozi wa familia moja kwa zaidi ya miongo minne.
Rais Gnassingbé alishika madaraka ya nchi hiyo mwaka 2005 kufuatia kifo cha baba yake, Gnassingbé Eyadéma, aliyetawala Togo kwa miaka 38. Alichaguliwa tena mwaka 2010.
Majengo kuharibiwa
Mwandishi wa BBC Ebow Godwin aliyepo katika mji mkuu, Lome, anasema maelfu ya watu wameshiriki katika maandamano hayo.
Polisi wa kutuliza ghasia wamewafyatulia waandamanaji mabomu ya machozi ambao nao walikuwa wakirushiwa mawe, majengo yameharibiwa na matairi kuchomwa moto katika mitaa ya mji mkuu huo.
Polisi angalau 10 na waandamanaji 17 wanasemekana wamejeruhiwa katika siku mbili za awali za maandamano hayo.
Waandamanaji wanataka marekebisho kwenye sheria za uchaguzi ya Togo iliyopitishwa na bunge la nchi hiyo wiki iliyopita, ambayo inaipendelea chama tawala.
Wanaharakati wa Operesheni Save Togo ambayo ni muungano wa makundi wanaharakati walioandaa maandamano hayo, wanasema wataendelea na maandamano hadi Rais Faure Gnassingbé akubali kufanya mazungumzo juu ya kanuni mpya wa uchaguzi pamoja na mapendekezo mengine ya mageuzi ya mfumo wa uchaguzi.
Waandamanaji wanataka Togo ifuate katiba yake ya 1992 ambayo inaweka kikomo cha mamlaka ya rais aliyepo madarakani kwa vipindi viwili.
Katiba ya nchi hiyo ilirekebishwa mwaka 2002 na bunge la nchi hiyo ambalo lina wabunge wengi kutoka chama tawala.
Uchaguzi wa wabunge nchini humo unatarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu, hata hivyo tarehe kamili bado haijapangwa.
No comments:
Post a Comment